Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Aggrey Mwanri akijibu maswali ya wabunge
bungeni Dodoma.
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Hussein Mwinyi akijibu swali la mbunge Bungeni Dodoma.
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleoa ya Makazi Angellah Kairuki, akijibu swali la mbunge Bungeni.
Mjumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, Capt. Mstaafu John Chiligati akiwasilsha taarifa ya kamati yake.
Baadhi ya wageni wa Spika waliohudhuria Bunge, wakiongozwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Ernest Mangu(wa kwanza mstari wa chini).Kulia kwake ni Kamishna wa Jeshi la Magereza (CGP) John Casmir Minja.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge, Jenista Mhagama akijibu swali la Mbunge la Mbunge wa Rombo Joseph Selasini.
Naibu Waziri wa Elimu, Anne Kilango akijibu hoja za Wabunge.
Mwenyekiti Mpya wa Bunge la Jamhuri Kidawa Hamidi Saleh
Serikali yafanikiwa kujenga Barabara za km 42 mjini Dodoma
Na Lorietha Laurence-Maelezo, Dodoma
SERIKALI kupitia mradi
wa uendelezaji miji (TSCP) imefanikiwa kujenga barabara zenye urefu wa kilometa
42 kwa mji wa Dodoma kwa msaada wa mfuko wa Benki ya Dunia.
Waziri wa Nchi Ofisi ya
Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge, Jenista Mhagama ameeleza hayo Bungeni
Dodoma, kuwa ujenzi huo wa barabara umehusisha pia ujenzi wa mifumo ya maji ya
mvua ,dampo la kisasa kwa kijiji cha Chidaya pamoja na mitambo y usombaji taka.
“Maboresho hayo ya
miundombinu kwa mji wa Dodoma, ni kuhakikisha kuwa mji mkuu huu wa Tanzania
unakuwa katika madhari mazuri na yenye kukidhi haja za wananchi wake”, alisema
Waziri Mhagama.
Alizitaja barabara
hizo kuwa ni pamoja na maboresho ya
barabara ya Mwanza, Barabara ya 6 hadi 11,Barabara za Nkuhungu na
Chamwino-chang’ombe zenye jumla ya
kilomita 15.7 ambapo ujenzi umekamilika kwa asilimia 100.
Aidha aliongeza kuwa
jumla ya kilomita 27.12 za barabara za pembezoni mwa mji nazo zilijengwa kwa
kiwango cha lami ambazo ni Area A kilomita 5.82, Kikuyu kilomita 5.65,Kisasa
kilometa 12.90 na Chamwino kilometa 2,75.
Hata hivyo, alisema Benki ya Dunia imeahidi kutoa
Dola za Kimarekani milioni 7.66 kwa
ajili ya kukamilisha mapungufu yaliyojitokeza katika awamu ya kwanza kwa ajili
ya ujenzi wa barabara ya Independence na barabara ya mbeya kuelekea uhindini.
Wamiliki wa Shule Binafsi, Serikali watakiwa kuzingatia kiwango cha ufaulu
Na
Lorietha Laurence-Maelezo, Dodoma
NAIBU Waziri wa Elimu
na Mafunzo ya Ufundi Anna Kilango Malecela ametoa wito kwa wamiliki wote wa
shule binafsi pamoja na za Serikali kuzingatia kiwango cha ufaulu kutoka kidato
kimoja kwenda kingine kilichowekwa na Serikali.
Akijibu swali la Mbunge
wa Rombo, Joseph Selasini, bungeni mjini Dodoma aliyetaka kujua kama Serikali
inajua na kuunga mkono kiwango cha ufaulu
kwa shule zisizo za Serikali zinazoweka viwango maalum vya ufaulu
tofauti na vile ilivyoviweka.
Naibu Waziri Anne
Kilango alisenma Serikali haiungi mkono utaratibu huo kwa kuwa umekiuka waraka wa
elimu namba 12 wa mwaka 2011 na waraka Namba 4 wa mwaka 2012.
“Napenda kusisitiza
kuwa yeyote atakayekaidi maelekezo haya ya serikali atachukuliwa hatua kali za
kinidhamu kwa mujibu wa sheria ya elimu Namba 25 sura ya 353 kifungu cha 35”
alisema Kilango.
Aliongeza kuwa Waraka
wa Elimu Na. 6 wa mwaka 2011 umetoa maelekezo kuhusu wastani wa ufaulu katika
mtihani wa Kitaifa wa kidato cha pili ambao ni asilimia 30.
Hivyo aliwataka walimu
waelewe kuwa wanafunzi wanatofautiana katika uelewa hivyo kuweka kiwango
kikubwa cha wastani kunasababisha wanafunzi kukosa fursa ya kuendelea na masoma
na hivyo kuanza utaratibu mpya ya kutafuta shule.
Alibainisha kuwa Serikali
itazindua program ya KKK Februari 7, 2015 ikiwa na nia madhubuti ya kuboresha
elimu kwa shule zote za serikali katika kutoa elimu bora kwa wananchi.
