Mkurugenzi
wa Takwimu
za Uchumi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Bw. Morrice Oyuke (katikati)
akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ukuaji
wa Pato la Taifa kwa bei ya Soko leo jijini Dar es salaam. Wengine ni
Bw. Oswald Ruboha (kulia) Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Sera na
Mipango, Wizara ya Kilimo na Dkt. Stephen Kirama (kushoto), Mhadhiri wa
Uchumi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Na Aron Msigwa – MAELEZO
11/9/2014. Dar es Salaam.
SEKTA ya
Kilimo, Uvuvi, Viwanda, Nishati na
Madini zimeelezwa kuwa miongoni mwa sekta muhimu zinazoongoza zaidi katika
kuchangia kukua kwa pato la Taifa hadi asilimia 7.4 katika robo ya kwanza ya
mwaka 2014.
Kwa mujibu wa taarifa
zilizokusanywa kutoka katika vyanzo mbalimbali vya uzalishaji nchini na Ofisi
ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kutumia kanuni za kimataifa kukokotoa pato la
Taifa zinaonyesha kuwa sekta hizo zimetoa mchango mkubwa wa kukua kwa pato la
Taifa kwa asilimia 7.4 kuanzia mwezi
Januari hadi Machi, 2014 ikilinganishwa
na asilimia 7.1 za mwaka 2013.
Mkurugenzi wa Takwimu
za Uchumi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Bw. Morrice Oyuke akizungumzia ukuaji
wa Pato la Taifa kwa bei ya Soko leo jijini Dar es salaam amesema kuwa Pato la
Taifa katika robo ya mwaka 2014 kuanzia Januari hadi Machi limekua kwa asilimia
7.4 kutokana na kukua kwa sekta za Kilimo, Uvuvi, Viwanda, Ujenzi, Umeme
na utoaji wa huduma.
Amesema sekta
zilizofanya vizuri katika ukuaji huo ni pamoja na sekta ya uchimbaji wa Madini,
mawe na kokoto ambayo imekua kwa asilimia 8.7 ikilinganishwa na asilimia 1.7 za
mwaka uliopita kutokana na kukua kwa masoko ya uuzaji ya nje ya nchi.
Ameongeza kuwa sekta
uzalishaji wa bidhaa za viwandani imekua kwa asilimia 8.5 kutoka 8.3 huku
shughuli za utoaji wa huduma na uchumi zikiwemo za ukarabati wa magari,
pikipiki na vifaa vingine vya majumbani zikikua kwa asilimia 8.0 kwa robo ya
mwaka 2014.
Bw. Oyuke ameeleza kuwa
shughuli za uchukuzi na mawasiliano zimefikia kasi ya ukuaji wa asilimia 16.5
katika kipindi hicho na kuongeza kuwa huduma za hoteli na migahawa zimefikia
kasi ya ukuaji wa asilimia 3.0, huku shughuli za uendeshaji wa Serikali
zikifikia asilimia 5.1, Elimu asilimia 5.2, huduma za Sfya na shughuli nyingine zikikua kwa asilimia 4.5.
Aidha, amefafanua kuwa
sekta ya umeme katika robo ya mwaka 2014 imekua kwa asilimia 12.6
ikilinganishwa na asilimia 6 ya mwaka uliopita kutokana na kupatikana kwa
vyanzo mbadala vya kuzalisha umeme hususan ugunduzi wa gesi nchini ambao
umeondoa tatizo la utegemezi wa umeme wa maji katika kuzalisha umeme.
“Kwa kipindi kirefu
sekta ya umeme imekuwa na mawimbi kwa kiasi kikubwa , umeme wetu umekuwa wa
kutegemea maji ya mvua, baada ya juhudi za Serikali na kugundulika kwa nishati
ya Gesi nchini na kupatikana chanzo mbadala cha nishati tatizo hili
limeshghulikiwa sasa sekta hii imeimarika” Amesisitiza.
Amesema Tanzania sasa
inafanya vizuri kiuchumi katika nchi za Afrika ya Mashariki kwa kuwa ya pili
ikifuatiwa na Uganda, Rwanda na Burundi na kuongeza kuwa hali ya amani na
utulivu iliyopo nchini inaiweka Tanzania katika nafasi nzuri ya kukua zaidi
kiuchumi.
Kwa upande wake mtaalam
wa wa Uchumi kutoka Benki Kuu ya Taifa (BOT) Bw. Davidi Kwimbere akifafanua
kuhusu hali iliyopo ya ukuaji wa uchumi amesema kuwa imechangiwa na kuongezeka
kwa shughuli za uzalishaji .
Amesema sekta ya Kilimo
na uzalishaji wa mazao imekua kutokana na matumizi ya mbolea, zana bora za
kilimo, mbegu bora, madawa na kufafanua kuwa endapo juhudi zaidi zitaendelea
kufanywa na wananchi kwa kuingia katika shughuli mbalimbali za uzalishaji
uchumi utaendendelea kuonekana kwa mtu mmoja mmoja.
Amefafanua kuwa maendeleo
katika nchi yoyote yanachukua muda na
kutoa wito kwa nchi za Afrika kuendelea kujifunza na kufafanua kuwa nchi zote zilizopiga hatua
kimaendeleo mpaka kufikia asilimia 15 ikiwemo China iliwachukua miaka 20
kuondoa umasikini.
Amesema Tanzania inayo
nafasi nzuri kukua kiuchumi kutokana na kuendelea kuimarika kwa
miundombinu na ukuaji wa sekta za ujenzi,
Nishati, madini, Viwanda, umeme , kilimo na uvuvi hali inayochangia kuongezeka
kwa uwekezaji.
No comments:
Post a Comment