Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kati kati akimpongeza Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. George Masaju aliyekaa upande wa kulia kwa kuteuliwa kushika wadhifa huo. Aliyepo upande wa Kushoto ni Waziri wa Katiba na Sheria wa Sewrikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mh. Aboubakar Khamis Bakari. Mh. Masaju amefika Zanzibar kujitambulisha rasmi baada ya kuteuliwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete kushika wadhifa huo.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. George Masaju akitoa ahadi kwa Balozi Seif ya kufanya kazi zake kwa uadilifu wakati akijitambulisha rasmi kushika wadhifa huo. (Picha zote na – OMPR – ZNZ)
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
23/1/2015.
MWANASHERIA Mkuu wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. George Masaju ameahidi kutumia uzoefu wake alioupata katika ngazi ya Taifa na Kimataifa katika kuhakikisha jukumu alilokabidhiwa na Taifa analitekeleza katika misingi ya uadilifu.
Mh. George Masaju alitoa ahadi hiyo wakati wa mazungumzo yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akijitambulisha rasmi baada ya kuteuliwa na Rais wa Zanzibar ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete kushika wadhifa huo.
Mazungumzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa (V.I.P) uliopo uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Zanzibar mazungumzo ambayo yalihudhuriwa pia na Waziri wa Katiba na Sheria wa Zanzibar Mh. Aboubakar Khamis Bakari, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mh. Fatma Abdulhabib Ferej pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Mh. Said Hassan Said.
Mh. George Masaju alisema yeye kama wakili wa Serikali atakuwa kiungo wa kuunganisha uhusiano unaohitajika kuendelea kuwepo kati ya Serikali mbili ile ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
“ Naahidi kusimamia ushirikiano uliopo kati ya Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania { SMT } na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar {SMZ } nikitumia uzoefu wangu nilioupata katika masuala ya kisheria “. Alisema Mwanasheria Mkuu huyo wa SMT.
Akitoa nasaha zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alimpongeza Mwanasheria Mkuu huyo wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. George kwa kuteuliwa kushika wadhifa huo.
Balozi Seif alisema Rais wa Kikwete hakufanya makosa Kumteua Mh. George kutokana na umakini wake wa kutekeleza jukumu analokuwa akikabidhiwa na umma.
Alimkumbusha Mwanasheria Mkuu huyo wa Serikali ya Muungano wa Tanzania kuendelea kuzingatia maadili yanayosisitiza uwajibikaji uliotukuka ambao hutoa fursa kwa kila mwananchi kupata haki zake kwa mujibu wa sheria.
Balozi Seif alieleza kwamba wadhifa wa uanasheria Mkuu wa Serikali sio kazi nyepesi kwa vile unasimama kwa kazi moja ya kuunganisha pamoja kati ya Serikali na ile mihimili mengine ya Nchi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alielezea matumaini yake kwamba wanasheria wakuu wote wawili wa Zanzibar na Tanzania wataendelea kufanya kazi kwa kusaidiana.
Balozi Seif alimuhakikishia Mwanasheria Mkuu huyo wa SMT kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar muda wote itajitahidi kumpa ushirikiano mzuri ili awe na uwezo madhubuti wa kutekeleza majukumu yake kwa Taifa.
No comments:
Post a Comment