Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi akimkabidhi Mipira kwa ajili ya Gari ya Chama ya Mkoa wa Singia Katibu wa CCM wa Mkoa huo Bibi Merry Chatanda akitekeleza ahadi aliyotowa wakati wa ziara yake Mkoani humo miezi michache iliyopita. Kulia ya Balozi Seif ni Mkewe Mama Asha Suleiman Iddi na Mbunge wa Mkoa wa Singida Viti Maalum Mh. Anna Chilolo, hafla iliyofanyika nyumbani kwa Balozi Seif Mtaa wa Farahani Mjini Dodoma. Balozi Seif akiuhakikishia Uongozi wa Mkoa wa Singida kuendelea kushirikiano nao katika harakati za Maendeleo licha ya kwamba ameondoka kwenye Mkoa huo kwenye wadhifa wa Ulezi wa Chama wakati akikabidhi msaada wa mipira kwa ajili ya gari la Chama, Mkoa wa Singida. (Picha zote na Hassan Issa – OMPR – ZNZ)
Na Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
6/2/2015.
MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba Viongozi wa Chama hicho wana kazi kubwa iliyo mbele yao ya kuhakikisha kwamba Chama cha Mapinduzi kinashinda kwenye uchaguzi Mkuu ujao wa mwezi Oktoba mwaka huu na kuendelea kuongoza Dola Nchini Tanzania.
Alisema Viongozi wa CCM walioko kwenye baadhi ya Majimbo yenye upinzani wanalazimika kuwajibika kufanya kazi ya ziada katika kusimamia Heshima ya Chama hicho na hatimae nafasi za Uongozi hasa zile za Ubunge, Uwakilishi na udiwani zilizoazimwa kwenda upinzani zinarejeshwa tena CCM.
Balozi Seif ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema hayo katika hafla fupi ya kukabidhi msaada wa mipira Minne kwa ajili ya Gari ya Chama cha Mapinduzi ya Mkoa wa Singida yenye Thamani ya Dola za Kimarekani Mia 600 hafla iliyofanyika hapo Nyumbani kwake Mtaa wa Farahani Mjini Dodoma.
Balozi Seif alikuwa akitekeleza ahadi aliyoitowa kwa Uongozi wa CCM Mkoa wa Singida wakati wa ziara aliyoifanya Mkoani humo wakati akiaga rasmi alipokuwa Mlezi wa Mkoa wa Singida ambapo kwa Sasa ameteuliwa na Chama kuwa Mlezi wa Mkoa wa Magharibi Unguja Kichama.
Alisema Chama cha Mapinduzi bado kinaendelea kupendwa na kukubalika na Wananchi walio wengi Nchini Tanzania Bara na Zanzibar . Hivyo ni lazima kwa Viongozi wa Chama hicho kuendelea kuyalinda mapenzi ya Wananchi na wanachama waliyokuwa nayo kwa Chama chao.
Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM aliupongeza Uongozi wa Chama na Serikali wa Mkoa wa Singida kwa ushirikiano uliompa wakati wa utekelezaji wa majukumu aliyopangiwa na Chama wakati alipokuwa Mlezi wa Mkoa huo.
Aliuhakikishia Uongozi wa Serikali na Chama wa Mkoa wa Singida kwamba akiendelea kuwa Kiongozi wa Kitaifa atakuwa tayari wawaki wowote kushirikiana na Viongozi na Wananchi wa Mkoa wa huo katika kuwaunga mkono kwenye harakati zao za kujiletea Maendeleo.
Kitoa shukrani kutokana na msaada huo kwa niaba ya Kamati ya Siasa pamoja na Wanachama wa CCM Mkoa wa Singida Katibu wa CCM wa Mkoa huo Bibi Merry Chatanda alimpongeza Balozi Seif kwa moyo wake wa kuimarisha nguvu za Chama cha Mapinduzi katika maeneo mbali mbali hapa Nchini.
Bibi Merry Chatanda alisema Mkoa huo hivi sasa unahitaji kuwa na vitendea kazi imara na muhimu kama usafiri wa Gari hasa katika kipindi hichi kinachoelekea kwenye uchaguzi mkuu wa Mwezi Oktoba mwaka huu.
Naye Mbunge wa Mkoa wa Singida Viti Maalum Mh. Anna Chilolo ambae alikuwepo kwenye hafla hiyo alisema kwamba Balozi Seif ameacha Historia kubwa ndani ya Mkoa huo kutokana na juhudi zake za kuunga mkono harakati za Maendeleo ya wananchi pamoja na za Kisiasa Mkoani humo.
Mh. Chilolo alisema Mlezi huyo mstaafu Kichama wa Mkoa wa Singida mbali ya kuhamasisha uhai wa chama lakini pia alijitahidi kuona kero na changamoto zinazowakabili wananchi wa Mkoa huo zinapatiwa ufumbuzi.
Alisema ipo Miradi mingi ya kiuchumi na kijamii ndani ya Mkoa wa Singida iliyoanzishwa na Wananchi kwa nguvu zao ambayo kwa kiasi kikubwa imepata msukumo wa fikra na pia uwezeshaji kutoka kwa Balozi Seif.
“ Ipo miradi kadhaa iliyoanzishwa na wananchi na hata ile iliyobuniwa na wana CCM ambayo baadhi yake ilikuwa ikisuasualakini kwa sasa imepata msukumo wa uwezeshaji kutoka kwa Balozi Seif “. Alisema Mbunge huyo wa Singida Viti Maalum.
Mh. Anna Chilolo alifahamisha kwamba Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi Balozi Seif ataendelea kukumbukwa na wanachama wa chama cha Mapinduzi pamoja na wananchi walio wengi wa Mkoa huo kutokana na mchango wake mkubwa usiomithilika alioufanya kwa wananchi hao.
No comments:
Post a Comment