Takriban wasichana 808 wamewacha shule katika kipindi cha miaka minane katika jimbo la Rukwa nchini Tanzania kutokana na mimba ,mkuu wa elimu katika jimbo hilo Fanuel Mkaruka amesema.
Bwana Mkaruka amefichua hili wakati alipokuwa akizungumza na wadau wa elimu katika mkutano uliolenga kuzungumzia maswala muhimu ya elimu katika jimbo hilo.
Miongoni mwa maswala mengine, wadau walizungumzia changamoto zinazowakumba wanaume katika elimu ya ngono chini ya mradi wa TMEP.
Kulingana na Bwana Mkaruka ,idadi hiyo inashirikisha wasichana walioshika mimba na kuwacha shule katika ya mwaka 2010 na 2014.
Amesema kuwa idadi hiyo inashirikisha wasichana 59 kutoka shule za msingi na 749 kutoka shule za upili.
Ameongezea kuwa wilaya ya Nkasi ambayo ipo katika sehemu ya ziwa Tanganyika inaongoza na wasichana 477 ambao walishika mimba na kuwacha shule.
Aliongezea kwamba miongoni mwa wasichana 477,31 walikuwa wakisoma katika shule za msingi huku 446 wakiwa katika shule za upili.
Kulingana na Mkaruka ,tatizo hilo limekuwa likiongezeka kutokana utamaduni uliopitwa na wakati ambao unawaruhusu wazazi kuwaoza wanao hata iwapo wapo shuleni.
''Ni wazi kwamba tunakabiliwa na changamoto katika eneo hili,wazazi wengi bado wanaamini tamaduni ambazo tayari zimepitwa na wakati.
Wasichana wananyimwa haki zao za kupata elimu kutokana na tamaduni potofu'',alisema.
Aliongezea kuwa ukosefu wa hamasa kuhusu maswala ya elimu miongoni mwa wazazi ni sababu nyengine ya wasichana wengi wa shule kuwacha masomo katika jimbo hilo.
Amesema kwa kuwa wazazi hawawahamasishi watoto wao kuhusu kwenda shule,wasichana wengi huwacha masomo na kuolewa kupitia baraka za wazazi wao.
Afisa wa mradi wa TMEP Bi Valerie Kalyalya amesema kuwa afisi yake itaendelea kutoa elimu kuhusu ngono kwa wavulana na wasichana walio na umri wa zaidi ya miaka kumi.
No comments:
Post a Comment