TANGAZO


Wednesday, January 7, 2015

Rais Dk. Shein: Serikali ya Muungano wakati wote itazingatia umuhimu wa kuwapatia wanajeshi huduma zao

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein.

Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wote itazingatia umuhimu wa kuwapatia wanajeshi huduma zao kwa kadiri hali ya uchumi inavyoruhusu likiwemo suala zima la kuwapatia makaazi bora katika makambi yao.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein aliyasema hayo katika  hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa nyumba 320 za makaazi ya Wanajeshi katika Kambi ya Ali Khamis kisiwani Pemba, ikiwa ni miongoni mwa  shamra shamra za maadhimisho ya miaka 51 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Katika hotuba yake Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inazingatia suala la umuhimu wa makaazi kwa  Wanajeshi kama ni moja ya mahitaji muhimu kama ilivyo kwa vitendea kazi vyengine.

“Ni jambo la kushukuru kwamba leo tumefikia hatua hii ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa nyumba hizo pia, napenda nikuahidini kwamba juhudi hizi hazitaishia kwenye mradi huu kwani lengo letu ni kuona wanajeshi wetu wote wanaishi kambini”,alisema Dk. Shein

Aidha, Dk. Shein alisema kuwa Serikali ys ajasmhuri ya  Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar zinathamini jukumu muhimu linalotekelezwa na Jeshi la Ulinzi la Tanzania na Vikosi vyengine vya ulizni na usalama na  zote kwa pamoja zitaendelea kuzifanyia kazi changamoto zilizopo ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.

Dk. Shein alisema kuwa ni wazi kuwa suala la watumishi wakiwemo askari kuishi katika nyumba za kupanga lina changamoto zake na kusisitiza kuwa mradi huo  ni kielelezo cha dhamira ya dhati ya Serikali kupunguza tatizo la makaazi kwa wanajeshi wake.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alisema kuwa katika kipindi cha miaka 53 tangu upatikane uhuru wa Tanzania Bara na miaka 51 tangu yafanyike Mapinduzi Matukufu ya Januari 12, mwaka 1964, Jeshi la Wananachi wa Tanznia limeonesha uwezo mkubwa wa kiulinzi katika mipaka ya tanzania pamoja na operesheni mbali mbali za kimataifa ilizoshiriki.

Alisema kuwa uwezo, umahiri na nidhamu ya Jeshi la Tanzania kunaleta faraja na kutoa taswira njema ya ulizni wa Tanzania Kimataifa. “Kwa kweli, tunaona fahari kuwa na Jeshi lenye uwezo na sifa kama ilivyo kwa Jeshi la Wananachi wa Tanzania”,alisema Dk. Shein.

Dk. Shein alisema kuwa Jeshi la Wananachi wa Tanzania litabaki kukumbukwa kutokana na  mchango wake wa kusaidia wapiganaji uhuru Kusini mwa Bara la Afrika katika mika ya 70 na katika mapambano ya kumtoa Nduli Iddi Amin aliyeivamia Tanzania mnamo mwaka 1978.

Aidha, Dk. Shein alitoa pongezi zake kwa Jeshi hilo kutokana na umahiri wake ambao umeendelea kusikika huko Dafur- Sudan na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo  ambapo lilishiriki katika operesheni za kusimamia amani za kimataifa sambamba na kusifu mchango wake katika michezo pamoja na kutoa huduma za afya na elimu kwa jamii.

Dk. Shein alitumia fursa hiyo kwa kutoa shukurani kwa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kupitia Benki ya Exim ya China kwa kukubali kutoa mkopo uliowezesha utekelezaji wa ujenzi wa nyumba 6,064 hapa nchini katika awamu ya kwanza ya mradi wenye lengo la kujenga nyumba 10,000.

Alieleza kuwa hicho ni kielelezo chengine cha uhusiano mwema na wa kihistoria uliokuwa nao Jamhuri ya Watu wa China kwa zaidi ya miaka 50 hivi sasa ambapo pia, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuwapongeza wakandarasi wa Shangai Construction Group (General) Company ya China ambao wanaendelea kutekeleza mradi huo wa ujenzi wa nyumba za wanajeshi.

Sambamba na hayo, Dk. Shein alisema kuwa ni wajibu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kutambua uzito wa jukumu kubwa liliyopo katika kuhakikisha usimamizi mzuri wa mradi huo ili utekelezaji wake uwe na ufanisi uliokusudiwa.

Mapema Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dk. Hussein Mwinyi alisema kuwa mchakato wa mradi huo ulianza rasmi mwaka 2011 kwa mazungumzo baina ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China na wafadhili ambapo makubaliano hayo ni kujenga nyumba 10,000 kwa makundi yote ya wnajeshi kwa gharama ya Dola za Kimarekani milioni 300.

Alisema kuwa katika fedha hizo Serikali ya Tanzania inachamgia Dola milioni 15 na Dola milioni 285 zilizobaki ni za mkopo nafuu kutoka Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kupitia Benki ya Exim ya China.

Alisema kuwa awamu ya kwanza ya ujezni huo imeanza kwa vikosi vilivyopo mikoa ya Dar-es-Salaam na Pwani ambapo jumla ya nyumba 391 za familia 3,128 zinajengwa na kuendelea kueleza kuwa ujenzi wa nyumba 145 kwa familia 1,160 zilziokuwa zikijengwa kwenye maeneo manne ya Dar-es-Salaam umekamilika na tayari zimeshakabidhiwa kwa Jeshi la Wananachi wa Tanzania.

Dk. Mwinyi alisema kuwa ujenzi wa nyumba 141 zilzobaki kwa Mkoa wa Dar-es-Salaam za familia 1,128 zikzo katika hatua ya umaliziaji na zinatarajiwa kukabidhiwa muda wowote mwezi huu huku akieleza kuwa awamu ya pili ya ujenzi wa nyumba 329 kwa familia 2,632 kwenye maeneo ya vikosi vilivyopo mikoa ya Arusha, Dodoma, Morogoro, PEMBA na Tanga ilianza mnamo mwezi Oktoba mwaka jana.

Mapema Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Wananachi wa Tanzania Luteni Jenerali Samuel Ndomba, alieleza juhudi zinazoendelea katika ujenzi huo sambamba na azma ya ujenzi wa nyumba hizo wa Wanajeshi.

No comments:

Post a Comment