Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein akifungua pazia kuashiria ufunguzi wa Jengo la Afisi Kuu ya Uhamiaji Zanzibar leo Kilimani Mjini Zanzibar akimuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein akikata utepe kama ishara ya ufunguzi wa Jengo la Afisi Kuu ya Uhamiaji Zanzibar leo, Kilimani Mjini Zanzibar akimuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete. Kutoka kushoto ni Kamishna Mkuu wa UhamiajiTanzania Sylvester Ambokile Mwakinyule na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Perera A. Silima.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein (katikati), akiangalia hatua za utengenezaji wa Passport za Uraia wa Tanzania wakati alipotembelea sehemu mbali mbali baada ya kulifungua Jengo la Afisi Kuu ya Uhamiaji Zanzibar leo, Kilimani Mjini Zanzibar akimuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete. Kushoto ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Perera Ame Silima na kulia ni Inspekta wa Uhamiaji Hassan Suleiman Ameir.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein (wa pili kulia) akipata maelezo kutoka kwa Asistance Inspekta Khamis Ali Haji (katikati), wakati alipotembelea katika chumba cha kumbukumbu za picha kwa Wananchi walioomba Passpoti za Uraia baada ya kulifungua Jengo la Afisi Kuu ya Uhamiaji Zanzibar leo Kilimani Mjini Zanzibar akimuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete
Na Said Ameir, Ikulu Zanzibar
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Jakaya Mrisho Kikwete amesema uimarishaji wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni juhudi endelevu hivyo hakuna kurudi nyuma katika kuhakikisha unakuwa imara na kusonga mbele kila kukicha.
Rais Kikwete amesema hayo leo katika hotuba yake ya ufunguzi wa Jengo jipya na la kisasa la Ofisi Kuu ya Uhamiaji Zanzibar iliyosomwa kwa niaba yake na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein.
Kwa hivyo alisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Nne anayoingoza imejikita katika uimarishaji wa taasisi za Muungano kwa nia ya kuhakikisha kuwa kunakuwepo Muungano imara ikiwa ni kuendeleza utamaduni wa serikali za awamu zilizopita ambazo zimekuwa zikiilinda vyema misingi ya muungano huo iliyowekwa na waasisi wake Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume.
“Hivyo, Serikali itaendelea kuimarisha na kuzijengea uwezo taasisi zote za Muungano ili zieweze kufanyakazi zake kwa ufanisi na katika sura halisi ya muungano kwa nia ya kuhakikisha kwamba wananchi wote wanaendelea kunufaika na matunda na Muungano” Dk. Kikwete alieleza.
Alibanisha katika hotuba hiyo kuwa kuboresha Sheria, Kanuni na Taratibu za ajira za watumishi katika Taasisi za Muungano ili kufanya utumishi wao uwe na sura muafaka ya kimuungano ni miongoni mwa mambo aliyoahidi wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka 2010 na amefurahi kuona kuwa suala hilo linatekelezwa katika maeneo yeote husika.
Hatua hiyo alisisitiza ni “kuhakikisha kwamba tunatekeleza kwa vitendo yale yote ambayo tuliahidi kwa nia ya kuimarisha Muungano wetu huu”
Katika hotuba yake hiyo, Rais Kikwete aliwataka watumishi wa Idara ya Uhamiaji kutoa huduma zinazoendana na uzuri wa jengo na mandhari yake ingawa alieleza kuwa anatambua kuwa mafanikio na ufanisi wa utekelezaji wa majukumu ya Idara yanategemea mambo mengi ikiwemo watumishi wenye mafunzo na weledi wa hali ya juu.
Kwa hivyo Dk. Kikwete aliwahakikishia watumishi wa Idara ya Uhamijai nchini kuwa Serikali itahakikisha inaendelea kuboresha zaidi mifumo ya huduma za uhamiaji ili ziweze kwenda na mahitaji ya wakati uliopo.
“Juhudi hizi zitakuwa ni pamoja na kuanzishwa kwa mfumo wa kutoa huduma za uhamiaji kwa njia ya mtandao, maarufu e-immigration ambao utaunganisha huduma za uhamiaji na mitandao mingine ndani na nje ya nchi”. Dk. Kikwete aliongeza.
Akitoa maelezo kabla ya kumkaribisha mgeni Rasmi, Naibu wa Mambo ya Ndani ya Nchi Pereira Ame Silima alisema kuwa Mazingira mazuri ya kufanyia kazi ni jambo la muhimu sana kwa watumishi na hata wale wanaokuja kupata huduma Ofisini.
Alibainisha kuwa huko nyuma katika baadhi ya maeneo kutokana na Ofisi za Uhamiaji na Polisi kuwa katika hali zisizolingana na majukumu yao baadhi ya wageni walikuwa hawaziamini ofisi hizo na hata kufikia wakati kukataa kulipia huduma wakiamini si ofisi rasmi.
Kwa hivyo alisema uimarishaji wa ofisi za Idara mbali mbali za Wizara hiyo husasan zinazohusiana na usalama wa raia limekuwa jambo la faraja kubwa kwa wizara hivyo hawana budi kuishukuru Serikali ya Awamu ya nne kwa kuiwezesha wizara kuimarisha mazingira ya Idara zake.
Hivyo, Waziri Silima alieleza matumaini ya Wizara yake kuwa Serikali itaendelea kuiwezesha Wizara hiyo ili kazi ya kuendelea kuboresha Mazingira ya kazi na Makaazi ya Askari wetu wote.
Akitoa taarifa ya ujenzi wa jengo hilo Kamishna Mkuu wa Uhamiaji Sylvester Ambokile, alieleza kuwa jengo hilo limegharimu shilingi bilioni 4.02 badala ya shilingi bilioni 2.3 zilizokadiriwa mwaka 2007 kutokana na kupanda gharama za ujenzi.
Fedha hizo alibainisha kuwa ni za serikali ikiwa ni gawiwo la fedha ambazo Idara hiyo inapata kutoka Hazina kutokana na malipo ya huduma mbalimbali zinazotolewa na Idara hiyo.
Kamishma Mkuu huyo aliipongeza Kampuni ya Quality Building Contractors chini ya Mkurungenzi wake Bibi Fatma Issa Kara kwa kukamilisha vyema ujenzi wa jengo hilo pamoja na Mshauri wa Mwelekezi, Idara ya Majenzi, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kusimamia vyema ujezi huo.
Aliongeza kuwa Idara yake imekuwa ikifanya jitihada kubwa kuimarisha ofisi zake na makaazi ya watumishi wa idara hiyo ili kuwapa fursa kufanya kazi zao kwa utulivu na ufanisi.
Hata hivyo alitaja baadhi ya changamoto zinazoikabili Idara hiyo kuwa ni pamoja na upungufu wa watumishi ambapo Idara hiyo hivi sasa ina watumishi chini ya 3,000 wakati mahitaji ni watumishi 8,000.
Alizitja changamoto nyingine kuwa ni upungufu wa majengo ya ofisi, vitendeakazi ufinyu wa bajeti na kukosa mawasiliano ya kimtandao yanayounganisha huduma zote za uhamiaji ili kuweza kubaini na kuzuia vitendo vya uhalifu katika mipaka na wahalifu wenyewe.

No comments:
Post a Comment