TANGAZO


Monday, February 9, 2015

Balozi Seif Idd alipongeza Shirika la Misaada ya Maendeleo la Marekani (USAID)

Kamanda Philip Knightsheen akitoa salamu za Shirika lake linalosimamia huduma za Kibinaadamu  na Afya la Usafricom  kwenye mafunzo ya siku tano ya zoaezi la kukabiliana na maafa Zanzibar hapo Zanzibar Beach Resort Mazizini. 
Mwakilishi wa shirika la Misaada la Marekani Us Aid Bibi Anna Senga akizungumza katika mafunzo ya siku tano kuhusu zoezi la kukabiliana na maafa Zanzibar. 
Waziri wa Ncho Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Moh’d Aboud Moh’d  akimkabidhi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Ripoti ya Maafa Zanzibar.
Mkurugenzi wa Idara ya Maafa Zanzibar Nd. Ali Juma Hamad wa kwanza kutoka kulia akiwa na baadhi ya watendaji wa Idara hiyo wanaoshiriki mafunzo ya sku tano kuhusu zoezi la kukabiliana na maafa Zanzibar.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya siku tano kuhusu zoezi la kukabiliana maafa Zanzibar yanayofanyika Hoteli ya Zanzibar Beach Resort Mazizini.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya siku tano kuhusu zoezi la kukabiliana maafa Zanzibar yanayofanyika Hoteli ya Zanzibar Beach Resort Mazizini.
Mwakilishi wa shirika la Misaada la Marekani Us Aid Bibi Anna Senga akibadilishana mawazo na Makamu wa Pili wa  Rais wa Zanzibar Balozi Seif nje ya ukumbi wa Zanzibar Beach Resort mara baada ya kufunguliwa rasmi mafunzo ya zoezi hilo. Nyuma ya Balozi Seif ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Idara Maalum Mh. Haji Omara Kheir. Kulia ya Balozi Seif ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Moh’d Aboud Moh’d  na  Mwakilishi wa Shirika  linalosimamia huduma za Kibinaadamu  na Afya la Usafricom Kamanda Philip Knightsheen. 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo ya siku tano kuhusu zoezi la kukabiliana na maafa Zanzibar yanayofanyika  Hoteli ya Zanzibar Beach Resort. Kushoto ya Balozi Seif ni Mwakilishi wa shirika la Usafricom  Kamanda Philip Knightsheen, Waziri wa Afya Zanzibar, Mh. Rashid Seif, Kaimu  Kamanda wa Brigedia Nyuki Zanzibar  na Mkuu wa Mkoa Mjini  Magharibi Mh. Abdulla Mwinyi. Kulia ya Balozi Seif ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Moh;d Aboud Moh’d, Mwakilishi wa shirika la Misaada la Marekani Us Aid Bibi Anna Senga, Waziri wa Nchio Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum Mh. Haji Omara Kheir, na Msadizi  Kamishna wa Polisi  Kamanda Hassan Nassir. (Picha zote na Hassan Issa – OMPR – ZNZ)

Na Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
9/2/2015.
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi ameipongeza Serikali ya Watu wa Marekani kupitia Shirika lake la Misaada ya Maendeleo la Us aid kwa jitihada zake za kuisaidia Zanzibar katika mipango yake ya kutafuta mbinu za kuwa tayari kwa kukabilana na maafa wakati wowote yatapotokezea.

Alisema Zanzibar imekuwa na historia pana ya majanga mbali mbali yaliyowahi kuikumba na kusababisha maafa makubwa  yatayoendelea kukumbukwa na vizazi vya sasa na vile vijavyo.

Balozi Seif alitoa pongezi hizo wakati akifungua rasmi  mafunzo ya siku tano kuhusu zoezi la kukabiliana na maafa Zanzibar yanayofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Zanzibar Beach  Resort Mazizini nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Alisema Marekani imekuwa mshirika mkubwa katika kusaidia harakati mbali mbali za maendeleo ya miundo mbinu ya mawasiliano ya Bara bara, huduma za Afya na ustawi wa Jamii wa Zanzibar jambo ambalo limekuwa likileta faraja kwa Wananchi walio wengi hapa Nchini.

Balozi Seif alifahamisha kwamba juhudi za Zanzibar katika kujiweka tayari kukabiliana na maafa yoyote yatakayoweza kutokea zimekuja kufuatia majanga tofauti yaliyowahi kutokea kama  maradhi ya Kolera, ajali za vyombo vya usafiri wa Baharini na majanga ya  moto ambayo yamesababisha vifo vya watu kadhaa.

“ Zanzibar imeshuhudia maradhi ya kolera karibu miaka 20 iliyopita na kukumbwa na ajali za usafiri wa Baharini miaka michache iliyopita na kulazimika kuchukuwa jitihada za tahadhari katika kukabiliana nayo endapo yatatokezea tena “. Alisema Balozi Seif.

