TANGAZO


Friday, January 9, 2015

Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Magdalena Sakaya ailalamikia CCM kuwachezea rafu Wenyeviti Serikali za Mitaa

*Amtaka Rais Kikwete kumwajibisha Waziri wa Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia
*Jeshi la Polisi latoa onyo kuhusu ghasia zilizotokea katika uchaguzi na kuapishwa washindi wa uchaguzi huo
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi Tanzania Bara, Magdalena Sakaya, akielezea jambo, wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam leo, kuhusu kile alichodai kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuendelea kuhujumu uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa kubatilisha matokeo ambayo chama hicho kilidai kushinda na pia kuapishwa kwa walioshindwa wa CCM badala ya walioshinda wa CUF. Kulia ni Ofisa Harakati na Matukio wa CUF, Nurdin Msati. (Picha zote na Kassim Mbarouk-www.bayana.blogspot.com)
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF)Tanzania Bara, Magdalena Sakaya, akielezea kusikitishwa kwake, wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam leo, kuhusu kile alichodai kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuendelea kuhujumu uchaguzi wa Serikali za Mitaa. 
Baadhi ya waandishi wa habari, wakichukua taarifa iliyokuwa ikitolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Tanzania Bara, Magdalena Sakaya, wakati alipokuwa akielezea kuhusu kile alichodai kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuendelea kuhujumu uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Baadhi ya wapigapicha wa vyombo mbalimbali vya Habari, wakichukua taarifa iliyokuwa ikitolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Tanzania Bara, Magdalena Sakaya, wakati alipokuwa akielezea kuhusu kile alichodai kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuendelea kuhujumu uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Baadhi ya waandishi wa habari, wakiwa kwenye mkutano huo na Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Tanzania Bara, Magdalena Sakaya, wakati alipokuwa akielezea kuhusu kile alichodai kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuendelea kuhujumu uchaguzi wa Serikali za Mitaa jijini leo.

Celina Mathew

CHAMA cha Wananchi (CUF), kimemtaka Rais Jakaya Kikwete kumwajibisha Mkurugenzi wa Wilaya ya kinondoni na Waziri wa Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia kwa kushindwa kuendesha uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Aidha, Chama hicho kimeonya CCM na serikali yake kuwa nguvu ya umma waliyokutana nayo kwenye uchaguzi huo itaongezeka kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.


Kauli hiyo inakuja siku chache baada ya kuapishwa kwa viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), aliodai kwamba hawakushinda kwenye uchaguzi huo, hivyo kusababisha vurugu kubwa katika baadhi ya maeneo zilizoambatana na mabomu ya machozi.


Hayo yalisemwa leo na Naibu Katibu Mkuu CUF Bara, Magdalena Sakaya alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi zao.

Alisema kitendo cha CCM kuapisha wenyeviti wa serikali za mitaa ambao hawakushinda kwenye uchaguzi huo na kuacha wagombea wa CUF walioshinda ni uchakachuaji mtupu hivyo lazima viongozi waliohusika wawajibishwa au kujiuzulu.

"Tunataka kuwaonya CCM kuwa moto tuliouonesha kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa ni sawa na fukuto tu. tumejipanga vizuri zaidi ya tulivyowadhibiti kwenye mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa na uapishwaji zilizo malizika hivi karibuni,"alisema. 

Sakaya alisema mchakato huo ulianzia kwenye ubatilishi matokeo ya maeneo mbalimbali ambayo Cuf imeshinda hivyo CCM wakaamua kujipanga kuvuruga zoezi hilo la kuapisha kwa wenyeviti hao wa serikali za mitaa.
Aliyataja baadhi ya maeneo ambayo yalitokea vurugu katika mchakato wa kuapishwa kuwa ni pamoja na Mtaa wa Mwinyimkuu, Kata ya Mzimuni Kinondoni ambapo Desemba 15 msimamizi wa uchaguzi huo alimtaja wa CUF Hassan Mwinchumu kuwa mshindi.

Baada ya mgombe huyo kutangazwa msimamizi huyo aliitisha uchaguzi mwingine Desemba 17 ambapo uligomewa na wananchi wa Mzimuni na baadaye msimamizi msaidizi kwa mara nyingine akamtangaza mgombe wa CCM Funua Ally kuwa ndiye mshindi.


Ambapo baada ya zoezi hilo la kutangazwa wananchi walilaani vikali na kumkataa lakini cha kushangaza alipewa barua ya kwenda kuapishwa ndipo wananchi wakazuia asiapishwe siku hiyo hali iliyosababisha vurugu.

