TANGAZO


Monday, March 30, 2015

Bungeni Mjini Dodoma leo:


Wananchi watakiwa kudai risiti wanunuapo mafuta kwenye vituo vya kuuzia petroli na dizeli


Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba

Na Johary Kachwamba - MAELEZO, DODOMA
SERIKALI  imewahimiza Wananchi kudai risiti pindi wanunuapo mafuta kwenye vituo vya kuuza Petroli na Dizeli ili kurahisisha ukusanyaji wa Kodi ya Mapato, Aidha kutokuchukua risiti ni kosa kisheria hivyo wote muuzaji na mnunuzi  wanastahili adhabu kwa mujibu wa sheria.

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mwigulu Nchemba amesema hayo bungeni mjini Dodoma wakati akijibu swali la Mhe. Rukia Ahmad, Mbunge wa Viti Maalum aliyehoji kwanini Serikali isitoze kodi kwa jumla pale vituo hivyo vinaponunua mafuta
Mhe. Nchemba amesema ulipaji wa kodi ya mapato hususani kwa makampuni yanayouza mafuta unafuata mfumo wa wafanyabiashara kujikadiria wenyewe na kulipa kodi kama ilivyoainishwa kwenye Sheria ya Kodi ya Mapato sura 132, kisha ukaguzi wa hesabu kufuata baadaye.

“baada ya kubaini kuwa kuna udhaifu katika utoaji risiti ambao husababisha upotevu wa mapato, Serikali imeanzisha mfumo wa matumiz ya mashine ya kodi ya kielektroniki kwenye biashara mbalimbali ikiwa ni pamoja na vituo vya kuuza mafuta” Mhe. Nchemba.

Hata hivyo mfumo wa matumizi ya mashine za kodi za kielektroniki katika kutoa risiti za mauzo umetekelezwa kwa awamu mbili, awamu ya kwanza iiwahusu wafanyabiashara waliosajiliwa na kodi ya ongezeko la thamani (VAT) wakati awamu ya pili inahusu wafanyabiashara wengine waliobaki

“vituo vingi vya mafuta nchini havijasajiliwa na kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwa kuwa mafuta ya Petroli na Dizeli hayatozwi kodi ya VAT” aliongezea Mhe. Nchemba

Kodi za Ushuru wa bidhaa, ushuru wa mafuta na ushuru wa Petroli hukusanywa Forodhani mara tu bidhaa hizi zinapoingizwa nchini, isipokuwa kwa mafuta ya Petroli na Dizeli yanayoenda nchi za jirani. Kodi hizi ulipwa forodhani na makampuni yanayoagiza mafuta ya Petrol na dizeli kwa kuzingatia kiasi cha ujazo wa lita zilizoingizwa nchini kabla ya kuuza kwenye vituo vya mafuta.

Jamii yatakiwa kutoa ushirikiano kukomesha mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi nchini

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi, Pereira Silima

Na Johary Kachwamba - MAELEZO, DODOMA
JAMII imetakiwa kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi nchini katika kutoa taarifa zitakazo fanikisha kukamatwa kwa wote walioshiriki mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi nchini.

Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani  Mhe. Pereira Silima bungeni mjini Dodoma alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mhe. Al -Shaimaa Kwegyir, Mbunge wa Viti Maalum aliyehoji kuchelewa kwa taarifa ya kupatikana kwa mtoto mwenye ulemavu wa ngozi, Pendo Emmanuel.