Bunge laridhika na hali ya ulinzi na usalama wa raia
Na Hussein Makame-MAELEZO, Dodoma
BUNGE
limeridhishwa na hali ya ulinzi wa nchi, usalama wa raia na mali zao kwa
kipindi cha mwezi Februari mwaka 2014 hadi Januari mwaka huu kutokana na hali
ya ulinzi wa nchi na usalama wa raia kuwa shwari.
Hayo
yamesemwa na Kamati ya Bunge ya Ulinzi na Usalama kupitia Mjumbe wa kamati hiyo
Capt. Mstaafu John Chiligati wakati akiwasilisha taarifa ya kamati hiyo kwa
kipindi cha mwezi Februari 2014 hadi Januari 2015, bungeni mjini Dodoma.
Alisema
pamoja na hali kuwa shwari kulikuwepo na changamoto chache za uvunjifu wa
amani, vitendo vya uporaji mali na
matukio ya mauaji ya vikongwe na watu wenye ualbino yaliyotokea katika
baadhi ya mikoa.
“Katika
ziara ya kamati pamoja na taarifa kutoka kwenye wizara husika, Kamati ilibaini
kuwa kwa ujumla hali ya ulinzi wa nchi na usalama wa raia katika kipindi hiki
ilikuwa shwari” alisema Capt. Mstaafu Chiligati na kuongeza.
“Ijapokuwa
zipo changamoto chache za uvunjifu wa amani na vitendo vya uporaji mali na matukio ya mauaji ya vikongwe na watu wenye
ualbino yaliyotokea katika baadhi ya mikoa”
Capt.
Mstaafu Chiligati alilipongeza Jeshi la Ulinzi la Wananchi kwa kazi kubwa na
nzuri inayofanya ya kulinda mipaka ya nchi kwani katika kipindi hiki hali ya
mipaka ya nchi imekuwa shwari.
Alibainisha
kuwa ili kudumisha hali iliyopo, aliishauri Serikali itenge fedha za kutosha
ili kuviwezesha vyombo vya ulinzi na usalama kufanya kazi nzuri zaidi na
kuifanya hali ya nchi kendelea kutulia na kuwa na amani na utulivu.
Kwa upande
wa masuala ya Ulinzina Usalama wa Mipaka, Capt. Mstaafu Chiligati alisema
katika kipindi hicho hali katika mipaka yote ya Tanzania imekuwa shwari licha
ya kuwepo kwa changamoto ya uingiaji wa wahamiaji haramu.
Kutokana na
hali hiyo Kamati hiyo ililipongeza pia Jeshi la Polisi nchini kwa jitihada za
kudhibiti uhalifu kote nchini na kupunguza matukio ya uhalifu katika baadhi ya
maeneo yaliyokubwa na matukio hayo hivi karibuni.
“Aidha
Kamati ilipotembelea mkoa wa Arusha iliridhika na hali ya kupungua kwa matukio
ya uhalifu na pia ilikuta hali ya utulivu na amani imerejea katika jiji la
Arusha” alisema Capt. Mstaafu Chiligati.
Alieleza
kuridhishwa kwa kamati na taarifa za kukamtwa na kufunguliwa kesi mahakamani
kwa baadhi ya watuhumiwa wa matukio ya kigaidi yaliyotokea katika mkoa wa
Arusha.
Hata hivyo
kamati alishauri kwamba kesi hiyo isikilizwe haraka na kutolewa hukumu ili
ikidhi matarajio ya wananchi.
Kwa upande
wa Mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa mujibu wa Sheria, kamati iliishauri
Serikali kuongeza muda wa mafunzo hayo kutoka miezi 3 hadi miezi 6 huku
ikiitaka Serikali kuwachukulia hatua za kisheria wanafunzi wanaokwepa
kuhudhuria mafunzo bila ya sababu za msingi.
Aliishauri
Serikali kupitia Wizara ya Ulinzi na JKT na ile ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi
kukaa pamoja ili kutafuta njia ya kuoanisha mihula ya vyuo ili isigongane na
muda wa mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria.
Serikali kuweka mikakati makini kulinda Utamaduni wa Mtanzania
Na
Lorietha Laurence-Maelezo Dodoma
SERIKALI imeweka
mikakati mahususi kuhakikisha utamaduni wa Mtanzania unalindwa ili kuepushwa kuathiriwa na mabadiliko ya teknolojia na utandawazi.
Hayo yamsemwa na Naibu
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Juma Nkamia, wakati akijibu swali
la Mbunge wa Viti Maalum, Amina Mwidau, aliyetaka kujua Serikali ina mikakati
gani ya kuimarisha sera na kanuni mbalimbali kudhibiti matumizi ya utandawazi na teknolojia.
