TANGAZO


Friday, October 17, 2014

Ajali tamasha la Korea Kusini

Watu wapatao 16 wamekufa na wengine 11 kujeruhiwa katika tamasha la muziki mjini Seongnam, kusini mwa mji wa Seoul nchini Korea Kusini, maafisa wamesema.
Wamesema eneo la jukwaa la kutolea hewa liliporomoka na mashabiki katika tamasha walianguka umbali wa mita 10 hadi eneo la chini la maegesho ya magari.
Umati wa watu wamekuwa wakiangalia onyesho hilo la nje lililofanywa na bendi ya mwanamuziki maarufu wa Korea iitwayo 4Minute na bendi nyinginezo.
Waathirika walipanda juu ya jukwaa ili waweze kuona vizuri onyesho hilo.
Wafanyakazi wa uokoaji wametahadharisha kuwa idadi ya watu waliokufa huenda wakaongezeka.
"Watu kumi na wawili walikufa katika eneo la tukio, wawili wengine walipoteza maisha walipokuwa wakikimbizwa kwenda hospitali. Wengine wanadhaniwa wamekufa wakati wakipatiwa matibabu," afisa wa idara ya zima moto katika eneo hilo alinukuliwa akisema hayo na shirika la habari la Korea Kusini Yonhap.
Watu wapatao 700 walikuwa katika tamasha hilo, ikiwa ni sehemu ya tamasha la eneo hilo ambalo hufanyika Pangyo Techno Valley, eneo la kampuni mbalimbali za teknolojia.
Katika umati mkubwa, watu kati ya 20 hadi 30 walipanda jukwaani kupitia upenyo wa kutolea hewa. Kutokana na uzito wao walisababisha jukwaa kuporomoka na kuanguka chini.
"kulikuwa na mayowe ya kushtua na nilipogeuka ilionekana kana kwamba watu walikuwa wakivutwa chini ya shimo," mmoja wa watu walioshuhudia tukio hilo amekiambia kituo cha habari cha YTN.
Mwandishi wa BBC mjini Seoul, Steve Evans amesema shughuli ya haraka ilikuwa kuokoa maisha ya watu waliojeruhiwa lakini ajali hiyo huenda ikasababisha mjadala kuhusu viwango vya usalama nchini Korea Kusini.
Baada ya kivuko cha Sewol kilizama miezi sita iliyopita, kwa watu zaidi ya 300 kupoteza maisha, wengi wakishutumu kuwa viwango vya usalama haviendani na kasi ya maendeleo ya kiuchumi ya Korea Kusini.

No comments:

Post a Comment