Rais Jakaya Kikwete, akiwahutubia wananchi wa Mangaka, Masasi na Mtwara, wakati alipokuwa akizindua mradi wa ujenzi wa Barabara ya Mangaka-Mtambaswala kuelekea nchini Msumbiji yenye urefu wa Km 65.5 na kuzindua Barabara mpya ya Masasi- Mangaka, yenye urefu wa Km 55.1 mjini Mangaka jana.
Rais Jakaya Kikwete, akifunua pazi ili kuweka jiwe la msingi wa mradi wa ujenzi wa Barabara ya Mangaka-Mtambaswala kuelekea nchini Msumbiji yenye urefu wa KM 65.5 itakayojengwa kwa kiwango cha lami na Kampuni ya China Sichuan Road and Bridge (Group) Corporation, mjini Mangaka, mkoani Mtwara jana. Kulia ni mkewe, Mama Salma na kulia kwake ni Balozi Mdogo wa Japan, Kaziyoshi Matsuyaga. (Picha zote na Kassim Mbarouk)
RAIS Jakaya Kikwete, amesema Mungu ni mwema baada ya kumwezesha kutimiza ahadi yake kwa wananchi wa Wilaya ya Masasi na Mangaka wilayani Nanyumbu.
Amesema mwaka 2005, akiwa Masasi katika kampeni zake za kuwania urais alitoa ahadi kwa kujibaraguza kuwa atawajengea barabara kwa kiwango cha lami huku akijua kwamba hiyo si kazi rahisi.
Rais Kikwete alitoa kauli hiyo jana jioni wilayani Nanyumbu wakati akizindua Barabara ya kutoka Masasi mpaka Mangaka yenye urefu wa km 55.1, na kuweka jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa Barabara ya Mangaka kwenda Mtambaswala na kueleza kuwa alifanya hivyo ili achaguliwe kuwa rais na akishachaguliwa aangaike nayo.
"Mwaka 2005 nilipokuja hapa nilitoa ahadi kwa kujivunga kuwa nitawajengea hii barabara kwa kiwango cha lami nikiamini si kazi rahisi. Kimsingi ni kwamba nilifanya hivyo ili nikichaguliwa na kuwa rais nitaangaika nayo.
"Mwenyezi Mungu ni mwema nilipochaguliwa kuwa rais nimepambana, nikaomba fedha Japan na Benki ya Maendeleo Afrika (ADB) na Marekani wakatusaidia na leo hii mnasafiri kwa urahisi tofauti na huko nyuma," alisema Rais Kikwete huku akishagiliwa na wananchi waliokuwa wamefurika kushuhudia uzinduzi huo.
Akiendelea kuzungumza Rais Kikwete alisema wananchi wa Mtwara wamesubiri kwa kipindi kirefu lakini kwa sasa wameanza kupata mwanga wa matumaini kwa Serikali kupata ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili.
Naye, Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB), Tonia Kandiero akizungumza katika uzinduzi huo alisema Tanzania imekidhi vigezo vya kupata fedha kutoa benki hiyo.
Alisema kuanzia sasa Tanzania baada ya kukidhi vigezo itakuwa ikipata fedha nyingi kwa ajili ya shughuli za maendeleo.
Kwa upande wake Balozi mdogo wa Japan nchini, Kazuyoshi Matsunaga alisema miradi hiyo ya barabara ni mojawapo ya miradi muhimu katika Afrika ikitiliwa maanani kuwa inaunganisha mikoa ya kusini mwa Tanzania na Msumbiji, Malawi na Zambia hivyo itaongeza usafirishaji wa watu na bidhaa za nchi hizo.
"Mtwara sasa umekuwa mkoa wenye shughuli nyingi kutokana na kugundulika kwa gesi. Nina imani kuwa mradi huu utatoa mchango katika maisha ya wananchi mkoani humo, si tu kwa ajili ya viwanda vitakavyotegemea gesi lakini pia sekta nyingine kama kilimo kwa kuhamasisha uuzaji wa mazao kwenda mikoa mingine na uendezaji wa uwekezaji kwa maeneo haya," alisema Matsunaga.
Alitumia fursa hiyo kuwakumbusha madereva kuendesha kwa kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kupunguza au kumaliza tatizo la ajali ambazo zimekuwa zikipoteza maisha ya watu.
"Natambua umuhimu wa barabara. Siri ya ukuaji wa uchumi wa Japan umetokana na barabara zenye ubora. Japan ni nchi ndogo kuliko Tanzania. Ni imani yangu kuwa Tanzania sasa kutokana na barabara zinazoendelea kujengwa itaweza kusafirisha mizigo na abiria kwenda nchi za jirani na hivyo kukuza uchumi wake. Lakini ili haya yatimie madereva wanapaswa kuzingatia uendeshaji wa uangalifu," alisema.
Barabara ya Mangaka mpaka Mtambaswala yenye urefu wa km 65.5, inajengwa na Kampuni ya Ujenzi ya China Sichuan Road and Bridge (Group) Corporation (SRBG) kwa gharama ya zaidi ya sh. Bilioni 124 inatarajiwa kumalizika katika kipindi cha miezi 24.
Fedha za ujenzi huo zimetolewa na Jaica, ADB na Serikali ya Tanzania.
No comments:
Post a Comment