Mchezaji soka, Ibrahima Traore ameiomba klabu yake ya Ujerumani Borussia Monchengladbach kumruhusu kuichezea timu yake ya taifa ya Guinea katika fainali ya kufuzu kwa michuano ya kombe la mataifa ya Afrika 2015.
Madaktari wa klabu hiyo wameelezea wasiwasi kuwa huenda akaambukizwa Ebola ikiwa ataenda kuichezea klabu yake nchini Guinea.
Timu ya taifa ya Guinea ,Syli Nationale itacheza katika mechi ambayo lazima washinde dhidi ya Uganda nchini Morocco ambako mechi hiyo ilihamishiwa kwa sababu ya mlipuko wa Ebola nchini Guinea.
''Niliwaambia kwamba ni lazima nichezee timu yangu ya taifa,'' alisema Traore.
''Kombe la mataifa ya Afrika ni mchuano muhimu kwa wachezaji wa Afrika kwa hivyo siwezi kukosa fursa ya kushiriki michuano hio,ni muhimu sana kwangu. ''
''Niliporejea katika klabu yangu nilipimwa na kila kitu kilikuwa shwari, na niliongea na kocha na akasema hapatakuwa na tatizo lolote. Alielewa kama kocha kwamba ni muhimu nisafiri kwenda kuchezea timu yangu, kwa hivyo sina shaka. Sidhani kama kutakuwa na kikwazo, '' aliongeza kusema Traore.
Ikiwa Guinea wataicharaza Uganda mjini Casablanca Jumatano, watafuzu kwa fainali ya kombe la mataifa ya Afrika itakayochezwa nchini Equatorial Guinea.
Traore anasema kwao kufuzu itakuwa hatua nzuri sana kwa timu hiyo ikizingatiwa matatizo yanayoikabili Guinea wakati huu.
"matatizo yote ambayo tumekuwa nayo, yatatupa nguvu ya kuweza kufanya vyema na ikiwa tutafuzu basi litakuwa jambo jema sana, '' alisema Traore.
No comments:
Post a Comment