TANGAZO


Wednesday, September 17, 2014

MAKALA: Mtwara na Harakati zake za kuuaga Umaskini

Daraja la Mkapa linalounganisha Mikoa ya Kusini mwa Tanzania linavyoonekana.


Daraja la Mtambaswala linaloziunganisha nchi ya Tanzania na Msumbiji, linavyoonekana.

Daraja la Mtambaswala linaloziunganisha nchi ya Tanzania na Msumbiji.
Wananchi wakiwa chini ya Daraja la Mtambaswala linaloziunganisha nchi za Tanzania na Msumbiji. (Picha zote na Aron Msigwa-Maelezo)

Na Benedict Liwenga, MAELEZO-DSM.
17/09/2014.
KAMA utakuwa umeshawahi kuishi ama kutembelea mkoa wa Mtwara kipindi cha miaka ya Sabini mpaka mwishoni wa miaka ya tisini na kufanikiwa kuuona ama kuwepo katika mkoa huo kwa kipindi cha karibuni,utakuwa sambamba nami kifikra juu ya usemi unaolindima kwa sasa ndani ya mkoa huo usemao “Mtwara kuchele”, yaani kwa maelezo mengine maana yake “Mtwara kumekucha”.
Kwa mujibu wa Ramani ya Tanzania, mkoa huo wenye watu wakarimu, wenye kuuenzi utamaduni wao na asili yao, uko katika pembe ya Kusini-Mashariki   kabisa ya nchi.

Umepakana na Mkoa wa Lindi kwa upande wa kaskazini, Bahari ya Hindi kwa upande wa Mashariki, nchi ya Msumbiji kwa upande wa kusini na Mkoa wa Ruvuma kwa upande wa Magharibi. 
Mtwara ni miongoni mwa mikoa midogo nchini Tanzania ukiwa na kilometa za mraba 16,720 na una jumla ya wakazi 1,128,523 kwa mujibu wa sensa ya 2002.
Kati ya makabila yanayopatikana ndani ya mkoa wa Mtwara Wamakonde wanajulikana zaidi kutokana na sanaa yao ya uchongaji vinyago, pia yapo makabila ya Wamakuwa na Wayao.

Wilaya zipatikanazo katika mkoa huo ni Wilaya ya Mtwara Mjini, Mtwara Vijijini, Masasi, Nanyumbu, Newala na Tandahimba ambapo ndani yake ndipo tarafa 21, kata 98 na Vijiji 554 huzaliwa.
Mtwara ilikuwa kati ya mikoa iliyobaki nyuma kimaendelea kwa miaka mingi kutokana na ugumu wa mawasiliano ya barabara isiyopitika kwa sehemu kubwa ila baada ya kujengwa kwa Daraja la mto Rufiji lijulikanalo kama Daraja la Mkapa mnamo mwaka 2002  pamoja na  ukarabati unaoendelea kwa barabara zote zinazounganisha mkoa huo pamoja na kujengwa na daraja linalounganisha mkoa wa Mtwara na nchi ya Msumbiji lijulikanalo kama daraja la Mtambaswala na kupelekea kukua kwa uchumi wa mkoa huo.
Kwa sasa upatikanaji wa bidhaa mbalimbali kiurahisi kutoka mikoa tofauti unafanyika kirahisi na kupelekea kukuwa kwa shughuli za kibiashara ndani ya mkoa huo.

Mtu akitaka kwenda Mtwara toka Dar es salaam kwa barabara atachukua masaa manane tu, tofauti na miaka ya Sabini mpaka miaka ya tisini ambapo ilikuwa inakuchukuwa zaidi ya siku mbili mpaka tatu kwa barabara, pia usafiri wa wa ndege unapatikana kwa wepesi zaidi katika mkoa huo wa Mtwara ambapo walau kila kukicha ndege za abiria zimekuwa zikifika mkoani hapo.

Hatuwezi kuuzungumza Mkoa wa Mtwara kinagaubaga tukaiweka kando historia ya Mkoa  huu juu ya kumbukumbu ya jaribio la Waingereza la kuanzisha mradi mkubwa wa maendeleo katika eneo hilo ambalo lilishindikana kwa kipindi hicho cha mkoloni. 
Taarifa zinasema kuwa kuanzia 1947 Serikali ya kikoloni ilijenga Bandari ya Mtwara pamoja na reli lakini vile vile waliweza kuupanga mji wa Mtwara Mikindani vizuri na serikali ya mkoloni ikaamua kuanzisha kilimo cha mashamba makubwa kwa ajili ya karanga hasa zilizohitajika kwa ajili ya mahitaji ya Waingereza ya mafuta ya kupikia.
Mradi huu ulikuja kushindikana kabisa na pesa nyingi zilipotea kiasi mradi huo kufutwa kabla ya Tanzania kupata Uhuru wake, pia reli ya Kusini ilikuja kuondolewa mnamo mwaka 1963.