Aidha alisema pia Mtaa wa Ukwamani Kata ya Kawe mgombea wa CUF alishinda na fomu za matokeo hazikusainiwa na kubandikwa hadi leo, badala yake CCM walichakachua fomu za matokeo na kuziwasilisha kwa Mkurugenzi wa Kinondoni.

Na kwamba wakati wa zoezi la kuapishwa aliyepewa barua ya kuapishwa ni mgombea wa CCM jambo lililosababisha wananchi kuzuia uapishwaji huo.

Alisema Mtaa wa Msisili A Kata ya Mwananyamala, msimamizi msaidizi wa uchaguzi alimtangaza mgomba wa CUF kuwa mshindi cha kushangaza kesho yake msaidizi huyo huyo akabandika matokeo ambayo yanaonesha mgombea wa CCM kushinda hali iliyosasabisha wananchi kuingilia kati kuzuia asiapishwe katika ukumbi wa LandMark Hotel.
Pia alisema katika Mtaa wa Kiwalani Kata ya Migombani uchaguzi huo ulivurugika na masanduku ya kura kuharibiwa na kesi hadi sasa iko katika kituo cha polisi Buguruni.

Alisema hata masanduku ya kura na kura zake ziko polisi kama vithibitisho na kitu cha kushangaza ni kuwa kwenye zoezi la kuapishwa jina la mgombea wa CCM Ubaya Chuma lilitangazwa na kupewa barua ya kuapishwa alipewa ndipo wananchi wakaingilia kati suala hilo.


Katika Mtaa wa Kigogo Fresh B matokeo hayakutangazwa baada ya vurugu kutokea lakini cha kushangaza kwenye kuapishwa jina la mgombea wa CCM Mariano Marius lilijitokeza jambo lililoashiria kuwa mtendaji wa Serikali za Mitaa alimpatia barua ya kuruhusiwa kuapishwa ambapo wananchi walizuia.

Aliongeza kuwa katika mitaa ya Kihiindwa na Malapa kuna wagombe wa CCM walitajwa kuwa washindi na kupewa barua ya kuapishwa jambo ambalo lilizua taharuki kwa wananchi na kuwasababishia kuzuia zoezi hili.

Alibainisha baadhi ya maeneo mengine yaliyofanyiwa hujuma kuwa ni pamoja na Kinyerezi, Migobani, Bunda (Mara) na kwamba wanaendelea kupokea malalamiko kama hayo.

Aidha Jeshi Polisi nchini limetoa onyo kwa wananchi waliohusika kwenye vurugu za uchaguzi wa wenyeviti wa serikali za mitaa na zoezi la kuapishwa kwa wenyeviti waliochaguliwa.

Pia limesema kama kuna mtu hajaridhika na matokeo ya uchaguzi huo afuate taratibu kwa kuwasilisha malalamiko kwenye ngazi husika ili kufanyiwa kazi kwa mijibu wa sheria.


Aidha, Jeshi hilo limewataka Wakurugenzi na Maafisa watendaji wenye dhamana ya kusimamia mchakato wa kuwaapisha wenyeviti waliochaguliwa, kufuatilia kwa karibu migogoro inayojitokeza na kuitatua migogoro hiyo mapema ili kuepusha migongano inayoweza kusababisha uvunjifu wa amani.


Taarifa hiyo ilitolewa Dar es Salam jana na Msemaji wa Jeshi la Polisi,Advera  Bulimba Kufuatia kukamilika kwa mchakato wa uchaguzi wa viongozi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji ambapo zoezi la kuapishwa kwa viongozi hao katika maeneo mbalimbali hapa nchini linaendelea.


"Kumejitokeza tabia ya baadhi ya wananchi kufanya vurugu na fujo katika zoezi hilo hivyo tunawapa onyo kali waache zoezi limalizike kwa amani lasivyo tutachukua hatua kali za kisheria,"alisema.

Alisema hali hiyo ilisababisha baadhi ya wananchi kujihusisha na vitendo vya kihalifu kwa kufanya fujo na vitendo vyavurugu ikiwemo kuwapiga baadhi ya watendaji wanaosimamia zoezi la kuapisha na kuwapiga viongozi wateule waliochaguliwa kihalali na wananchi kwa madai kuwa hawakushinda kihalali katika uchaguzi huo jambo ambalo ni kinyume cha sheria, kanuni  na taratibu za nchi.
"Jeshi la Polisi halitamvumilia mtu ama kikundi chochote kitakachofanya vurugu ama fujo kwa kisingizio cha ushabiki wa siasa na badala yake atakayebainika hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake,"alisema.

No comments:

Post a Comment