TANGAZO


Friday, May 8, 2015

Mfumuko wa bei nchini waongezeka kidogo - Ofisi ya Taifa ya Takwimu

Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bw. Ephraimu Kwesigabo akitoa taarifa ya kuongezeka kidogo kwa mfumuko wa bei nchini kwa mwezi Aprili 2015 leo jijini Dar es salaam.Mfumuko wa Bei kwa Mwezi Aprili 2015 umefikia asilimia 4.5 kutoka asilimia 4.3 iliyokuwepo mwezi Machi 2015.

Na Aron Msigwa – MAELEZO
8/5/2015. Dar es salaam.
OFISI ya Taifa ya Takwimu imesema kuwa Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa mwezi Aprili 2015 umeongezeka Kidogo hadi kufikia asilimia 4.5 kutoka asilimia 4.3 za mwezi Machi 2015 kutokana na kuendelea kuongezeka kwa kasi ya bei ya baadhi ya bidhaa za vyakula na huduma katika maeneo mbalimbali nchini.

Akitoa taarifa ya Kuongezeka kwa mfumuko huo leo jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa sensa ya Watu na Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bw. Ephraim Kwesigabo amesema kuwa kuongezeka kwa mfumuko huo kumesababishwa na kasi ya upandaji wa bei ya bidha za vyakula zinazotumiwa na kaya binafsi kwa mwezi Aprili 2015.

Amezitaja bidhaa hizo kuwa ni Mchele ,Nyama,Choroko,Sukari,Samaki waliokaushwa, Maharage, Viazi mviringo,Viazi vitamu, unga wa mahindi na mahindi.

Kuhusu Fahirisi za bei kwa maana ya kiwango cha badiliko la kasi ya bei ya makundi 12 ya bidhaa na huduma zote zinazotumiwa na Kaya binafsi kwa kuzingatia kipimo cha mwezi amesema zimeongezeka hadi kufikia 157.21 mwezi Aprili 2015 kutoka 151.88 za mwezi Machi 2015 huku Fahirisi za kipimo cha mwaka yaani mwezi Aprili 2015 zikifikia 157.21 kutoka 150.50 za Aprili 2014.

Kwa upande wa uwezo wa shilingi 100 ya Tanzania katika kununua bidhaa na huduma za mlaji kwa mwezi Aprili , 2015 amesema kuwa umefikia shilingi 63 na senti 61 ikilinganishwa na kiasi cha shilingi 64 na senti 15 za mwezi Machi 2015. 

“Uwezo wa shilingi 100 ya Tanzania katika kununua bidhaa na huduma zilezile kwa mlaji kwa mwezi Machi 2015 na Aprili 2015 umepungua kidogo, hii inamaanisha sasa mtu atahitaji kuongeza ziada ili aweze kununua bidhaa na huduma sawa sawa na zile alizonunua mwezi Machi mwaka huu"

Kwa upande wa mfumuko wa Bei wa mwezi Machi 2015 katika nchi za Afrika Mashariki amesema una mwelekeo unaofanana , Kenya ukiongezeka na kufikia asilimia 7.08 kutoka 6.31 za Machi 2015 huku Ugandamfumuko wa bei kwa mwezi Aprili 2015 ukiongezeka hadi asilimia 3.60 kutoka asilimia 1.90 za mwezi Machi 2015.

No comments:

Post a Comment