Naibu Waziri Nkamia alisema
sera hizo znasiamamiwa na Baraza la
Kiswahili Tanzania, Bodi ya Filamu Tanzania, pamoja na kamati ya maudhui iliyo
chini ya Mamalaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ambayo husimamia maudhui ya
vyombo vya habari.
“Hata hivyo natoa wito
kwa wananchi kushirikiana na serikali kuhakikisha kuwa tunalinda na kudumisha utamaduni
wetu kwa kila mmoja kuwa mlinzi wa mwenzake “ alisema Nkamia.
Aidha aliongeza kuwa
Serikali itaendelea kuhamasisha jamii kuongeza uzalishaji wa bidhaa na huduma zenye
kuimarisha utambulisho wa Tananzania kwa kununua na kutumia bidhaa hizo.
Naye Mariam
Msabaha Mbunge wa Viti Maaluma alihoji
hatua zilizochukuliwa na serikali katika
kuzuia filamu zisizo na maadili kuingia nchini, ambapo Naibu Waziri Nkamia alisema
kuwa Bodi ya Filamu Tanzania inahusika katika kuhakiki maudhui ya filamu kutoka
nje kabla ya kuingia sokoni na kwa zile zinazoingia kwa njia ya magendo husakwa
na kuteketezwa kwa moto.
“Hakuna filamu
inayoingia nchini bila ya kukaguliwa na watu wa Bodi ya Filamu ili kujiridhisha
na maudhui yake na hivyo kuweza kuingia sokoni tayari kwa kutumiwa na
watanzania”. alisema Nkamia.
Vilevile alieleza kuwa wizara yake imejipanga katika kuongeza kasi ya kutoa taarifa kwa umma kuhusu utendaji wa
kazi zake ikiwemo tafiti mbalimbalili zinazofanywa.
Bunge
lafanya uteuzi wa Wenyeviti wapya
Na Hussein
Makame-MAELEZO, Dodoma
BUNGE la
Jamhuri la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limewateua Mbunge wa Viti Maalum
(CCM), Lediana
Mng'ong'o na Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Kidawa
Hamidi Saleh kuwa wenyeviti wa Bunge
hilo.
Akitangaza uteuzi
huo Bungeni mjini Dodoma, Spika wa Bunge Anne Makinda alisema wenyeviti hao
wapya wanachukua nafasi za aliyekuwa mwenyekiti wa Bunge ambaye sasa ni Waziri
wa Nchi, Sera, Uratibu na Bunge, Jenista Mhagama.
Kufuatia
uteuzi huo Mwenyekiti Mng’ong’o ameanza kazi leo baada ya kipindi cha maswali
na majibu Bungeni kilichokuwa chini ya Mwenyekiti Musa Azzan Zungu.
Pika Makinda
alisema Mwenyekiti mpya Kidawa anachukua nafasi ya aliyekuwa mwenyekiti wa
Bunge hilo kutoka upande wa Zanzibar ambaye kwa sasa hayupo kutokana na kazi
maalum, Mohamed Seif Khatibu.
Alifafanua
kuwa uteuzi huo umefanywa na Kamati ya Bunge ya Utawala ambayo ilikaa jana
mchana na kupitisha majina hayo ambayo aliyapeleka Bungeni ili kupigiwa kura na
wabunge.
Hivyo, Spika
Makinda aliwaomba wabunge kupiga kura ya ndio au hapana kuthibitisha uteuzi
huo, ambapo wabunge walipitisha uteUuzi huo kwa kupiga kura ya ndio na kubariki
wenyeviti hao wapya.
Serikali yaendelea kupokea fidia ya athari ya vita kutoka Uganda
Na Lorietha Laurence-Maelezo Dodoma
Na Lorietha Laurence-Maelezo Dodoma
SERIKALI ya Tanzania
imepokea takribani shillingi bilioni 15.5 kutoka Serikali ya Uganda ikiwa ni
fidia itokanayo na athari za vita vya
Kagera.
Naibu Waziri wa Fedha
Adam Malima ameeleza hayo Bunge mjini Dodoma kuwa fidia iliyokuwa inatakiwa kulipwa ni Dola za Marekani milioni 18.4 ingawa Uganda imelipa Dola
milioni 9.7 zilizoingizwa kwenye mfuko mkuu wa Hazina.
“Kiasi hicho cha fedha kilipokelewa na kuwekwa katika Mfuko Mkuu wa Hazina kwa ajili ya
matumizi ya maendelao ya wananchi ” alisema Malima.
Alibainisha kuwa taratibu za fidia zitokanazo na hasara za
vita hiyo zinaongozwa na sheria na kanuni
za kimataifa pamoja na utaratibu wa kutathmini kiwango cha hasara
kitokanacho na vita.
Aliongeza kuwa licha ya
kwamba vita hivyo viliathiri taifa zima la Tanzania ,mkoa wa Kagera umepokea
fedha kutoka Mfuko Mkuu wa serikali ambayo imesaidia kusukuma maendelao ya
wananchi.
No comments:
Post a Comment