Benki mbili kuu nchini Uingereza zimeanzisha uchunguzi wa akaunti zinazohusishwa na Shirikisho la soka duniani FIFA.
Benki za Barclays Standard Chartered, na HSBC, zimetajwa katika ripoti ya idara ya ujasusi ya Marekani FBI kuwa zilitumika kufanikisha malipo ya kiinua mgongo na rushwa kwa maafisa wakuu katika FIFA.
Ripoti hiyo ndiyo iliyotumika kuwakamata maafisa wakuu 7 wa FIFA juma lililopita walipokuwa wamewasili mjini Zurich Uswisi kwa kongamano la kila mwaka la FIFA.
Kongamano hilo,lilimchagua rais wa FIFA Sepp Blatter kuhudumu kwa muhula wa 5 licha ya shinikizo kutoka kwa wadau wakimtaka ajiondoe ilikuruhusu uchunguzi wa kina kuhusu madai ya ufisadi unaoendelea ndani ya FIFA.
Benki za Barclays na HSBC zimekataa kujadili swala hilo huku benki ya Standard Chartered ikikiri kuwa inaendesha uchunguzi wa kina ilikubaini iwapo malipo hayo ya mlungula yalipitia ndani ya akaunti zake.
Wakati huohuo waziri mbadala wa afya Andy Burnham ameongezea sauti yake katika kampeini ya kuitaka Uingereza isusie kombe la duniania la mwaka wa 2018 itakayofanyika huko Urusi.
Hata hivyo mwenyekiti wa shirikisho la soka la Uingereza Greg Dyke ameonya kuwa Uingereza haiwezi kuchukua hatua hiyo ikiwa pekee yake.
''itatubidi kuwashawishi mataifa makubwa kisoka iwapo tunataka sauti yetu isikike na iwe na athari tunayoikusudia''.
Wasimazizi wa soka barani Uropa wanapanga kukutana jijini Berlin Ujerumani wiki ijayo kufanya maamuzi ya iwapo watasusia mchuano wa kombe la dunia la mwaka wa 2018 utakaoandaliwa Urusi au la .
No comments:
Post a Comment