Ofisa Uhusiano wa Mamlaka ya Chakula na Dawa
(TFDA) Bi. Gaudensia Simwanza
akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhuhu
mafanikio yaliyofikiwa na Mamlaka hiyo ikiwemo kuimarisha ukaguzi wa bidhaa
zinazoingia na kutoka nchini. Kushoto
ni Afisa Uelimishaji wa Mamlaka hiyo Bw. James Ndege.
Na Frank Mvungi- Maelezo
Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) yaendelea kupata
mafanikio katika Kutekeleza Mpango mkakati wa miaka mitano (5) unaolenga kutekeleza jukumu la kulinda
afya ya jamii kwa kudhibiti ubora na usalama wa vyakula,dawa,vipodozi na vifaa tiba.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es salaam na Afisa
Uhusiano wa Mamlaka hiyo Bi Gaudensia Simwanza wakati akiwaeleza waandishi wa
habari kuhusu utekelezaji wa Mpango Mkakati huo.
Katika kutekeleza Mkakati huo kwa mwaka 2013.14 TFDA
ilifanya Ukaguzi wa majengo na bidhaa katika maeneo 5,785 ambapo idadi hiyo ni
Zaidi ya majengo 1,869 (48%) ikilinganishwa na majengo 3,916 yaliyokaguliwa
katika kipindi cha mwaka 2012/13 na jumla ya maeneo 4,000 sawa na 69% yalikidhi
vigezo alisema Simwanza.
Akizungumzia uchunguzi wa maabara Simwanza amesema
Mamlaka yake ilipokea Sampuli 2,389 kwa ajili ya uchunguzi wa kimaabara na kufanya
kuwa na jumla ya sampuli 2,686 zikiwa ni pamoja na baki ya sampuli 305 za mwaka
jana ambapo kati ya hizo sampuli 2,456 (91%) zilichunguzwa ambapo sampuli 2,379
sawa na 97% zilifaulu.
Sampuli zilizochunguzwa kwa mwaka huo ni pungufu ya
sampuli 235 (9%) ikilinganishwa na zilizochunguzwa mwaka uliopita wa 2012/13,
hii inaonyesha kwamba bidhaa nyingi zilizopo sokoni zinakidhi vigezo vya ubora
na usalama.
Aidha katika kudhibiti usalama na ubora wa bidhaa
zinazoingia na kutoka nchini TFDA iliidhinisha jumla ya maombi 11,887 ya
Chakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba ambapo maombi 10,082 ya kuingiza bidhaa
ndani ya nchi na 312 ya kutoa bidhaa nchini sawa na 87%.
Pamoja na mafanikio yaliyofikiwa Simwanza alisema
kuwa TFDA inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo
kasi kubwa ya kukua kwa teknolojia na soko huria ambavyo vinachochea
utengenezaji wa bidhaa bandia hivyo ni jukumu la kila mwananchi kuhakikisha
ananunua bidhaa zenye ubora na kutoa taarifa anapobaini bidhaa zisizo na
viwango.
No comments:
Post a Comment