TANGAZO


Thursday, February 5, 2015

BUNGENI LEO MJINI DODOMA

Waziri Mkuu Mizengo Pinda akijibu maswali ya wabunge ya papo kwa papo Bungeni, Dodoma.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mahmoud Mgimwa akijibu swali bungeni. 
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Ame Silima akijibu swali Bungeni.
 Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Anne Kilango Malecela

Mwenyekiti Mpya wa Bunge, Kidawa Salehe akiongoza Bunge . 
 Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii, Saidi Mtanda akiwasilisha taarifa ya kamati.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii,  Margareth Sitta akiwasilisha taarifa ya kamati yake. 
Mbunge wa  Viti Maalum (CCM) Vicky Kamata akiuliza swali kwa Waziri Mkuu Bungeni.
Mbunge wa Viti Maalum (CHADEMA) Susan Lyimo akiuliza swali kwa Waziri Mkuu.
 Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Al- Shaymaa Kwegyir akichangia taarifa ya kamati.
 Mbunge wa Mbinga Magharibi, Kapteni John Komba akichangia taarifa ya kamati.
 Baadhi ya wandishi wa habari wakifuatilia kikao cha Bunge.
Mbunge wa Lushoto, Henry Shekifu (kulia) akiambatana na wenzake kutoka nje ya ukumbi wa Bunge,huku wakibadilishana mawazo. 
Mbunge wa Mbinga Magharibi, Kapteni John Komba, akimpa mkono Mwenyekiti Mpya wa Bunge Kidawa Saleh, kumpongeza kwa kuliongoza Bunge huku Mwenyekiti mpya mwenzake Lediana Mng’ong’o (kushoto) na mbunge Martha Mlata wakifumrahia. 
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt. Seif Rashid (kushoto)akiteta jambo na Mbunge wa Mbozi Mashariki Godfrey Zambi. (Picha zote na Hussein Makame-MAELEZO, Dodoma)

Muswaada wa Sheria ya Habari kuwasilishwa bungeni
Na Hussein Makame-MAELEZO,Dodoma
SERIKALI inatarajia kuwasilisha Muswada wa Sheria ya Habari katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania la mwezi April mwaka huu ili kujadiliwa na kupitishwa kuwa Sheria kamili.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Jamii Saidi Mtanda wakati akiwasilisha taarifa ya kazi za kamati yake kuanzia Januari 2014 hadi Januari 2015.

Alisema muswada huo ni moja kati ya kilio cha wadau wa habari nchini ambao unatarajiwa kuikomboa taaluma hiyo kwa kusimamia masuala yote yanayohusu taaluma hiyo muhimu duniani.

Akizungumzia huhusu Mfuko wa Maendeleo ya Vijana na Wanawake, Mwenyekiti Mtanda alipendekeza kuwa halmashauri zote nchini ambazo hazijatenga asilimia 5 ya wanawake na asilimia 5 ya vijana ziorodheshwe na zichukuliwe hatua kali.

Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, tangu kuanzishwa kwa Mfuko wa Mandeleo ya Vijana na Wanawake mwaka 1993, ni halamashauri chache zimekuwa zikitenga fedha hizo kama inavyotakiwa.

Katika taarifa yake, Mwenyekiti Mtanda alionesha kuridhishwa na maendeleo ya Mfuko wa Maendeleo ya Vijana wa halamashauri ya Wilaya ya Temeke ulio chini ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo.

Alisema katika ziara ya kutembelea mfuko huo Januari 19 mwaka huu, walitembelea miradi ya vijana ya kikundi cha Sokoine Youth Development, Waungwana Youth Family na African Legends.

Kwa upande wa Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake, Mwenyekiti alizipongeza halmashauri ya mji Korogwe na zingine ambazo zimekuwa mfano wa kuigwa kwa kutenga fedha za mfuko huo na kuzitumia kama ilivyokusudiwa.

Mbali na mradi huo, alisema kamati pia ilitembelea mradi wa vituo vya kurushia matangazo ya Redio Mafifi, Iringa na Kola Hill, Morogoro uliogharimu shilingi Milioni 200.

“Mradi wa Mafifi Gangilonga, Iringa ni katika ya miradi mikubwa ya kufunga mitambo ya kurushgia matangazo katika vituo 9…Maeneo yaliyonufaika na mradi huu ni mkoa wa Manyara, Morogoro, Moshi, Mpanda, Newala, Shinyanga, Songea na Tunduru” alisema Mtanda.

Alisema mradi huo umewezesha kupatikana kwa matangazo ya redio kwa ubora zaidi ambapo matangazo hayo yanapatikana katika masafa ya FM-TBC Taifa (107.1MHz) na TBC FM (96.2MHz).

