Na Beatrice Lyimo,
Maelezo-DSM.
20/10/2014.
WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Mhe. Dkt. Shukuru Kawambwa
anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Harambee ya kuchangia kuchangia ujenzi wa
nyumba za walimu vyumba vya madarasa na ununuzi wa samani katika shule ya Sekondari
ya Enaboishu iliyopo mkoani Arusha.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Bodi wa shule hiyo, Bw.
Emmanuel Munga wakati alipokuwa akizungumza na waandishi leo jijini Dar Es
Salaam.
Munga amesema kuwa Harambee hiyo inatarajiwa kufanyika siku
ya tarehe 25 Oktoba mwaka huu katika shule hiyo wilayani Aremure mkoani Arusha
ambapo Kauli mbiu ya harambee hiyo ni ‘penye nia pana njia’.
Alisema kuwa, katika harambee hiyo wamewashirikisha wanafunzi
wote waliosoma katika shule hiyo wakiwemo wazazi, viongozi mbali mbali wa Serikali,
Vyama vya siasa, Mashirika yasiyo ya kiserikali, wadau, shule za jirani na
wananchi kwa ujumla.
“katika harambee hii tunatarajia kukusanya zaidi ya shilingi milioni
200 na fedha zitakazopatikana zitatumika kutatua changamoto zinazozikabili
shule”, alisisitiza Munga.
Akizungumzia kuhusu changamoto zinazoikabili shule hiyo alisema
kuwa, shule hiyo yenye mchanganyiko wa wanafunzi wa kike na wakiume iliyoanza
mwaka 1966 inakabiliwa na changamoto za nyumba za walimu, nyumba za madarasa, mabweni
ya wanafunzi na maabara.
Ameongeza kuwa shule hiyo imetoa baadhi ya viongozi wakubwa
waliopo serikalini wakiwemo Naibu Waziri wa Tamisemi Mhe. Agrey Mwanri na Naibu Katibu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni
na Michezo Profesa Elisante Ole Gabriel.
No comments:
Post a Comment