Mwenyekiti wa Misa-Tanzania-Media Institute of Southern Africa (Taasisi ya vyombo vya habari Kusini mwa Afrika) Bwana Simon Berege akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusiana na maadhimisho ya siku ya uhuru wa habari duniani (WPFD) yatakayofanyika tarehe 2 mwezi Mei mwaka huu mkoani Morogoro.
Na Modewjiblog team
WANAHABARI na wadau wa habari wanatarajiwa kukutana Mkoani Morogoro kwa siku mbili kwa kusanyiko la maadhimisho ya siku ya Uhuru wa habari duniani (WPFD), litakalofanyika katika hoteli ya Nasheera, Mjini Morogoro.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mwenyekiti wa Misa-Tanzania-Media Institute of Southern Africa (Taasisi ya vyombo vya habari Kusini mwa Afrika), Ndugu Simon Berege alieleza kuwa, kusanyiko hilo la wandishi wa habari na wadau wa habari litafanyika mjini humo Mei 2-3, mwaka huu.
“Hii ni mara ya kwanza WPFD kuadhimishwa mkoani Morogoro na mwakani itafanyika mkoa mwingine nia ni kufanya kila mkoa kupata nafasi ya kuadhimisha siku hiyo.
Wakati wa maadhimisho hayo wadau watakumbuka gharama za waandishi wa habari kukusanya taarifa mbalimbali na kuwapatia wananchi, gharama ambazo wakati mwingine ni uhai wao au hata kunyimwa uhuru’ alieleza Berege.
Aidha siku hiyo watakumbukwa wale waliopoteza maisha kutokana na harakati za kutafuta habari kwa ajili ya umma.
Siku ya WPFD, ambayo huadhimishwa duniani kote kila mwaka ilianzishwa na Umoja wa Mataifa kwa lengo la kuadhimisha kanuni za uhuru wa habari na kuwakumbuka wale waliokufa wakijaribu kutekeleza kanuni hizo.
Kwa maneno mengine WPFD ni jukwaa linalotumika na waandishi wa habari na wadau wengine katika kutoa kauli za kushawishi serikali mbalimbali kutunga sheria rafiki za vyombo vya habari ambazo zitahakikisha uwapo wa uhuru wa habari.
Kauli mbiu ya mwaka huu ni ‘Usalama wa habari katika ulimwenguj wa dijiti: Uandishi bora, Usawa wa jinsia na faragha’.
Berege alibainisha kuwa, kwa kuzingatia kauli mbiu hiyo, WPFD 2015 itaangalia masuala matatu muhimu: Ikiwemo Uandishi bora na ulio huru katika dunia ya dijiti.
Humu itajadiliwa uwingi wa vyombo vya habari na athari zake katika majukumu ya uandishi na uwajibikaji kwa umma, masuala ya kujiwabisha wenyewe, changamoto katika habari za uchunguzi, kauli za uchochezi na vyombo vya habari na mafunzo ya habari.
Pia suala lingine ni juu ya Wanawake na menejimenti ya vyombo vya habari; na namna vyombo vya habari vinavyomuona mwanamke huku la mwisho likiwa ni suala la Usalama wa waandishi wa habari hasa katika maeneo yenye vurugu na jinsi ya kuhami vyanzo vya habari dhidi ya ufichuaji wa kidijiti.
Katika kongamano hilo pia litatoa nafasi ya kujadili na kutoa maazimio kuhusu sheria zilizopitishwa na bunge na zile ambazo zimetamkwa kwa mara ya kwanza. Sheria hizo ni pamoja na za Cybercrime Act, Statistics Act, Media Services Bill and the Access to Information Law.
Hata hivyo, imeelezwa kuwa, Wakati wa kongamano hilo walioathirika kwa kuvunjwa kwa uhuru wa habari watatoa ushuhuda wao.
Pia taarifa ya hali ya vyombo vya habari Kusini mwa Afrika iliyoandaliwa na MISA itazinduliwa rasmi.
Aidha, katika tukio hilo, mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini, Bw. Alvaro Rodriguez huku wadau zaidi ya 200 wakiwemo wadau wa habari na maendeleo pamoja na wawakilishi kutoka serikalini na mashirika mbalimbali ya kimataifa, mabalozi, wabunge, vyama vya kijamii, asasi zisizokuwa za kiserikali, waandishi maveterani,wakuu wa vyuo vya habari na waandishi wa habari.
Tukio hilo limeandaliwa kwa pamoja na Media Institute of Southern Africa-Tanzania Chapter [MISA (T) Chapter], Media Council of Tanzania [MCT], Tanzania Media Fund [TMF], Union of Tanzania Press Clubs [UTPC], United Nations Tanzania Office, UNESCO.
Wengine ni Konrad-Adenauer-Stiftung Tanzania [KAS], Media Owners Association of Tanzania [MOAT], Tanzania Editors’ Forum [TEF], Tanzania Media Women’s Association [TAMWA), Morogoro Press Club na Tanzania Communication Regulatory Authority [TCRA).
Aidha kamati ya maandalizi ya WPFD 2015 imewezesha tukio hilo kwa kushirikisha pia Government Employees Pensions Fund [GEPF], Alliance One Tanzania, IPP Group of Companies, European Union (EU) na Tanzania National Parks [TANAPA].
Mkurugenzi wa Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF) ambao ni miongoni mwa wadau wa maandalizi ya maadhimisho hayo Bw. Ernest Sungura akifafanua jambo katika mkutano na waandishi wa habari (hawapo pichani) uliofanyika katika hoteli ya Holiday Inn jijini Dar es Salaam leo. Kulia Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa ambao ni miongoni mwa wadhamini wa maadhimisho hayo, Usia Nkhoma Ledama.
Makamu Rais wa Umoja wa Vilabu vya Waancdishi wa habari nchini (UTPC), Jane Mihanji akisisitiza umuhimu wa wanahabari kuhudhuria maadhimisho ya siku ya uhuru wa habari duniani (WPFD) ambayo kitaifa yanatarajiwa kufanyika mkoani Morogoro Mei 2 mwaka huu. Katikati ni Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa ambao ni miongoni mwa wadhamini wa maadhimisho hayo, Usia Nkhoma Ledama na kushoto ni Mkurugenzi wa Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF) ambao ni miongoni mwa wadau wa maandalizi ya maadhimisho hayo Bw. Ernest Sungura.
Miongoni mwa wadau wa maandalizi ya maadhimisho ya siku ya uhuru wa habari duniani (WPFD) Bw. Richard Shaba kutoka KAS Tanzania na Mwakilishi kutoka TAMWA, Godrida Jola wakisikiliza maswali kutoka kwa wanahabari (hawapo pichani).
Sehemu ya waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali nchini waliohudhuria mkutano huo.
No comments:
Post a Comment