Aliongeza kuwa mradi huo umeweza kuongeza usikivu wa matangazo ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kwani kwa sasa yanasikika katika maeneo mengi zaidi nje ya mji wa Iringa. 

Mafunzo ya Ufundi kwa Vijana
Na Lorietha Laurence-Maelezo, Dodoma
SERIKALI kupitia Wizara ya kazi na Ajira imetenga kiasi cha shilingi bilioni 3 kwa mwaka wa fedha wa 2014/2015 kwa  ajili ya kutekeleza  mpango wa kukuza ajira kwa vijana.

Hayo yalisemwa na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Anne Kilango Malecela, akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Susan Lyimo kuhusu mkakati wa serikali kuwakopesha vifaa wahitimu wa mafunzo ya Veta ili kujiajiri.

Aidha aliongeza kuwa kupitia mpango huo, Serikali ina lengo la kuwapatia vijana  mitaji yenye masharti nafuu na nyenzo za uzalishaji mali ili waweze kujikimu kimaisha na kuondokana na tatizo la ukosefu wa ajira.

“Ili kufanikisha hili nawaomba vijana waliohitimu mafunzo ya ufundi waweze kujiunga katika vikundi  kwa kuandika mpango mradi kwa ajili ya kuomba mkopo ili  kupata  mitaji na vitendea kazi” alisema Kilango.

Aliongeza kwamba Halmashauri za wilaya, Miji na Majiji zimekuwa zikitenga  asilimia 5 ya bajeti zake kila mwaka kwa ajili ya kuwawezesha vijana kupata mikopo wakiwemo wahitimu wa mafunzo ya ufundi stadi kutoka vyuo vya VETA.


Vilevile  alieleza  kuwa ili kuhakikisha  vijana wanaohitimu  vyuo vya ufundi stadi  wanaweze kujiajiri  mada   zinazohusu Taasisi za Fedha pamoja na somo la ujasiriamali zimekuwa zikitolewa ili kuwawezesha kujiajiri na kupata mikopo.


Serikali imejizatiti kukabiliana na ujangili
Na Lorietha Laurence-Maelezo,Dodoma
SERIKALI imejizatiti katika kudhibiti ujangili na biashara haramu ya mazao ya maliasili kwa kuridhia na kutekeleza  mikataba minne ya kudhibiti ujangali wa tembo na unaovuka mipaka na kulinda mapori ya akiba.

Hayo yalisemwa na Naibu Waziri wa Utalii na Maliasili Mahmoud Mgimwa, bungeni Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mch. Peter Msigwa Mbunge wa Iringa Mjini kuhusu utekelezaji wa maazimio  ya kimataifa kukomesha ujangili nchini.

Alisema Tanzania imeridhia na kutekeleza mkataba wa kudhibiti ujangili na biashara ya wanyama walioko hatarini kutoweka kama tembo (CITES) kuhifadhi na kulinda maeneo ya Urithi wa dunia kama pori la akiba la Selous(UNESCO), kudhibiti ujangili unaovuka mipaka (INTERPOL na LATF).

Naibu Waziri Mgimwa alisema  katika kutekeleza maazimio hayo serikali iliandaa mikutano miwili ya kimataifa ya uhifadhi iliyofanyika mwezi Mei jijini Arusha na Dar es Salaam kwa kushirikisha wadau wa maendeleo na mashirika ya kimataifa.

“Maazimio ya kikao cha mjini Arusha,  Tanzania iliridhia makubaliano maalum ya kikanda kudhibiti uhalifu dhidi ya wanyama pori na ujangili unaovuka mipaka ya nchi za Burundi, Kenya, Malawi, Msumbiji, Uganda, Zambia na Sudani Kusini”alisema Mgimwa.

Aliongeza kuwa Serikali ilizindua mkakati wa kitaifa wa uzuiaji ujangili na biashara haramu ya wanyamapori pamoja na mfuko wa pamoja (Basket Fund) kukabiliana na ujangili.

Vilevile Tanzania imefanikiwa kupata faida mbalimbali kwa kutekeleza maazimio hayo ikiwa ni Euro 30,000 na USD 100,000 zilitolewa na UNDP, vifaa mbalimbali vya doria  ikiwemo magari 21, helicopter, mahema ,binocular na sare pamoja na kuwajengea uwezo watumishi 100  kwa kuwapatia mafunzo ya  kudhibiti  ujangiri.

Hata hivyo alisema inaendelea kujenga uwezo wa rasilimali watu, fedha na vitendea kazi katika ukusanyaji na utumaji wa taarifa za kiintelijensia kwa kushirikiana na wananchi pamoja na Taasisi za ndani na nje ya nchi katika kudhibiti ujangili unaovuka mipaka.

No comments:

Post a Comment