Shirikisho la mpira wa miguu nchini Tanzania (TFF) limesema kuwa halina taarifa kama mchakato uliofanywa na klabu ya Simba wa kumsajili kiungo mshambuliaji wa klabu ya Express ya Uganda Simon Sserunkuma ulighushiwa na kuwa na harufu ya rushwa.
Mkurugenzi wa mashindani wa TFF, Boniface Wambura ameiambia BBC Dar es Salaam kuwa hawajapata taarifa zozote kutoka kwa shirikisho mwenza (FUFA) la Uganda juu ya uhasidi huo.
“Tunachojua sisi TFF ni kuwa mchakato ulikuwa ni halali, ndio maana wenzetu wa Uganda, baada ya mawasiliano yetu, wametutumia cheti cha uhamisho wa mchezaji huyo”, alisema Wambura.
‘Kupewa cheti cha uhamisho na FUFA kuna maanisha mchakato ulikuwa sahihi, kama kuna lingine ni juu ya FUFA sio TFF).
Kauli ya Wambura inakuja siku chache baada mwenyekiti wa timu ya Express Francis Ntalazzi kuripotiwa na vyombo vya habari vya Uganda akisema kuwa sahihi yake iligushiwa ili kumsainisha mchezo huyo.
Ntalazzi alidai kuwa huenda rushwa ilitumika na kuongeza kuwa hiyo itakuwa kazi ya Polisi endapo itathibitika.
Kauli ya Ntalazzi imepingwa na mwenyekiti wa kamati ya usajili ya Simba, Hans Poppe akisema mchakato ulikuwa sawa na kama Ntalazzi hakushirikishwa na viongozi wenzake hilo haliwahusu Simba.
Endapo upepo huo mbaya utapita, Sserunkuma, aliyesajiliwa kwa mkataba wa dola 40,000, ataungana na Daniel ‘Muzei’ Sserunkuma, Joseph Owino(Kutoka Kenya) , Murushid Jjuuko , (kutoka klabu ya chuo cha Victoria-Uganda na Emmanuel Okwi (Uganda).
No comments:
Post a Comment