Information Technology (ICT)
Moja ya vituo vinavyotumiwa kwa ajili ya kufundishia masomo ya TEHAMA
Na Benedict Liwenga, MAELEZO-DSM.
16/09/2014
TEHAMA ni moja kati ya Sekta zinazokua kwa kasi hapa
nchini na duniani kote na imekuwa ikichangia kikamilifu katika maendeleo ya
Taifa na pia imekuwa ikiwezesha sekta nyingine kukua na kuboresha maisha ya
wananchi na huduma za jamii kwa ujumla.
Kutokana na ukuaji wa Sekta hii, jitihada za makusudi
zinahitajika katika kusimamia na kuratibu shughuli za TEHAMA ili nchi iweze
kunufaika zaidi kwani mchango wa sekta hiyo unaweza kuwa mkubwa kama TEHAMA na
matumizi yake yataratibiwa, kusimamiwa na kuendelezwa vyema zaidi kuliko hali
ilivyo sasa.
Katika kuhakikisha masuala ya TEHAMA nchini
yanaratibiwa, kusimamiwa na kuendelezwa vyema, Serikali iliona ni vema ikaundwa
Tume ya TEHAMA (ICT Commission).
Tarakilishi
“Computer” katika lugha ya Kiswahili ni kifaa ambacho kimebadilisha mfumo wa maisha
ya binadamu katika miongo takribani sita iliyopita.
Kutokana na kuwepo kwa kifaa hiko
dunia imejikuta katika maendeleo makubwa kabisa kuliko kipindi chochote kile
katika historia ya kuwapo kwake.
Bila shaka kila mwanadamu katika
dunia hii anafahamu ukuaji mkubwa na uwezo wa mawasiliano ambao umeleta
mapinduzi makubwa katika ukuaji wa chumi za nchi na mwingiliano wa jamii moja
kutoka jamii nyingine.
Ni maendeleo haya ya kiteknolojia
ambayo yamesababisha utandawazi ambao hakika umeifanya dunia kuonekana kama
kijiji kidogo kilicho na jamii nyingi zenye taratibu, maendeleo, mila na
desturi na siasa tofauti.
Kwa kimombo Teknolojia ya Habari
na Mawasiliano inafahamika kama Information
Technology au IT kwa kifupi na Kwa
Kiswahili teknolojia hiyo inafahamika kama TEKNOHAMA.
TEHAMA duniani imeanza kupiga
hatua ya kasi sana toka mwishoni mwa Karne ya ishirini na imeleta mabadiliko
makubwa katika nyanja za mawasiliano, uchumi, tafiti na ukusanyaji wa takwimu
mbalimbali.
Pamoja na uwepo wa sheria ya 1974
iliyokuwa ikipinga uagizwaji wa vifaa vya tarakilishi zenyewe na seti za
runinga, mfumo wa mabadiliko mbalimbali ndio uliopelekea Tanzania kupiga hatua
ya kutosha katika kuboresha mfumo wa habari.
Sera ya Taifa ya TEHAMA ya mwaka 2003 inaelekeza
kuundwa kwa chombo cha TEHAMA ikiwemo juhudi na programu mbalimbali
zinazoendelea hapa nchini zinazohitaji utaratibu wenye ufanisi.
Jitihada za kuanzisha Tume zililenga kutekeleza Sera
ya Taifa ya TEHAMA pamoja na maazimio mbalimbali ya kitaifa na kimataifa
ikiwemo maagizo ya Mkutano wa Dunia wa Jamii Habari (World Summit on Information Society).
Aidha, jitihada mbalimbali zimefanywa na Serikali
katika kuhakikisha Sekta ya TEHAMA inakua nchini na miongoni mwa jitihada hizo
ni pamoja na uanzishwaji wa vituo vya Mawasiliano vya Jamii (Community Telecentres), ujenzi wa
Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (National ICT Broadband Backbone-NICTBB), Uanzishwaji
wa Wakala wa Serikali wa Mtandao, Uanzishwaji wa Vituo vya Kutunzia kumbukumbu
za TEHAMA (Data centres), na Mradi wa Anwani za Makazi na Simbo za Posta.
Tume hii inalenga kutambua na
kuvutia fursa za uwekezaji katika TEHAMA, kutoa ushauri, kuendeleza rasilimali
watu kitaifa kwenye sekta ya TEHAMA, kuendeleza program za kitaifa za TEHAMA na
kushiriki katika kuendeleza miundombinu mbalimbali ya TEHAMA yenye sura ya
kitaifa kwa kushirikisha wadau wa sekta zote.
