Na Sijawa Omary, Mtwara
MKOANI mtwara maeneo mbalimbali ikiwemo wilaya, vijiji na vitongoji havijafanya uchaguzi wa serikali za mitaa uliyofanyika nchini kote Desemba 14 mwaka huu.
Akizungumza na jambo leo katibu wa CCM Mkoa Shaibu Akwilombe alisema kuwa, kumekuwa na baadhi ya maeneo mkoani humo kwa kutofanya uchaguzi kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kubwa ya ukosefu wa vifaa hususani Wilaya ya Nanyumbu.
Alisema, kwa mujibu wa kanuni za sheria inabidi uchaguzi ufanyike ndani ya wiki moja na si vinginevyo na maeneo ya vijiji ambayo hayajafanya chaguzi ikiwemo Wilaya ya Nanyumbu vijiji 11 ambapo uchaguzi wake unafanyika kesho, Wilaya ya masasi kijiji 1 na uchaguzi wake unafanyika leo.
Pia Wilaya ya Newala kijiji 1, wilaya ya mtwara vijijini 2 na katika vitongoji ikiwemo wilaya ya Newala vitongoji 4, wilaya ya Nanyumbu vitongoji 7 na wilaya ya mtwara vijijini vitongoji 5.
Kwa mujibu wa matokeo ya uchaguzi wa serikali za mitaa katika manispaa ya mtwara mikindani yaliyotolewa na mkurugenzi wa manispaa hiyo Limbakisye Shimwela alisema, katika mitaa 111 ya manispaa mitaa 100 tu ndiyo imefanyafanya chaguzi na mitaa 11 imepita bila kupingwa kwa ccm kutokana vyama pinzani havikusimamisha wagombea.
Akifanunua zaidi mkurugenzi huyo alisema, katika idadi hiyo ccm imeshinda mitaa 54 sawa na asilimia 48.6%, cuf mitaa 36 sawa na asilimia 32.4%, chadema 16 sawa na asilimia 14.4%, nccr mageuzi 4 sawa na asilimia 3.6% na tlp mtaa 1 sawa na asilimia 1% ambapo kwa asilimia hizo zote inakuwa ni asilimia %.
Hata hivyo Mkurugenzi katika Wilaya ya mkoani humo Tandahimba Abdallah Njovu kwenye matokeo ya wilaya hiyo alisema, Wilaya ina vitongoji 650 kati ya hivyo CCM imepata vitongoji 394, CUF 217, Chadema 25 na TLP 6.
Naye Mkurugenzi wa Wilaya ya Masasi, Beatrice Dominic alisema kuwa, wilaya hiyo ina vitongoji 864 ambapo kati ya hivyo CCM imepata vitongoji 802, CUF 28, Chadema 31 na NLD 1.
Na Baltazar Mashaka, MWANZA
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mwanza, kimesema kiko imara na hakijatikiswa na matokeo ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji uliofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita.
Pia kimekiri kuwepo kwa dosari katika ucaguzi huo na wingi wa viti vilivyonyakuliwa na vya upinzani,umekizindua na kukiimarisha kuliko wakati mwingine wowote ule, katika siasa za mkoa wa Mwanza na kote nchini.
Kauli hiyo imetolewa leo na Katibu Mwenezi wa CCM mkoani hapa, Simon Mangelepa,alipozungumza na waandishi wa habari katika ofisi za chama hicho.
Alisema CCM itaendelea kuongoza kutokana na wananchi kukiamini na kukiunga mkono na kukipatia ushindi katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa,Vijiji na Vitongoji.
“Nawapongeza wananchi kwa kuendelea kuamini CCM na kuipa ushindi. Ahadi yetu ni kuendelea kuisimamia serikali itekeleze ilani ya Uchaguzi ya chama chetu ili kuwaondolea kero wananchi zao,”alisema Mangelepa
Alisema kuwa wananchi wamepata mwamko,hivyo CCM ina kazi kubwa sana kuhakikisha inatimiza na kutekeleza ahadi zake kupitia ilani ya uchaguzi ya chama hicho ili kukidhi matakwa ya wnaanchi.
