Mwimbaji wa muziki wa taarabu, Bi. Isha Ramadhan maarufu kama Mashauzi akiongea na waandishi wa habari kuhusu Siku ya Msanii Tanzania itakayofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City siku ya tarehe 25 Oktoba, 2014 jijini Dar es Salaam.
Na Beatrice Lyimo- Maelezo
20/10/2014.
KAMATI ya Siku ya Msanii Tanzania (SYM) imetangaza rasmi
majina ya wasanii watakaotumbuiza katika maadhimisho ya siku hiyo
itakayofanyika Oktoba 25 mwaka huu katika ukumbi wa Mlimani City uliopo jijini
Dar es Salaam.
Akizingumza na waandishi wa habari leo jijini Dar Es Salaam, Ofisa
Uhusiano wa SYM, Bw. Peter Mwendapole amesema
kuwa, kutokana na siku hiyo kuwa ni ya Sanaa zote, Kamati imeangalia uwakilishi
wa sanaa za aina mbalimbali ili ziweze kuwakilisha siku hiyo katika historia ya
Tanzania.
“Leo tungependa kuwatangaza Wasanii watatu wa Bendi ya
Kilimanjaro Wana Njenje wenye vionjo vya Tanzania na Wawakilishi wa kundi la Wanamuziki
wakongwe”, alisema Mwendapole.
Mwendapole alisema kuwa, kwa upande wa sanaa kuatkuwa na msanii
maarufu kama Isha Mashauzi ambaye atawakilisha fani ya muziki wa jukwaani na upande
wa Taarabu, kwani msanii huyo ameweza kufanya mapinduzi makubwa kwenye muziki
wa taarabu pamoja na kuweka vionjo mbalimbali vya dansi, asili na taarabu.
Aliongeza kuwa, kutakuwa na kikundi cha sanaa kijulikanacho
kama Ako Mpiruka Sound, bendi ya muziki, kikundi cha ngoma, kikundi cha
sarakasi, wacheza Yoga na pia kutakuwa na shoo ya muziki wa dansi pamoja na
dansi za mitaani.
Amebainisha kuwa, vijana wanaocheza muziki mitaani
wakiwezeshwa wanaweza kujiajiri na kupunguza idadi kubwa ya watu ambao hawana
ajira.
“Siku ya msanii tunataka kuonyesha jinsi gani wanenguaji wana
uwezo wa kucheza bila ya kuonyesha maungo yao”, alisisitiza Mwendapole.
Akifafanua kuhusu kiingilio cha siku hiyo ya msanii alisema
kuwa, kiingilio hicho kitakuwa ni shilingi 70,000 kwa VIP na 50,000 kwa viti
vya kawaida.
Siku ya msanii inaandaliwa na kampuni Haak Neel Production
(T) Ltd kwa kushirikiana na Baraza la Sanaaa la Taifa (BASATA) na kudhaminiwa
na New Habari (2006) LTD kupitia magazeti ya Bingwa, Dimba, The African, na
Mtanzania.
Wadhamini wengine wa SYM pamoja na PSPF, Azam Media, EFM,
Magic FM, Clouds FM, Channel Ten, CXC, Ledger Plaza Hotel pamoja na Proin
Tanzania.
No comments:
Post a Comment