TANGAZO


Thursday, April 30, 2015

TAARIFA KWA UMMA: UFAFANUZI KUHUSU KANUNI UWIANISHAJI WA MAFAO YA PENSHINI YA MWAKA 2014


UTANGULIZI:
Hivi karibuni kumekuwa na taarifa katika baadhi ya  vyombo vya habari juu ya kauli ya baadhi ya vyama vya wafanyakazi juu ya kanuni ya uwianishaji mafao ya pensheni kwa wale wanaostaafu kwa hiari. Kauli ambayo imeleta wasiwasi  miongoni mwa wanachama wa Mifuko ya Hifadhi ya jamii na Umma  kwa ujumla. Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) inapenda kutoa ufafanuzi kama ifuatavyo:

Sera ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii ya mwaka 2003 iliainisha changamoto mbalimbali zilizokuwa zinaikabili sekta ya hifadhi ya jamii ikiwemo kupishana kwa vikokotoo vya mafao. Utofauti wa vikokotoo hivi ulileta malalamiko mengi kutoka kwa wanachama kwa kuwa vilisababisha kuwepo kwa tofauti kubwa ya viwango vya pensheni vilivyotolewa na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.

Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) kwa kushirikiana na Wizara ya Kazi na Ajira; Vyama vya wafanyakazi; Chama cha Waajiri; Mifuko ya Hifadhi ya Jamii pamoja na wadau wengine ilichukua hatua mbalimbali kutatua changamoto hizo kwa nia ya kuboresha sekta hii.Hatua hizo ni pamoja na kutoa Kanuni ya Uwianishija Mafao ya Pensheni. Kanuni hizi zimeanza   kutumika tarehe 1 Julai 2014.
UFAFANUZI
Kanuni ya Uwianishija Mafao ya Pensheni ya 2014 ina vipengele 15 ambavyo vinalenga kuboresha mafao ya pensheni ya wanachama, kulinda na kutetea maslahi ya wanachama, kuhuisha kiwango cha uchangiaji na malipo ya pensheni ya wanachama wa Mifuko mbalimbali na kutengeneza mfumo madhubuti ya kisheria katika kuwianisha viwango vinavyohusiana na mafao ya pensheni.
Taarifa zilizotolewa katika vyombo vya habari zinazungumzia kipengele cha 13 cha kuwianisha mafao ya wanachama wanaostafu kwa hiari. Hawa ni wale wanaostaafu  kabla ya kufikisha umri wa miaka 60. 
Wastaafu hawa ni chini ya asilimia 5 ya wastaafu wote kwenye Sekta. Katika taarifa za vyombo vya habari,  mwakilishi wa Wafanyakazi anasema wanachama wanaostaafu kwa hiari wanakatwa asilimia 18 ya mafao yao kwa mwaka suala ambalo linatafsiriwa kama ni ukandamizaji  wa haki za wanachama. Mamlaka inakanusha kwamba hakuna kipengele kinachoelekeza kukata asilimia 18 kwa mwaka.
Ukweli ni kwamba, kipengele cha 13 kinatoa punguzo la elekeza kupunguzo asilimia 0.3 kwa kila mwezi kutoka kwenye mafao ya mwanachama aliestaafu kwa hiari yaani kati ya miaka 55 mpaka 59. Punguzo hili hukoma pale mstaafu anapofikia miaka 60.
Kiwango hiki kilifikia baada ya kuzingitia mambo yafuatayo; malalamiko ya wanachama ya kupishana kwa mafao; uzoefu wa nchi zingine zenye mfumo sawasawa na wa Tanzania yaani (Defined benefit); umri wa kustaafu kwa lazima wa miaka 60; taarifa ya watathimini wa Mifuko waliopendekeza asilimia 0.6; vilevile ikumbukwe kwamba  baadhi ya  Mifuko ilikuwa  inatoza asilimia 0.5 kwa mwaka  kabla ya kanuni hii. 

Majadiliano yalifanywa na Wadau yalipendekeza kiwango kishuke na kuwa  asilimia 0.3. Wadau hao ni pamoja na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi. Kwa uchache vikao ambavyo vilikuwa na ushiriki wa Shirikisho ni pamoja  na tarehe 27 Julai 2012 katika ukumbi wa NSSF, tarehe 23 Machi 2013 ukumbi wa PSPF Jubilee Tower; tarehe  27 Mei 2013 ukumbi wa Wizara ya Kazi na Ajira na tarehe 15 April 2014 ukumbi wa mikutano wa Wizara ya Kazi na Ajira. 
Hata baada ya kutoa kanuni hizo Serikali imeendelea kutoa elimu na kufanya vikao mbalimbali. Vikao hivyo ni pamoja na kile cha Tarehe  21 Octoba 2104 ukumbi wa SSRA ; 8 Desemba 2014 na Tarehe 25 Februari 2015 kule Morogoro
Tafsiri halisi ya kipengele hiki ni kwamba mwanachama anayestaafu kwa hiari atapunguziwa asilimia 0.3 kwa mwezi sawa na 3.6 kwa mwaka hadi pale atakapofikia  kufikia miaka 60. Hivyo  si sahihi kusema kwamba kuna kanuni zinakata asimia 18 kwa mwaka. Hapa mwanachama anayestaafu kwa hiari akiwa na  miaka 59 anakatwa  asilimia 3.6 tu. Mwenye  miaka 58 anakatwa jumla ya asilimia 7.2.  
Hali kadhalika mwenye miaka 57 anakatwa jumla ya asilimia 18 katika kipindi cha miaka mitano au miezi 60. Hata hivyo pamoja na punguzo la asilimia 0.3 bado mstaafu wa hiari anamzidi yule anayestaafu akiwa na miaka 60 kwa asilimia 10. 

Bila punguzo hilo anayestaafu kwa hiari akiwa na miaka 55 anamzidi mwenzake wa miaka 60 kwa asilimia 28. Hii inaondoa usawa wa mafao katika hifadhi ya Jamii. Jambo ambalo limekuwa likilalamikiwa na vyama vya wafanyakazi na wanachama kwa ujumla.
Kuhusu suala la kutokushirikishwa kwa wadau, Mamlaka inapenda kuweka wazi kuwa Sekta ya hifadhi ya  jamii imekuwa ikiendeshwa kwa utatu; yaani Serikali, Wafanyakazi na Waajiri , kwa hiyo hata katika hili utatu ulizingatiwa na wadau walishirikishwa ipasavyo.

HITIMISHO

Mamlaka ya Udhibiti na Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii inapenda kuwaondoa wasiwasi wanachama na kutoa wito kwa wanachama wa sekta ya hifadhi ya jamii na kwa watanzania kwa ujumla  kuunga mkono Maboresho katika Sekta ya Hifadhi ya Jamii kwa lengo la kuboresha mafao na kuifanya sekta kuwa endelevu.

Mamlaka inapenda kuufahamisha Umma kwamba mpaka sasa haijapokea malalamiko yoyote kutoka kwa wanachama. Iwapo kuna malalamiko yoyote kutokana na utekelezaji wa kanuni hii basi wanachama wasisite kuwasiliana na Mamlaka ili wapatiwe ufumbuzi mapema iwezekanavyo.

 Mwisho tunatoa shukrani zetu za dhati kwa ushirikiano mkubwa tunaopata toka kwa vyama vya Wafanyakazi pamoja na Shirikisho lao; chama cha Waajiri; vyombo vya habari pamoja na Serikali kwa ujumla
 Imetolewa na:
Mkurugenzi mkuu
Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii – SSRA
S.L.P 31846

Dar es Salaam

No comments:

Post a Comment