“Kujitetea ni unapoingia kwenye uchaguzi, sasa wananchi wanaelewa sana.Tuna kazi kubwa kuhakikisha tunajipanga vizuri na kuondoa mapungufu yaliyosababisha tupote mitaa,vijini an vitongoji.Mahitaji ya jamii bado ni makubwa kwa CCM na serikali yake,hivyo tutazatiti kumaliza shida zao,”alisema Mangelepa.
Hata hivyo alisema uchelewashaji wa vifaa katika baadhi ya wilaya za mkoa wa Mwanza ni moja ya dosari zilizosababisha wananchi washindwe kupiga kura kwa wakati na kudai hali hiyo ilitokana na ukosefu wa umakni kwenye usimamizi.
Aidha duru za kisiasa mkoani hapa zinasema kuwa ushindi wa vyama vinavyounda UKAWA,ni anguko la chama hicho kikongwe kuelekea kuelekea uchaguzi Mkuu wa 2015 na inaonesha jinsi gani wanancvhi wamekichoka.
Kwamba dalili za CCM kuanguka zilijionyesha mapema kutoka chama hicho na serikali yake kuandamwa na kashfa mbalimbali,huku wananchi wakikosa huduma muhimu hasa katika sekta ya afya,maji na elimu.
Inaelezwa kuwa viongozi wa serikali ya CCM wameshindwa kukidhi matarajio ya wananchi kwa kuwaondolea kero zao nyingi,badala yake wamejikita kwenye vitendo vya ufisadi na kuisahau jamii ikiendelea kulalamika.
Katika uchaguzi huo CCM iliambulia viti 96 katika wilaya ya Nyamagana Jiji la Mwanza, huku CHADEMA 71, CUF 7 na ACT kiti kimoja kati ya mitaa 175. Katika Manispaa ya Ilemela CCM Iilipata mitaa 106 ,CHADEMA 62na CUF mitaa 3,ambapo mitaa mine uchaguzi wake ulirudiwa jana.
Wilayani Magu CCM ilishinda katika vijiji 53,CHADEMA vijiji 26 na UDP 3 kati ya vijiji 82. Misungwi CCM ilishinda vijiji 97 CHADEMA 16 kati ya vijiji 113.Ukerewe CCM iliambulia vijiji 27,CHADEMA 47 na CUF 2 kati ya vijiji 76. Kwimba CCM 33, CHADEMA 3 na TLP 1.
Katika ngazi ya vitongoji Magu CCM ilipata ushindi katika vitongoji 246 na CHADEMA 111, Ukerewe CCM walipata 311, CHADEMA 184 na CUF 19 kati ya 514, Kwimba CCM 184, CHADEMA 29 na TLP 2 kati ya 215.
Jimbo la Buchosa Sengerema uchaguzi huo ulifanyika jana baada ya kushindwa kufanyika Jumapili kutokana an vifaa kuchelewa kufika kwenye vituo.Hadi tunakwenda mitamboni matokeo yalikuwa bado hayajatangazwa.
Na Magreth Magosso, Kigoma
Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kigoma kimeendelea kuongoza katika wilaya Nne kwa kunyakua jumla ya viti 165 katika nafasi ya uenyekiti na ujumbe katika Halmashauri Nnne kati ya sita zilizopo mkoani humo.
Akizungumza leo, Katibu mwenezi na itikadi mkoani hapa, Kalembe Masudi alisema katika halmashauri ya manispaa ya kigoma mjini chama hicho kimenyakua viti 46 katika mitaa 68na halmashauri ya wilaya ya kigoma imenyakua viti 30 kati ya vijiji 45.
“kwa buhigwe tunaongoza kwa viti 17 na upinzani wana viti saba,ila kutokana na vijiji 10 kufutwa kwa uchaguzi hatujajua hatma ya kura zilizopigwa kwa umma wa buhigwe “ alibainisha Masudi.