Kwa sasa, Idara za Serikali, Mashirika,
na Asasi za aina zote zimejitahidi kuwa na tovuti zao, ili wananchi wapate
habari za vyombo hivyo kupitia mtandao huo wa kompyuta.
Serikali
imeanzisha uhamasishaji na uendelezaji wa wataalam wa TEHAMA (ICT Professionals) katika taasisi za
Serikali na sekta binafsi ili kujenga rasilimali watu nchini itakayowezesha
kutumia fursa na rasilimali za TEHAMA vizuri na kwa manufaa zaidi.
Kwa upande wa
Serikali, Wizara kwa kushirikiana na wadau wengine wa TEHAMA imekamilisha
Muundo wa Utumishi wa teknohama ambao tunaamini utatoa fursa mahsusi katika
kuendeleza watumishi wa fani hiyo ambao ina jukumu kubwa sana katika maendeleo
ya nchi yetu katika zama hizi za TEHAMA.
Mafanikio katika jitihada hizo yamekabiliwa na
changamoto nyingi ikiwemo kutokuwepo kwa chombo mahususi kinachoratibu,
kusimamia na kuendeleza TEHAMA nchini.
Ni dhahiri kuwa sekta ya Mawasiliano inakuwa kwa kasi
kubwa sana duniani kote na hapa nchini kwetu, na hivyo kufanya baadhi ya mambo
kuwa na changamoto katika utekelezaji wake hususan kutokuwepo na uratibu wa
kitaifa katika miradi na program zenye sura ya kitaifa.
Kukosekana kwa mpango wa Kitaifa wa usimamizi wa
kuhakikisha kuwa mifumo ya TEHAMA inawasiliana na hatimaye kuepuka upotevu wa
rasilimali unaotokana na taasisi mbalimbali kufanya kitu kile kile.
Changamoto nyingine ni kutokuwapo na usimamizi,
usajili wa kitaifa wa kuendeleza weledi kwa wataalamu wa TEHAMA na kuhakikisha
utoshelevu wa rasilimali watu utakaokidhi mahitaji ya maendeleo ya TEHAMA, pia
kutokuwepo chombo mahususi chenye majukumu ya kisheria.
Tume ya Teknolojia, Habari na Mawasiliano itasaidia
kukuza uchumi wa Taifa kutokana na kukua kwa sekta ya TEHAMA na kuchochea
uzalishaji, ukuaji wa sekta zingine kiuchumi na usambazaji wa huduma za jamii;
kuwa na taifa la jamii habari, lenye wataalam wanaotambulika kitaifa na Kimataifa,
na wajasiriamali katika Nyanja mbalimbali za TEHAMA kuendana na kasi ya ukuaji
wa teknolojia duniani; kuwa na uhakika wa usalama katika matumizi ya TEHAMA na
kuwepo na mfumo unaoainisha na kuendeleza uwekezaji katika sekta ya TEHAMA
kitaifa.
Tume hii inatarajia kuondoa
changamoto nyingi na kujenga mfumo utakaowezesha uwekezaji wa kushirikisha
sekta binafsi katika ujenzi wa miundombinu ya mawasiliano na TEHAMA yenye sura
ya kitaifa; Kuwepo mfumo utakaowezesha wabunifu na wajasiriamali kuendeleza
sekta ya TEHAMA; na kuweka utaratibu na miongozo ya namna bora ya kuhifadhi
vifaa chakavu vya TEHAMA (e-waste management).
“Miongoni mwa mambo muhimu na ya msingi
katika kuratibu sekta ya TEHAMA nchini, tume ya TEHAMA inatakiwa ihakikishe
inaunda Bodi ya Wataalamu wa TEHAMA ambao watasajiliwa na kufahamika kisheria
ili kulinda weledi na maadili ya usambazaji na ubora wa huduma za TEHAMA
zinazotolewa kwa jamii”, alisema Naibu Waziri wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi
na Teknolojia Mhe. January Makamba alisema
Kwa namna hiyo, tume itakuwa imesaidia
kuwa na Taifa Habari lenye wataalam waliounganishwa na chombo kimoja na hivyo
basi kuongeza wigo na dhamana ya uwajibikaji kwa huduma zitolewazo kwa jamii.
Mhe. Makamba aliongeza kuwa Tume ya Teknnolojia
ya Habari na Mawasiliano pamoja na mambo mengine itatakiwa iendelee kuleta mabadiliko na maboresho katika nyanja ya
mawasiliano na habari kwa kuhakikisha inafuta na kuondoa uwepo wa vyuo visivyo
na hadhi (feki) vinavyotoa elimu ya sayansi na teknolojia isiyokidhi viwango
vinavyotakiwa katika kuboresha sekta ya TEHAMA.
