TANGAZO


Thursday, February 12, 2015

Wagonjwa wa Ebola waongezeka Guinea

Wafanyakazi wa kutoa huduma kwa wagonjwa wa ebola huko Afrika magharibi.
Kamati ya Kimataifa ya Chama cha Msalaba Mwekundu, imesema wastani wa mashambulio kumi kwa mwezi yanafanyika dhidi ya watumishi wake wa kujitolea wanaotoa elimu juu ya ugonjwa wa Ebola nchini Guinea.
Mwaka jana, watu wanane wakijaribu kutoa elimu zaidi kuhusu ugonjwa wa ebola walishambuliwa kwa kupigwa hadi kufa na wananchi wa Guinea ambao waliamini kuwa watu hao walikwenda katika kijiji chao kueneza ugonjwa huo. Anaripoti mwandishi wa BBC wa masuala ya Afrika Mary Harper.
Shambulio la hivi karibuni dhidi ya wafanyakazi wa chama cha Msalaba Mwekundu lilitokea Jumapili wakati wafanyakazi wawili wa kujitolea walipigwa katika mji wa magharibi wa Fouecariah wakati wakijaribu kuelekeza namna salama ya kuzika mtu aliyekufa kutokana na ugonjwa wa ebola. Mkuu wa chama cha Msalaba Mwekundu nchini Guinea, Youssouf Traore, amesema ugonjwa wa ebola hautatokomezwa hadi hapo watu watakapobadili mtazamo wao kuhusu ugonjwa huo.
Licha ya jitihada za kutoa elimu ya uelewa juu ya ugonjwa huo, bado kuna imani kubwa ya ushirikina kuhusu ebola. Wananchi wa Guinea mara nyingi wanaamini kuwa waliokuja kuzika, wanaondoa maambukizi katika maeneo yenye ugonjwa, na imani hiyo kwa kweli inasambaza ugonjwa.
Wiki iliyopita, idadi ya wagonjwa wapya wa ebola nchini Guinea iliongezeka karibu mara mbili-- ishara kwamba ujumbe kuhusu ugonjwa wa ebola bado haujafanikiwa.
Guinea ni miongoni mwa nchi zilizoathirika zaidi na ugonjwa ebola Afrika magharibi. Nyingine ni Liberia na Sierra Leone. Zaidi ya watu elfu nane wameripotiwa kupoteza maisha kutokana na ugonjwa wa ebola.

No comments:

Post a Comment