Katika wilaya ya Kibondo ccm imepata viti 33 kati ya vijiji 50,ambapo kwa chama cha Chadema kiliambulia viti 3, CUF viti 2, Nccr-mageuzi viti 11 huku ACT ikishika kitongoji kimoja, Chadema 1, CUF 1, DP 1 na UDP ikishika kitongoji kimoja.
Wakati huohuo katika wilaya ya Uvinza ccm ilinyakua viti 39, ACT viti 3, Nccr-mageuzi 3 ambapo Chadema na CUF waliambulia kiti kimoja kimoja.
Katibu Mwenezi Itikadi Taifa kupitia Chama cha NRA mkoani humo Fadhili Kiswaga alisema ni mara ya kwanza chama hicho kushika nafasi mbalimbali katika chaguzi ndogo na kubwa ambapo walianza kujikita kwenye ushindani mwaka 2010 na 2014 wamefanikiwa kunyakua kijiji cha mazungwe na vitongoji 3 hivyo ina jumla ya watendaji husika viti 4 katika Kata ya Kazulamimba .
Naye Katibu wa Jimbo la kigoma kusini Thobias Kichwa alisema katika jimbo la kigoma kusini wamefanikiwa kupata viti 4 ,na Katibu mwenezi wilaya ya kigoma mjini Anzuluni Kibera alisema wilaya ya uvinza wana viti vinne katika vitongoji vinne.
Ambapo Jimbo lakigoma kaskazini wamefanikiwa kunyakua vitongoji 23 na kijiji kimoja cha Kasuku na Halmashauri ya manispaa ya kigoma Ujiji wana viti 9 kati ya mitaa 68 na kudai hawatambui uchaguzi huo kwa kuwa uchaguzi haukuzingatia haki na taratibu za uchaguzi na kutaka uchaguzi urudiwe.
Na Paul Wilium, Kilimanjaro.
HALI si Shwari kwa vyama vinavyounda umoja wa wananchi UKAWA, baada ya ngome yao wanayoitegemea ambapo ndipo wanapotoka viongozi wake wakubwa mkoa wa Kilimanjaro, kuburuzwa na CCM na kusababisha viongozi hao kubaki midomo wazi.
Mkoa wa Kilimanjaro ndipo anapotoka Mwenyekiti wa chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) Fremon Mbowe, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi James Mbatia, pamoja na Mwenyekiti wa TLP Dkt. Agustino Liatonga Mrema, jana walikimbia majimbo yao mchana kweupe na kukimbilia jijini Dar es salaam.
Mkoa huo wenye jumla ya vijiji 515, na Vitongoji 2247, na Mitaa 60, ambapo chama cha CCM kilifanikiwa kuchukua vijiji 336, Chadema 124, NCCR-Mageuzi 27 huku TLP wakiibuka na viti 8 na CUF wakipata o.
Kwa upande wa Vitongoji chama cha CCM kiliibuka mshindi kwa kupata vitongoji 1365, CHADEMA 460, NCCR-Mageuzi 132, TLP 17, huku CUF wakiambulia kiti kimoja na katika Mitaa CCM walipata mitaa 28, huku Chadema wakipata mitaa 27.
Katika hali ya kushangaza na kusikitisha Mwenyekiti wa Chadema, Mbowe akiwa katika jimbo lake la Hai, kwenye ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri, mwenyekiti huyo alichukua uamuzi mzito wa kuondoka na kuelekea moja kwa moja katika Uwanja wa ndege KIA, na kuanza safari ya kuelekea jijini Dar es salaam baada ya kupoteza viti vingi vya vijiji na vitongoji.
Matokeo katika wilaya hiyo ya Hai,(Linaongozwa na upinzani) chama cha CCM kiliibuka kidedea kwa kupata vijiji 34, huku Chadema wakipata viti 25, na katika vitongoji CCM walibuka kwa kupata viti 104, ambapo Chadema wakipata 44 na CUF wakifurukuta kwa kupata kimoja.
