Mwezeshaji kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bibi Ester Riwa akitoa mada ya Stadi za Maisha kwa vijana wa Wilaya ya Ileje walioudhuria semina ya Ujasiriamali, Ujuzi, Stadi za Maisha na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana jana katika Wilaya ya Ileje Mkoa wa Mbeya.
Baadhi ya Vijana wa
Wilaya ya Ileje wakifuatilia kwa makini mafunzo yaliyokua yakiendelea wakati wa
semina ya Ujasiriamali, Ujuzi, Stadi za Maisha na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana
jana katika Wilaya ya Ileje Mkoa wa Mbeya.
Na Genofeva Matemu –
Maelezo, Mbeya
Tarehe 23/01/2015
HALMASHAURI ya Wilaya
ya Ileje Mkoa wa Mbeya yaishukuru serikali kupitia Wizara ya Habari, Vijana
Utamaduni na Michezo kuwakopesha Shilingi Milioni 10 zilizokopeshwa katika
Saccoss za vijana wa Wilaya hiyo.
Kauli hiyo imetolewa na
Afisa Maendeleo ya jamii Bw. Rodrick Sengela walipotembelewa na ujumbe kutoka
Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo jana kwa ajili ya kutoa elimu ya
Ujasiriamali, Stadi za Maisha, Ujuzi na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana kwa vijana
wa Wilaya ya Ileje Mkoa wa Mbeya.
“Tunaishukuru Wizara ya
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana
kuwakopesha vijana wa Ileje shilingi milioni 10 zilizokopeshwa mwaka 2005 na
kupelekwa katika Saccoss ya Vijana ya Ngulilo na Saccoss ya Vijana ya Chitete
zilizotumika kuendeleza shughuli za vijana katika Wilaya” alisema Bw. Sengela.
Hata hivyo Bw. Sengela
amesema kuwa Wilaya ya Ileje imekua ikijitahidi kuiendeleza jamii ya Ileje
kwani kwa mwaka wa fedha 2014/2015 Wilaya imeshachangia shilingi million 6
katika mfuko wa vijana na wanawake kutimiza agizo la kila Halmashauri kuchangia
alisimia 5 katika mfuko huo kuwaendeleza vijana na wanawake.
Kwa upande wake
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Ileje Bw. Musa J. Otieno amesema
kuwa Wilaya ya Ileje imekua na changamoto kubwa kutokana na Wilaya hiyo kuwa
mpakani na nchi ya Malawi kwani vijana wengi wamekua na tabia ya kuchukua
mikopo inayotolewa na Serikali na kuhamia nchi ya Malawi hivyo kuifanya Wilaya
hiyo kushindwa kurejesha mikopo hiyo.
Aidha Mwezeshaji kutoka
Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bibi Ester Riwa amewataka vijana
wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje kuwatumia viongozi wa Wilaya yao kupata mbinu
mbadala za kuijasiriamali na kutumia mikopo wanayoipata kuendeleza shughuli za
maendeleo zilizopo katika Wilaya hiyo.
Bibi Riwa amesema kuwa
Wilaya ya Ileje imehamasika na zoezi la kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa
vijana linalofanywa na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo hivyo
kuwataka vijana wote waliopata mafunzo hayo kuyatekeleza na kuyatoa kwa vijana
wengine ambao hawakubahatika kuhudhuria mafunzo hayo.
No comments:
Post a Comment