Waziri wa Ardhi,nyumba na Maendeleo ya makaazi nchini Tanzania Professa Anne Tibaijuka amesema kuwa hayuko tayari kujiuzulu kutokana na kashfa ya ecsrow inayomkabili.
Kulingana na Gazeti la the Citizen Tanzania ,Tibaijuka ambaye pia ni mbunge wa Muleba kusini ameviambia vyombo vya habari kwamba hana hatia na kuongezea kwamba si haki kumshinikiza kujiuzulu kutokana na kashfa hiyo ya kutolewa kwa takriban billioni 306 kutoka kwa akaunti ya Escrow.
''Ninasulubiwa bila kupewa fursa ya kusikizwa'',alisema kufuatia wito wa yeye kujiuzulu kutokana na maswala ya maadili.
Lakini Profesa Tibaijuka amesema kuwa atajiuzulu tu iwapo itabainika kuwa ana hatia na kuongezea kuwa billioni 1.6 alizopata kutoka kwa James Rugemalira hazikuwa chafu.
Waziri huyo amesema kuwa fedha hizo alipewa kama msaada wa kusaidia shule ya Babro Johnson School baada ya bodi ya wakurugenzi wa hazina ya Joha ambayo huendesha shule hiyo,kuomba msaada huo kutoka kwa bwana Rugemalira, mfanyibiashara wa Tanzania ambaye alikuwa na hisa chache katika kampuni ya Independent Power Tanzania.
Alizungumza siku mbili tu baada ya mwanasheria mkuu Frederick Werema kujiuzulu kutokana na jukumu lake katika kashfa hiyo.
''Sioni sababu ya mimi kujizulu kwa sababu kufikia sasa serikali haijasema kwamba nina hatia.
Nitajiuzulu tu iwapo itabainika kuwa nina hatia'',alizungumza katika hoteli ya Grand Hyatt.
Profesa Tibaijuka amesema kwamba kwa sababu hazina ya Joha haitumii fedha chafu yuko tayari kurudisha fedha hizo kwa bwana Rugemalira iwapo itajulikana kwamba fedha hizo zilitolewa kwa njia mbaya.
Waziri huyo amesema kuwa bwana Rugemalira alikubali kutoa ufadhili kwa masharti kwamba atafungua akaunti katika banki ya Mkombozi.
Ameongezea kuwa hakupewa fursa ya kujitetea wakati jina lake lililotajwa bungeni.
No comments:
Post a Comment