TANGAZO


Thursday, October 16, 2014

Mfuko wa Pensheni wa LAPF wafikisha Sh. Bil. 830

Meneja wa Takwimu, Tathmini na Hadhari toka Mfuko wa Pensheni wa LAPF, Bw. Aboubakar Ndwata akiwaeleza waandishi wa habari leo, Jijini Dar es Salaam kuhusu utekelezaji wa miradi mbalimbali unaofanywa na mfuko huo ukiwemo wa jengo linalokadiriwa kuwa refu zaidi jijini Dar es Salaam lenye urefu wa gorofa 30 ambalo limejengwa kijitonyama jijini Dar es salaam likiwa na thamani ya Shilingi bilioni 58, kulia ni Meneja Masoko na Mawasiliano wa Mfuko huo Bw.James Mlowe na kushoto ni meneja Matekelezo Bw. Victor  Kikoti.
Baadhi ya waandishi wa habari wakiwa ndani ya moja ya ukumbi wa kisasa hapa nchini Tanzania wenye viwango vya Kimataifa uliopo ndani ya Jengo la Gorofa thelani lililojengwa na mfuko wa pensheni wa LAPF Katika eneo la Kijitonyama jijini Dar es  salaam, wakati walipotembelea mradi huo kujionea hatua iliyofikiwa.
Sehemu ya Ukumbi wa Kisasa uliopo katika jengo la LAPF  Kijitonyama (maarufu kama millennium tower phase II)
Baadhi ya waandishi wa habari wakimsikiliza Meneja wa Takwimu, Tathmini na Hadhari toka Mfuko wa Pensheni wa LAPF, Bw. Aboubakar Ndatwa (hayupo pichani) akifafanua kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo ushiriki wa mfuko katika ujenzi wa majengo marefu ambayo ni moja ya vitega uchumi vya mfuko huo.

Frank Mvungi-Maelezo
Mfuko wa Pensheni wa LAPF umekua na kuongezeka ambapo thamani yake  imefikia Sh. bilioni 830 hivyo kuwa ni mfuko unaokua kwa kasi zaidi hapa nchini.
Hayo yamesemwa jana jijini  Dar es salaam na Meneja wa Takwimu,Tathmini na Hadahari toka LAPF bw. Aboubakar Ndwata wakati wa Ziara ya waandishi wa habari katika moja ya miradi inayotekelezwa na mfuko huo katika eneo la kijitonyama Jijini Dar es salaam.
 Akifafanua kuhusu mafanikio ya Mfuko huo Ndwata amesema moja ya miradi inayotekelezwa ni ujenzi wa jengo la kisasa katika jiji la Mwanza  wenye thamani ya bilioni 60 ambao utaongeza na kukuza shughuli za kiuchumi katika jiji hilo.
“Mradi wa eneo la mabasi wa msamvu Mkoani Morogoro ambao unakadiriwa kutumia Sh. bilioni 35 ambapo michoro imeshakamilika na shughuli za kutangaza zabuni zinaendelea” alisema Ndwata.
Katika mradi wa ujenzi wa Mabweni Katika chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo Ndwata amesema awamu ya kwanza ya mradi huo iliyogharimu bilioni 39 imekamilika na awamu ya pili michoro yake imekamilika na inakadiriwa kutumia Sh. bilioni 15.
Pia LAPF imetekeleza mradi wa ujenzi wa Shule ya Afya katika chuo Kikuu Dodoma ambapo mradi huo ulikamilika Agosti 2010 ukiwa na thamani ya Sh. bilioni 22.
Mfuko huo pia unajenga Jengo la Kisasa kwa ajili ya ofisi ya Dodoma lenye thamani ya Sh. Bilioni 47 ambapo mradi huo ulianza mwaka 2012 na unatarajiwa kukamilika mwaka huu.
Katika hatua nyingine Ndwata alisema Makao makuu ya Mfuko huo yako Dodoma na ofisi za Kanda ya kati zinajumuisha Mikoa ya Dodoma, Singida,Tabora, Kigoma na Kanda ya Mashariki inayojumuisha Mikoa ya Dar es salaam, Mtwara, Lindi, Morogoro na Pwani.
Kwa Upande wa Kanda ya Kaskazini Ndatwa alisema kuwa inajumuisha Mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjarao,Tanga na Kanda ya  Ziwa  Mwanza, Kagera, Mara, Geita, na Shinyanga.
Naye Meneja Masoko na Mawasiliano wa Mfuko huo Bw. James Mlowe  alisema mfuko huo umekuwa  ukitoa fao la elimu kwa njia ya mkopo kwa wanachama wake ambao umeanza rasmi agosti mwaka 2014.
Aidha, Mlowe ameongeza kuwa LAPF inaendelea kutoa mafao bora kwa wanachama wake tangu kuanzishwa kwake hadi sasa.
Mfuko wa pensheni wa LAPF  unaendeshwa chini ya Sheria ya LAPF ( The Local Authorities Pensions Fund Act No 9 of 2006) ambapo sheria hii imefanyiwa marekebisho kukidhi mahitaji ya sheria ya usimamizi wa Hifadhi ya Jamii ya Mwaka 2008 (SSRA).

No comments:

Post a Comment