Alifahamisha  kwamba Zanzibar ikiwa miongoni mwa Mataifa machanga Duniani inawajibika kuimarisha Idara yake ya Maafa kwa kushirikiana na taasisi za ulinzi, Afya na Mawasiliano ili kuona huduma za kukabiliana na maafa Nchini zinapatikana kwa ubora unaokusudiwa.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kuwa ile nia ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kujenga vituo vya mafunzo na uokozi wakati yanapotokea maafa katika  eneo la Nungwi Mkoa wa Kaskazini   Unguja na Chake chake kwa Pemba bado iko pale pale.
Alisema kilichokwamisha utekelezaji wa mpango huo kwa sasa ni upatikanaji wa vifaa na fedha licha ya juhudi kadha zinazoendelea kuchukuliwa  na Serikali kuu katika kuomba misaada ya kiufundi kwa Taasisi za Kimataifa zilizobobea katika taaluma hiyo muhimu.

Balozi Seif alieleza kuwa katika kuimarisha huduma za kukabiliana na maafa Nchini Mswada wa Sheria ya Kuanzisha Sheria ya Kupunguza na Kukabiliana na Maafa Zanzibar  uliwasilishwa na  kujadiliwa na Baraza la Wawakilishi Zanzibar  hivi karibu na hatimae kupitishwa katika Mkutano wa 18 wa Baraza hilo.
Alisema  Mswada huo ulikusudiwa kuweka sheria mpya inayoweka mfumo wa kisheria katika shughuli za kukabiliana na maafa na mambo ambayo yataondosha mapungufu yanayoonekana katika sheria iliyopo hivi  sasa.

Balozi Seif alisisitiza kwamba Sheria hiyo mpya itawiana na Sera ya Kukabiliana na Maafa ya  mwaka 2011 pamoja na Makubaliano na Mikataba ya Kikanda na Kimataifa inayohusiana na masuala ya kukabiliana na maafa iliyoridhiwa na nchi yetu.
Mapema Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Ahmad Kassim alisema lengo la zoezi hili la kukabiliana na maafa Zanzibar ni kujenga nguvu za pamoja kati ya Taasisi za Umma, binafsi zikiungwa mkono na washirika wa maendeleo.

Nd. Ahmad alisema kwa vile majanga yanapotokea  yanakumba kila kilichoko mbele yake ushirikiano wa karibu unahitajika kwa pande zote zinazohusika ili kujiweka tayari kukabiliana na majanga yoyote yanapotokezea.

Wakitoa salamu za Taasisi zao za kimataifa zinazoshiriki zoezi hilo Mwakilishi wa Shirika linalosimamia huduma za Kibinaadamu  na Afya la Usafricom,  Kamanda Philip Knightsheen  na Mwakilishi wa shirika la Misaada la Marekani Us Aid Bibi Anna Senga walisema suala la ulinzi wa maisha ya Mwanadaamu linamuhusu kila mwana jamii.

Walisema licha ya kwamba nguvu kubwa imewekwa kwa vikosi vya ulinzi na uokozi kukabiliana na maafa yanapotokea, lakini bado jukumu hilo litaendelea kusimamiwa kwa pamoja na taasisi zote za umma,binafsi kwa kushirikiana na washirika wa maendeleo.
Wawakilishi wa taasisi hizo za Kimataifa walisema kwamba Nchi za Malawi, Msumbiji na Senegal zinazokuwa zikikabiliana na mafuriko ya mara kwa mara zimekuwa zikipata msaada ya kibinaadamu kwa lengo la kuwapa matumaini wananchi wake wanaokumbwa na kadhia hiyo.

Waliahidi kwamba Taasisi na mashirika ya maendeleo ya Kimataifa wakiyatolea mfano yale ya Unicef, WHO,Usafricom,CDHAM  na mengine ya kujitolea yataendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kukabiliana na majanga na maafa wakati yanapotokea.

Akimkaribisha mgeni rasmi kufungua zoezi hilo Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu  wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh.  Moh’d Aboud  Moh’d  alizishukuru Taasisi inayohudumia masuala ya Kibinaadamu na Afya {USAFRICOM} na ile ya kujikinga na Majanga ya Kibinaadamu { CDHAM } kupitia Serikali ya Marekani kwa kukubali kugharamia mafunzo ya zoezi hilo.

Waziri Aboud alisema msaada wa Taasisi hizo utasaidia kuwawezesha washiriki wa mafunzo hayo kutoka Mataifa mbali mbali rafiki kupata taaluma pana itayoweza kuwasaidia katika kutekeleza majukumu yao kwenye taasisi wanazotokea.

Mafunzo hayo ya  siku tano kuhusu zoezi la kukabiliana na maafa Zanzibar yanayofanyika  katika ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya Zanzibar Beach Resort yameshirikisha wawakilishi wa Taasisi za ulinzi, maafa, Utawala, pamoja na wataalamu wa Afya kutoka nchi mbali mbali Duniani.

No comments:

Post a Comment