TANGAZO


Wednesday, September 17, 2014

PSPF yaeendelea kuboresha maisha ya wanachama wastaafu


Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Bw. Assah Mwambene akitoa pongezi kwa Mfuko wa Pensheni wa PSPF kwa mafanikio waliopata tangu kuanzishwa kwa mfuko huo, kwenye mkutano na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Pensheni wa PSPF Bw. Adam Mayingu akiwaeleza waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu mafanikio ya mfuko huo kwa kipindi cha miaka 15 tangu ulipoanzishwa. Kushoto ni Afisa Uhusiano Mwandamizi wa PSPF Bw. Abdul Njaidi.

Baadhi ya watumishi wa PSPF na waandishi wa habari wakifuatilia mkutano wa mfuko huo uliofanyika leo jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Pensheni wa PSPF Bw. Adam Mayingu akijibu maswali ya waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu tofauti za malipo ya pensheni kwa wastaafu  ambapo alisema kuwa tofauti hizo zinatokana na kiwango cha mshahara na muda wa utumishi wa mwanachama. Kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Bw. Assah Mwambene.


Wakurugenzi wakionesha kwa waandishi wa habari (hawapo pichani), tuzo mbalimbali zilizotolewa kwa Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF) kutokana na mafanikio yake. Kutoka kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa mfuko huo, Bw. Adam Mayingu, Mkurugenzi wa Fedha na Utawala, Bw. Masha Mshomba, Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Bw. Assah Mwambene na Mkurugenzi wa Uendeshaji wa PSPF, Bi. Neema Muro. (Picha zote na Georgina Misama-MAELEZO)




Na Fatma Salum- MAELEZO
MFUKO wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF), umeendelea kuboresha maisha ya wanachama wastaafu kwa kuwawezesha kupata mkopo kupitia Benki ya Posta Tanzania.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa mfuko huo Bw. Adam Mayingu wakati akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuhusu mafanikio ya mfuko kwa miaka 15 tangu ulipoanzishwa.
Mayingu alifafanua kuwa mpaka sasa zaidi ya shilingi bilioni 13 zimetumika kuwakopesha wastaafu wa PSPF wapatao 4,097 kwa lengo la kuwasaidia kwenye shughuli zao mbalimbali za maendeleo.
“PSPF ni mfuko wa kwanza nchini kuingia mkataba na Benki ya Posta ambapo wanachama wastaafu wa mfuko wanaweza kupata mkopo  na  mpango huu ulizinduliwa rasmi Juni 2014.”

Akieleza zaidi mafanikio ya mfuko huo Mayingu alisema kuwa takwimu za Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) zinaonyesha Mfuko wa PSPF una idadi kubwa ya wastaafu na wategemezi kuliko mifuko mingine ambapo kwa miaka kumi sasa unahudumia wastaafu na wategemezi wapatao 53,000 na kiasi cha trilioni 2.83 zimelipwa kwa wanachama wake.
Aidha Mayingu aliongeza kuwa PSPF wameweza kupata tuzo za kitaifa na kimataifa kutoka kwa wadau mbalimbali wa hifadhi ya jamii ambao wametambua mchango wa mfuko huo katika kuboresha maisha ya wanachama wake na kuchangia maendeleo ya nchi.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Bw. Assah Mwambene ameupongeza Mfuko wa PSPF kwa kutoa mafao bora na kwa wakati na kuwataka waendelee kuboresha huduma zao ili wanachama waweze kunufaika zaidi.
Akitoa rai kwa waandishi wa habari Mwambene amesema wanapaswa kuhakikisha wanaandika habari zitakazowasaidia watanzania kuelewa mambo mbalimbali hasa katika kipindi hiki cha  mchakato wa katiba mpya badala ya kukazania habari zisizokuwa na tija kwa jamii.

No comments:

Post a Comment