Aidha katika Jimbo lililo na Upinzani mkubwa la Vunjo ambapo lipo wilaya ya Moshi- vijijini, ambapo ndipo James Mbatia ameweka kambi yake kupitia chama cha NCCR-Mageuzi, CCM iliibuka kidedea kwa kupata vijiji 76, Chadema 45, NCCR-Mageuzi 27, huku chama cha mbunge wa Jimbo hilo ambaye pia ni Mwenyekiti wa TLP kikipata viti 8.
Katika Jimbo la Moshi-Mjini, linaloongozwa na Ndesamburo CCM ilionyesha makucha yake kwa kujikusanyia mitaa 28, huku Chadema wakijikusanyia mitaa 27.
Upande wa Vitongoji CCM ilijiwekea viti 343 kibindoni wakifuatiwa na Chadema 201, NCCR-Mageuzi 132, huku TLP 17.
Jimbo la Mwanga ambalo ndipo anapotoka Waziri wa Maji, Prof. Jumanne Abdalla Maghembe, CCM iliwabwaga wapinzani kwa kupata viti vingi vya vijiji ambapo ilipata 66, ikifuatiwa na Chadema 27, ambapo katika Vitongoji CCM ilipata viti 263, Chadema 19.
Jimbo la Same, CCM iliibuka kinara kwa kupata vijiji 78, ikifuatiwa na Chadema 17, na katika Vitongoji CCM iliongoza kwa kupata 405, na Chadema 87.
Katika Jimbo la Siha, ambapo ndipo anapotoka Naibu Waziri wa Tawala na Serikali za Mitaa, Agrey Mwandri, CCM iliibuka mshindi kwa kujikusanyia vijiji 52, ikifuatiwa na Chadema 8, ambapo katika Vitongoji CCM ilipata 149, Chadema 21.
Jimbo la Mwisho ni jimbo la Rombo, ambalo linaongozwa na Upinzani(SELASINI- chadema), CCM iliibuka kidedea kwa kushinda vijiji 30, huku Chadema wakipata 22, na katika Vitongoji CCM wanaongoza kwa kupata 101, Chadema 80.
Aidha Vijiji 16, Vitongoji 89, na Mitaa 5, hawajapiga kura kutokana na sababu mbalimbali ambapo wanategemewa kupiga kura kesho, Desemba 18-21, katika maeneo hayo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo vurugu katika vituo vyao.
Katika hali ya kushangaza Vituo mbalimbali vya kupigia kura, karatasi ziliisha mapema na kusababisha Wananchi wengi kupoteza haki yao ya kupiga kura.
Akizungumzia Ushindi huo Katibu wa CCM, mkoani Kilimanjaro Deogratius Ruta alisema kuwa, matokeo hayo ni dalili mbaya kwa wapinzani mkoani Kilimanjaro, japo wameweza kuungana na kuwa kitu kimoja.
Ruta alisema kuwa, uhakika wa kurudisha majimbo yanayotawaliwa na vyama vya upinzani mkoani hapo ni mkubwa, kutokana na wapinzani kutumia nguvu kubwa katika uchaguzi wa Serikali za mitaa lakini wamemwagwa.
“Kwa sasa Ukawa ambao wameanza kwa kasi sana mkoani Kilimamanjaro, tunakwenda kuwazika kabisa, wamewaonga wananchi fedha ili wawapigie kura katika uchaguzi huu, lakini bado wameshindwa kukingoa chama cha mapinduzi hiyo ni dalili mbaya kwao” alisema Ruta.
Aliongezea kuwa, tatizo la karatasi kuisha mapema katika vituo vingi vya kupigia kura, zilikuwa ni hujuma za wapinzani baada ya kuwanunua Watendaji wa vijiji, ili kuhakikisha ccm kinaanguka lakini badala yake upepo umewageukia wao.
Mmoja wa wanachama wa CCM, wilayani Siha, hali yake ni mbaya baada ya kupigwa na Jiwe kichwani na Mwanachama wa Chadema, wakiwa wanashangilia ushindi wa CCM, ambapo amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC, huku jeshi la Polisi likiendelea kumsaka mtuhumiwa baada ya kutoweka kusikojulikana.
No comments:
Post a Comment