“Pendo alitekwa kutoka mikononi mwa mama yake mzazi, hii changamoto ni kubwa sana, tunaomba jamii itusaidie kutoa taarifa zitakazo saidia kufanikisha kukamatwa kwa wahusika, tushirikiane kwa pamoja kukomesha tatizo hili” alisema Mhe. Silima

“tangu kutekwa kwa mtoto Pendo watu 14 wanashikiliwa na jeshi la polisi akiwemo baba mzazi, uchunguzi bado unaendelea na watuhumiwa watafikishwa mahakamani hivi karibuni, ila Pendo bado hajapatikana” aliongezea Mhe. Silima

Aidha akijibu Swali la msingi la Mhe. Salumu Barwany, Mbunge wa Lindi Mjini, aliyehoji idadi ya kesi za mauaji ya walemavu wa ngozi na sababu za kuchelewa kutolewa hukumu. Mhe. Silima alisema kesi 10 zinaendelea kisikilizwa mahakama mbalimbali

“kati ya mwaka 2006 hadi 2015 jumla ya matukio 56 ya uhalifu dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi yaliripotiwa nchini. Matukio 41 yalihusisha vifo 43, matukio 13 yalihusisha majeruhi 13 na matukio 2 ya kupotea kwa watu wenye ulemavu wa ngozi” alifafanua Mhe. Silima

“kesi 46 kati ya matukio 56 zilifikishwa Mahakamani ambapo kesi 10 zenye watuhumiwa 12 zilitolewa hukumu ya kifo na kumi ziko chini ya upelelezi. Aidha kesi 26 watuhumiwa wake waliachiwa huru kwa kukosa ushahidi” aliongezea Mhe. Silima

Kuchelewa kwa hukumu au upelelezi wa baadhi ya kesi zilizotajwa kunachangiwa na sababu mbalimbali kama vile matokeo ya uchunguzi wa DNA toka Mamlaka ya Uchunguzi na/au mashahidi kutopatikana kwa urahisi na kwa wakati.

Statoil yafanya ugunduzi wa nane 
wa gesi asilia katika Bahari Kuu ya 
Tanzania
Waziri wa Nishati na Madini (wa pili Kulia) Mhe.George Simbachawene akizungumza na waandishi wa Habari Mjini Dodoma kuhusu Ugunduzi wa nane wa gesi asilia uliyofanywa na Kampuni ya Statoil katika eneo la Bahari Kuu,(wa kwanza kulia) ni Naibu Waziri Nishati na Madini Dkt Charles Mwijage,na (wa kwanza kushoto) ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu Nishati na Madini Mhe.Richard Ndassa (Mb) wa Sumve CCM. (Picha na Anitha Jonas-MAELEZO)

Na Johary Kachwamba – MAELEZO, DODOMA
SERIKALI kupitia Wizara ya Nishati na Madini imetangaza ugunduzi wa gesi asilia katika Miamba ya Mchanga kwenye kisima kinachochimbwa na Statoil cha Mdalasini-1 kwenye bahari kuu ya Tanzania.

Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. George Simbachawene amebainisha hayo kwenye mkutano na Waandishi wa Habari mjini Dodoma. Baada ya kuthibitishwa na Makamu wa Rais wa Statoil, Nick Maden pamoja na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).

“ugunduzi huo wa gesi asilia wa futi za ujazo trilioni 1.0-1.8, unaongeza kiwango cha gesi asilia iliyopatikana kwenye kitalu namba 2 kufikia futi za ujazo trilioni 22. Kisima cha Mdalasini -1 kimechimbwa katika urefu wa mita za maji ya bahari 2,296 kusini mwa kitalu namba 2” alisema Mhe. Simbachawene.

“kuanzia mwanzo wa uchimbaji, Februari 2012, tumechimba visima 13 na tumefanya ugunduzi katika visima 8 ikiwemo Mdalasini-1. Bado tunaona uwezekano wa gesi zaidi katika eneo la Kitalu namba 2” aliongezea Mhe. Simbachawene

Statoil ni Mkandalasi katika Leseni ya Utafutaji ya Kitalu namba 2 kwa niaba ya TPDC na inayohisa ya asilimia 65% na mshirika wake ExxonMobil and Production Tanzania Limited inazo hisa asilimia 35%.

Wakati wa uendeshaji baada ya Serikali kutoa Leseni ya uzalishaji, TPDC kulingana na mkataba inaweza kushiriki katika uendeshaji na uzalishaji kwa kutwaa asilimia 10% ya uwekezaji.

No comments:

Post a Comment