Tanzania imetia saini rasmi Hati ya Makubaliano ya Mkutano wa mtoto wa kike uliofanyika mwaka jana nchini Uingereza.Kwa mujibu wa waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto wa Tanzania, Sophia Simba, kusaini kwa hati hiyo, ni kuonyesha dhamira ya serikali ya nchi hiyo katika kupambana na kuhakikisha inatokomeza vitendo vya ukeketaji na ndoa za utotoni.
Utiaji saini huo, umefanyika mbele ya wawakilishi kutoka shirika la umoja wa mataifa la Idadi ya watu, UNFPA, balozi wa Uingereza nchini Tanzania na wawakilishi kutoka mashirika yasiyo ya kiserikali.
Sophia Simba ni waziri wa maendeleo ya jamii jinsia na watoto.
Takwimu nchini Tanzania zinaonyesha kuwa katika kila watoto watano wa kike, wawili kati yao wanakeketwa huku wengine wakipitia ndoa za utotoni hali inayowanyima watoto wa kike haki zao za msingi ikiwemo kupata elimu.
"Kimsingi ukeketaji na ndoa za utotoni zinawakwaza watoto kimasomo na kukosa afya njema na kuathiri maendeleo ya Tanzania. Nchi zinazoruhusu watoto wote wa kike kwenda shule na kukamilisha elimu yao, hizi ndizo nchi ambazo zina mafanikio makubwa katika kupunguza umaskini."Anasema Dianna Melrose, balozi wa Uingereza nchini Tanzania. Baadhi ya wanaharakati wanasema kutofanikiwa kwa mapambano haya mara nyingi kunasababishwa na kukosekana kwa utashi wa kisiasa kama ambavyo anasema Valerie Msoka, mkurugenzi mtendaji wa chama cha wanahabari wanawake nchini Tanzania, TAMWA.
Mkoa wa Shinyanga ndio unaoongoza nchini Tanzania kwa mimba na ndoa za utotoni.
Takwimu kutoka mashirika mbalimbali ikiwemo UNICEF zinaonyesha kuwa, kwa siku, watoto 16 wanapachikwa mimba za utotoni.
Kwa mujibu wa wataalamu, hali hii imekuwa ikiendelea kwa muda mrefu na kwa asilimia kubwa imezorotesha maendeleo ya mtoto wa kike katika eneo hilo.
No comments:
Post a Comment