TAMKO LA SERIKALI KUHUSU TETESI ZA KUWEPO MGONJWA ANAYEHISIWA KUWA NA UGONJWA WA EBOLA MKOANI KILIMANJARO
Kaimu Katibu Mkuu, Dkt. Donan Mmbando
Utangulizi
Mnamo tarehe 22 Oktoba 2014, Wizara ilipokea taarifa
kutoka Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro ya kuwepo kwa mgonjwa
aliyehisiwa kuwa na dalili za ugonjwa wa Ebola. Mgonjwa huyu mwanaume ana umri
wa miaka 37, na mkazi wa Dar es salaam (Kimara ) ambaye alikwenda Kilimanjaro tarehe 20 Oktoba 2014
katika kijiji cha Kirua kwa ajili ya kusalimia ndugu. Mgonjwa huyu alikuwa na
dalili za homa kali ( 38.2 0c), maumivu ya Misuli, kuchoka na
maumivu ya kichwa pamoja na maumivu ya koo na kupoteza hamu ya kula.
Mgonjwa huyu anatibiwa katika Kituo cha Afya Shirimatunda,
Kilimanjaro kuanzia tarehe 22.10.2014 ambako yupo hapo hadi sasa. Mgonjwa huyu
kikazi ni “Land Surveyor” na hufanya kazi zake nchini na nje ya nchi ikiwemo
nchi ya Senegali. Mnamo siku za karibuni alikwenda nchini Senegali kwa kazi za
mkataba na kurejea nchini mwanzoni wa Oktoba 2014. Hata hivyo, mgonjwa huyu hakuwa na historia ya kusafiri kwenda nchi
zilizoathirika na ugonjwa wa Ebola yaani Liberia, Guinea au Sierra Leone.
Hatua zinazochukuliwa hadi sasa;
i.
Sampuli
ya damu ya mgonjwa kwa ajili ya uchunguzi wa Kimaabara ilifanyiwa uchunguzi na kuonekana kuwa na malaria. Matokeo ya
awali dhidi ya magonjwa ya jamii ya ebola yakiwa ni pamoja na Dengue na
Chikungunya yanaonyesha kuwa mgonjwa hakuwa na magonjwa haya.
ii.
Mgonjwa
anaendelea kuhudumiwa katika kituo cha Afya cha Shirimatunda.
iii.
Wanafamilia
wa karibu pia wamechunguzwa na kuonekana kuwa hawana dalili za ugonjwa wa
Ebola.
Mwongozo wa utambuzi wa ugonjwa huu (Standard Case Definition) unaeleza kwamba ili mgonjwa aweze kuhisiwa
kuwa na ugonjwa wa Ebola anatakiwa akidhi vigezo vifuatavyo:
i.
Dalili
za awali ni homa kali ya ghafla, kulegea
mwili, maumivu ya misuli, kuumwa na
kichwa, na kutokwa na vidonda kooni. Mara nyingi dalili hizi hufuatiwa na
kutapika, kuharisha,kutokwa na vipele
vya ngozi, kwa baadhi ya wagonjwa hutokwa na damu ndani na nje ya mwili
ii.
Awe
amesafiri kwenda sehemu zilizothibitishwa kuwa na ugonjwa wa ebola ndani ya
kipindi cha wiki 3 na hizi zikiwemo Guinea, Sierra Leone na Liberia. Aidha
Shirika la Afya Duniani (WHO) limeshatangaza kutokuwepo kwa ugonjwa huu nchini
Senegali na Nigreia na hivyo kuzitoa nchi hizi kwenye nchi hatarishi.
iii.
Dalili
nyingine ni Kugusa majimaji kutoka kwa mgonjwa, maiti au mnyama anayehisiwa au kuthibitishwa kuwa na
ugonjwa wa Ebola.
Hitimisho
Wizara
inapenda kuwatoa hofu wananchi kuwa hadi sasa HAKUNA MGONJWA yeyote
aliyethibitishwa kuwa na virusi vya ugonjwa wa Ebola hapa nchini. Mgonjwa huyu kutoka Kilimanjaro hana ugonjwa
wa Ebola bali anatibiwa kama mgonjwa wa MALARIA.
Adiha Wananchi wanashauriwa kutokuwa na hofu ila
wanatakiwa kuendelea kuchukua tahadhari za kuepuka kupata maambukizi ya ugonjwa
huu ambazo:-
o Kuepuka kugusa au kuingiwa na mate, damu, mkojo, jasho,
kinyesi, machozi na majimaji mengine
yanayotoka mwilini mwa mtu mwenye dalili
za ugonjwa wa Ebola kupitia sehemu zenye
michubuko au vidonda.
o Kuepuka kushughulikia maiti ya mtu aliyekufa akiwa na
dalili za ugonjwa wa Ebola; badala yake watoe taarifa kwa uongozi wa kituo cha
huduma za Afya kwa ushauri. Wataalam watasimamia maziko ikiwa itatokea.
o Wananchi waepuke mila na desturi zinazoweza kuchelewesha kupata huduma muhimu
na kusababisha kuzidi kueneza kwa ugonjwa wa Ebola.
o Kutoa taarifa mapema kwa viongozi wa Serikali na watoa
huduma za Afya katika ngazi zote pale anapotokea mtu mwenye dalili za ugonjwa wa Ebola.
o Kuwahi katika vituo vya kutolea huduma za Afya pale mtu anapohisiwa kuwa na dalili
za ugonjwa huu
Imetolewa na,
Dkt. Donan Mmbando
KAIMU KATIBU MKUU
24 Oktoba, 2014
No comments:
Post a Comment