Tatizo la kuwepo na uanzishwaji wa vyuo
vya masuala ya habari ambavyo kimsingi havina ubora na havifuati Sera ya Habari
na Mawasiliano iliyoanzishwa 2003 na hivyo basi kutengeneza wataalamu wasioweza
kuendana na kasi ya mabadiliko katika nyanja ya mawasiliano nchini.
Wizara
ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia ilikabidhiwa dhamana ya kuhakikisha kwamba Teknolojia ya
Habari na Mawasiliano, Sayansi, Teknolojia na Ubunifu vinachangia kikamilifu
katika maendeleo ya nchi yetu.
Pamoja
na jukumu hilo, Wizara hii imepewa
dhamana ya kusimamia Taasisi, Mashirika, Tume na Kampuni ambazo zinachangia juhudi za Wizara
katika kuyafikia malengo na matarajio ya
wananchi. Taasisi hizo ni: Taasisi ya
Teknolojia Dar es Salaam (DIT); Taasisi ya Sayansi na Teknolojia Mbeya (MIST),Taasisi
ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela - Arusha (NM-AIST); Tume ya Nguvu za
Atomiki Tanzania (TAEC); Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH);
Shirika la Posta Tanzania (TPC); Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL); Mamlaka ya
Mawasiliano Tanzania (TCRA); na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCAF).
Kwa
mujibu wa taarifa ya Wizara hiyo, Serikali imeendelea kujenga Mkongo wa Taifa
wa Mawasiliano, ujenzi ambao ulianza rasmi mwezi Februari 2009. Awamu ya Kwanza
ya ujenzi wa mkongo wa mawasiliano imekamilika na huduma za mawasiliano
zimeanza kutolewa. Katika awamu hii, jumla ya kilometa 4,300 za Mkongo katika
Mikoa 16 zimejengwa. Mikoa hiyo ni: Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Iringa,
Mbeya, Dodoma, Singida, Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Tanga, Shinyanga, Mwanza,
Tabora, Mara na Kagera.
Taarifa
zilisema kuwa, kabla ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kuwepo na kabla ya Mikongo
ya Baharini kuunganishwa na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, gharama za simu kwa
sekunde moja zilikuwa kati ya shilingi 2.50 na shilingi 3.00.
Aidha,
gharama za mtandao wa intaneti zilikuwa shilingi 12,400,000 kwa kiwango cha
sita (6) mega bits/sec dedicated internet bandwidth ambapo hivi sasa, gharama
ya simu na matumizi ya mtandao zimepungua.
Serikali kupitia
wizara husika imekamilisha tathmini ya uanzishwaji wa Mtandao wa Elimu na
Utafiti (National Education and Research
Network-NREN) utakaounganisha vyuo vikuu na vituo vya utafiti 27 katika
Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kupitia Mradi wa Sayansi Teknolojia na Elimu ya
Juu unaofadhiliwa na Benki ya Dunia katika
jitihada za Serikali kupeleka huduma za mawasiliano hadi vijijini, Serikali
imeanzisha Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCAF).
Madhumuni ya Mfuko
huu ni kusaidia juhudi za upelekaji mawasiliano ikiwa ni pamoja na kutoa ruzuku
kwa wawekezaji watakaokuwa tayari kupeleka huduma za mawasiliano maeneo ya
vijijini na baadhi ya maeneo ya mjini yasiyokuwa na mvuto kibiashara.
Hadi sasa Mfuko
umeainisha vijiji 239 katika mikoa 17 ambayo ni Dodoma, Arusha, Tanga,
Morogoro, Pwani, Lindi, Ruvuma, Iringa, Mbeya, Singida, Tabora, Rukwa,
Shinyanga, Kagera, Mara, Manyara na Kigoma (Kiambatisho Na.10). Aidha, vijiji 139
vimechaguliwa kwa ajili ya mradi wa majaribio (pilot project). Uhakiki wa
maeneo mengine unaendelea.
Mabadiliko na
maboresho katika teknologia ya habari na mawasiliano Tanzania yametokana juhudi
madhubuti zilizofanywa na serikali sambamba na hitaji na malengo ya millenium
na Dira yake ni kuhakikisha maisha bora
kwa kila Mtanzania katika nyanja mbali mbali yanafikiwa ifikapo 2025.
No comments:
Post a Comment