TANGAZO


Friday, June 5, 2015

Kesi dhidi ya mawaziri 3 zatupwa Kenya

Keriako Tobiko
Mwendesha mashtaka mkuu nchini Kenya Keriako Tobiko imeagiza kesi ya ufisadi dhidi ya mawaziri watatu na seneta wa jimbo la Nairobi Mike Sonko, kufutiliwa mbali.
Mawaziri hao pamoja na waziri wa kilimo, wa nishati na waziri wa uchukuzi Michael Kamau ambaye alifikishwa mahakamani siku ya alhamisi na kauchiliwa kwa dhamana ya shillingi milioni moja.
Mawaziri hao walisimamishwa kazi na rais Uhuru Kenyatta kufuatia ripoti zilizowahusisha na sakata za ufisadi.
Waziri wa kilimo alituhumiwa kuhusika na njama ya kuidhinisha uagizaji wa sukari bila kufuata sheria naye wa uchukuzi alituhumiwa kuidhinisha kandarasi iliyopewa kampuni moja ya usafirishaji na uagizaji mali.
Naye waziri wa nishati pamoja na seneta wa Nairobi Mike Sonko walikuwa wakichunguzwa kuhusiana na zabuni iliyotolewa na kampuni ya kusafirisha mafuta nchini Kenya, Kenya Pipeline.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na ofisi ya mwendesha mashtaka mkuu, Keriako Tobiko, kesi dhidi ya mawaziri hao zilifulitiliwa mbali kutokana na ukosefu wa ushahidi wa kutosha kuwafungulia mashtaka.
Maafisa wengine ambao kesi zao zimetupiliwa mbali ni pamoja na gavana wa Narok, Samuel Tunai na maafisa wengine saba wa kaunti hiyo ambao walikuwa wakikabiliwa na tuhuma za kutumia mamlaka yao vibaya.
Kesi pia iliondolewa kutokana na ukosefu wa ushahidi wa kutosha.
Taarifa hiyo imesema kuwa jumla ya faili ishirini na nane zimewasilishwa kwa ofisi ya mwendesha mashtaka, sita kati yao zikifungwa kutokana na ukosefu wa ushahidi wa kutosha.
Aidha faili kumi na saba zimeidhinishwa kupelekwa mahakamani, faili mbili nazo zikirejeshwa kwa tume hiyo na mwendesha mashtaka.
Kwa ujumla washukiwa sabini na wanne watafunguliwa mashtaka.
Miezi miwili iliyopita rais Kenyatta aliwasilisha bungeni majina ya maafisa wakuu wa serikali waliotuhumiwa kuhusika na ufisadi na kuwasimamisha kazi wote kwa muda wa miezi miwili.
Orodho hiyo ilikuwa na majina ya mawaziri watano na tayari kesi dhidi ya waziri wa ardhi imetupiliwa mbali. Hatma ya waziri wa leba bado ingali mikononi mwa tume hiyo.
Kwa miongo kadhaa wanaharakati wa kijamii na wafadhili wamelalamikia kukithiri wa ufisadi serikali.

No comments:

Post a Comment