Ni dhahiri kuwa kwa sasa Mtwara kumekucha na mwangaza wa matumaini ya ushindi dhidi ya umasikini uliotamalaki kuwa ni ndoto baada ya nyota kuu tatu zinazoweza kuondoa giza la kiuchumi mkoani Mtwara kung’ara, ambazo ni Bandari, zikiwemo shughuli za sekta za Mafuta na Gesi.

Ndani ya mkoa huo, hizo ni nyota za mapambazuko ya kiuchumi kwani hatua nyingine kubwa zimepigwa mkoani humo baada ya hivi karibuni Bandari yake kuingia katika mchakato wa kuwa Eneo huru la biashara.

Waziri wa Uchukuzi, Dkt. Harrison Mwakyembe alisema kuwa, kufanywa kwa Mtwara kuwa na eneo la Bandari Huru ni fursa kwa Makampuni kote duniani kuwekeza mkoani humo ili kuhudumia Mashirika yanayohusika na shughuli za gesi asilia na mafuta.
“Nawasihi wote wanaohusika wafanye maandalizi yanayohitajika ili wenye kutaka kuja kuwekeza waweze kufanya hivyo bila vikwazo,” alisema Dkt. Mwakyembe.
Dkt. Mwakyembe, aliongeza kuwa Bandari hiyo itawezesha kufanyika kwa biashara ya maeneo ya mbali ya Kusini na Mashariki mwa Afrika, yakiitumia Bandari hiyo kama kitovu cha biashara.
Chini ya Mkataba kati ya Mamlaka za Bandari Tanzania (TPA) na Export Processing Zone Authority (EPZA), jumla ya eneo lenye ukubwa wa hekta 110 limetengwa kwa ajili ya uwekezaji katika shughuli za gesi na mafuta huku zikivuta kampuni za Kimataifa mbalimbali zikiwemo; Schlumberger, Weatherford, Halliburton International Inc za nchini Marekani, pia kampuni ya Lena, FFF (T), Alpha Group, Tans Ocean Industries & Services, Queensway kutoka Dubai na Uingereza; Altus Tanzania Ltd kutoka Singapore na Inter-shore Tanzania Ltd ya Afrika Kusini bila kukisahau Kiwanda cha Cement cha Dangote.
Kampuni hizo zinaongeza idadi katika kampuni nyingine kubwa ambazo zimekuwa zikiendesha shughuli zake za awali mkoani Mtwara kama BG Group, Exxon Mobil, Statoil, Petrobras, na nyingine kama Ophir Energy, Ndovu Resources, na Maurel & Prom.
Nyaraka kadhaa zilizoandaliwa mwaka 2012 na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, zinaonyesha kuwa, katika kipindi cha miaka mitano hadi minane ijayo mkoa huo utakuwa Kitovu cha Uchumi unaoendeshwa kwa Gesi Asilia na mazao yatokanayo na gesi na mafuta kwa eneo lote la Afrika Kusini Mashariki kwa maana ya Congo DRC, Malawi, Msumbiji, Tanzania na Zambia.

“Bandari ya Mtwara ni lango la asili kwa biashara za Kimataifa yenye uwezo wa kuhudumia eneo tajiri kwa maliasili la Kusini Mashariki mwa Afrika lijulikanalo kama Ukanda wa Maendeleo wa Mtwara (Mtwara Development Corridor) uliosambaa katika maeneo ya kijiografia ya Malawi ya Kati na Kaskazini, Kaskazini mwa Msumbiji, Kusini mwa Tanzania, Kaskazini mwa Zambia na Kusini Mashariki mwa Congo DRC,” Alisema Dkt. Mwakyembe.

Nyaraka zinaeleza pia, ukiacha kwamba Mtwara itakuwa kitovu cha shughuli za utafutaji na uzalishaji gesi asilia na mafuta.

Chini ya mpango wa muda mrefu wa Mtwara Development Corridor, mkoa huo utahusika na usafirishaji na uwekezaji wa miradi mikubwa ya madini kama vile Nickel, Uranium, Chuma, Titanium, Shaba pamoja na Makaa ya mawe yanayokadiriwa kuwa yataongeza tani za mzigo zipatazo milioni 15 kila mwaka zote zikipita katika Bandari ya Mtwara.

Tayari Kampuni ya Sichuan Hongda Group kutoka China na Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) wameingia mkataba wa dola za Marekani bilioni tatu katika mradi wa ubia wa kuendeleza hazina ya madini katika eneo la Liganga na makaa ya mawe katika maeneo ya Mchuchuma na Ngaka.

Pia tayari kazi imeanza ya ujenzi wa kiwanda cha Saruji cha Dangote kitakachozalisha meta milioni tatu pembezoni mwa mji wa Mtwara.
Taarifa zinaendelea kueleza kuwa Kiwanda hicho kinatarajiwa kuzalisha hadi tani milioni saba ifikapo mwaka 2018, na hiyo ni sehemu ya taarifa shughuli zilizokwishakuanza na ambazo zitaendelea kwa miaka mingi ijayo mkoani humo na maeneo yake ya jirani.
Kutokana kukucha kwa mkoa wa mtwara kunakotokana na kuchanua kwa mazingira ya kiuchumi kwa uwepo wa bandari ya asili na yenye kina kirefu Afrika Mashariki pamoja na ugunduzi wa mafuta na gesi alikadharika na kuunganisha mkoa wa Mtwara na mikoa mingine chini ya mradi wa Mtwara Development Corridor wawekezaji mbali mbali wakubwa na wadogo wanajisogeza ndani ya mkoa huo kuwekeza na kuufanya ukuwe kiuchumi zaidi.
Hivi sasa kuna ujenzi wa nyumba za makazi na majengo ya biashara kwa wingi kutokana na ongezeko kubwa la wageni wanaokuja kufanya biashara na wengine kuajiriwa katika miradi na sekta mbalimbali zinazoendelea ndani ya mkoa huo.

Tayari benki mbalimbali kama vile CRDB Bank imaahidi kufungua tawi katika eneo la Kiwanda cha Dangote ambapo itawezesha wafanyakazi wa eneo hilo kupata huduma za kibenki kwa urahisi lakini pia Benki Kuu ya Tanzania (BOT) wanajenga ghorofa kwa ajili ya ofisi zao.
Ujenzi wa hoteli za kisasa umeshamiri kwa ajili ya kuhakikisha kuwa wageni wanaofika mkoani humo kila kukicha wanapata mahala pazuri pakupumzika kitu ambacho hupelekea biashara ya hoteli kukua pamoja na nyumba na hasa thamani ya ardhi kupanda mara dufu.
Ndani ya Manispaa ya Mtwara Mikindani miundombinu ya barabara za lami imeongezeka kutoka nne zilizokuwepo mwaka juzi na ambapo kwa sasa Benki ya Dunia imefadhili ujenzi wa barabara kadhaa ambazo pia zitawekwa taa za barabarani kama ilivyo katika Majiji mengine hapa nchini.

Nikiwa shuhuda wa haya, nimeweza kuona Ujenzi wa barabara ziendazo Soko la Samaki (Ferry) kijulikanacho kama Kivuko cha kwenda Msanga Mkuu, pia nimeambiwa kuwa uundwaji wa kivuko hicho unaendelea vizuri.
Aidha, Kivuko cha Kilambo kwenye Mto Ruvuma kuelekea nchi ya Msumbiji kimekwishamilika.
Sambamba na hayo, Serikali imekwishaweka mpango wa upanuzi wa Uwanja wa Ndege mkoani humo ili usafiri uzidi kuwa wa urahisi kwa ndegelakini pia ukpo usafiri mzuri wa mabasi ya kisasa yatokayo Mtwara kwenda Dar es Salaam pamoja na wilaya zilizopo jirani na mkoa lakini jambo lililo zuri zaidi, katika mkoa huo ni kwamba hakuna mgao wa umeme.
Hali ya uwepo wa Vituo vya redio ni ya kuridhisha kwani kwa sasa vituo vingi vya redio vimefunguliwa na vinaendelea kufanya kazi ya kuhabarisha Umma.
“Ama kweli Mtwara kuchele!!!”

No comments:

Post a Comment