Hussein
Makame-MAELEZO
WAKATI Wakuu wa Nchi za Afrika Mashariki walipotia
saini Mkataba wa kuanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1999, kila upande
ulilenga maslahi ya kiuchumi na maendeleo kwa nchi na wananchi wake katika
nyanja mbalimbali.
Lakini ni ukweli ulio wazi kwamba mafanikio ya nchi
katika jumuiya hiyo hutegemea kwa kiasi kikubwa na ushiriki wa wananchi katika
hatua za mtanagamano huo kwani wao ndio walengwa wakuu katika mchakato huo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki Joyce Mapunjo akizungumza na moja ya chombo cha habari wakati wa maadhimishi ya wiki ya Utumishi wa Umma yaliyofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam.Picha na Hussein Makame-MAELEZO.
Ni miaka 14 imepita tangu wakuu wa nchi za Afrika
Mashariki waliposaini Mkataba wa kuanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki na miaka
9 tangu kuanza kwa utekelezaji wa hatua ya kwanza ya mtangamano wa jumuiya
hiyo.
Pamoja na mafanikio ambayo Tanzania imeanza kuyapata
kutokana na hatua mbalimbali za mtangamano wa jumuiya hiyo, inaelezwa kuwa bado
mwitikio wa wananchi katika kuchangamkia fursa zilizopo uko chini.
Msemaji wa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Vedastina Justinian anasema baada ya maandalizi ya miaka sita, nchi
tano wanachama wa jumuiya hiyo zilianza kutekeleza rasmi hatua ya Umoja wa
Forodha mwaka 2005.
Katika hatua hiyo nchi ziliwekeana muda wa kipindi
cha miaka mitano za utekelezaji ambapo nchi ya Kenya ilianza kuingiza bidhaa
katika nchi ya Tanzania na Uganda kwa kutozwa ushuru ambao ulikuwa unapungua
mwaka hadi mwaka.
“Sisi Tanzania na Uganda tulikuwa tunapeleka bidhaa
zetu Kenya bure bila ya kutozwa ushuru kwa sababu Kenya ilikuwa imeendelea
kiviwanda, kwa hiyo ilitupa muda na sisi tuwe tumejiandaa vizuri” anasema
Vedastina.
Anafafanua kuwa mpaka mwaka 2010 Kenya ilianza
kuingiza bidhaa katika nchi hizo mbili bila ya kutozwa ushuru na baadaye nchi
wananchama zilianza hatua ya pili ya mtangamano huo ambayo ni Soko la Pamoja.
Soko la pamoja lilianza kutekelezwa kuanzia Julai mwaka
2010 na lilijumuisha soko huru la bidhaa, soko huru la mitaji, wananchi kuingia
na kukaa katika nchi anayotaka ilimradi ana pasipoti pamoja na soko huru la
ajira.
Vedastina anasema kuwa kila nchi ilianisha maeneo
ambayo iliyafungua kwa mfano Tanzania ilifungua maeneo ya walimu wanaofundisha
lugha za kigeni, maafisa ugani, madaktari, marubani na maeneo mengine ambayo yalikuwa
yanaonekana kuwa na upungufu.
Anasema kwa sasa shirikisho hilo liko kwenye hatua
ya Umoja wa Fedha ambao itifaki yake ilisainiwa Novemba mwaka 2013, muda wa
miaka 10 uliwekwa kufanya maandalizi ya kutekeleza hatua hiyo.
“Maandalizi hayo ni kuweka uchumi wetu ukae vizuri
tuwe na mfumuko wa bei angalau unayofikia asilimia 8 kila nchi, tuwe na bajeti
zisiyotegemea misaada kwa nakisi za bajeti zetu zisizidi asilimia 3 ya Pato la
Taifa” anafafanua Vedastina na kuongeza kuwa:
“Vile vile tuwe na akiba za fedha za kigeni ya
kutosha ambayo tulijiwekea kuwa kila nchi iwe na akiba ya fedha za kigeni za
kukutosheleza muda wa miezi minne na nusu, pia nchi tuwe tumejiwekea taasisi
muhimu za utekelezaji wa umoja wa fedha kwa mfano benki kuu kuna taasisi ambazo
zinatakiwa ziwepo.”.
Anasema baada ya miaka hiyo 10 nchi wanachama
zitakaa chini kuangalia kama zimejiandaa vya kutosha kuanza utekelezaji wa
matumuzi ya sarafu moja na hatua hizo
zitakapotekelezwa ipasavyo nchi zitaanza utekelezaji wa shirikisho la kisiasa.
Akizungumzia matarajio ya Umoja wa Fedha wa Jumuiya
ya Afrika Mashariki, Vedastina anasema baada ya miaka 10 hatua inayofuata ni sarafu
moja ambapo gharama za kufanya biashara zitapungua.
“Sasa hivi unapokwenda kufanya biashara nje ya
Tanzania katika nchi za Jumuiya kwa mfano Kenya inabidi ubadilishe fedha kwenda
shilingi ya Kenya au Franga za Burundi au Rwanda au uende kwenye fedha ya
Uganda” anasema Vedastina.
Anafafanua kuwa kwa sasa mtu anapobadilisha fedha
kuna fedha anayokatwa kwa sababu anayekubadilisha
anataka faida, lakini ikifikia hatua ya umoja wa sarafu kutakuwa na fedha ya
aina moja itakayotumia katika nchi zote za Jumuiya.
Akizungumzia mwitikio wa Watanzania kuchangamkia
fursa zilizopo, Vedastina anasema katika eneo la ajira Watanzania bado
wanajiweka nyuma kwamba hawataki kuvuka mipaka kwenda kufanya kazi nchi
nyingine.
“Katika eneo la ajira natoa wito tu kuwa Watanzania
wachangamkie hizi fursa kwani,Watanzania bado wanajiweka nyuma kwamba hawataki
kuvuka mipaka kwenda kufanya kazi sehemu nyingine, ni wachache ambao wameweza
kuthubutu na wameweza kufauru kwenda katika nchi nyingine” anasema Vedastina.
Anawataka Watanzania wanapotafuta ajira wasiangalie
tu kwa Tanzania na kusema wamekosa ajira badala yake waangalie soko la Afrika
Mashariki kwani ajira zipo na pia kwa bidhaa kuna soko la watu milioni 140
katika jumuiya hiyo.
“Wakati mtu anatafuta ajira aingie kwenye mtandao
aangalie hata kwa wenzetu wanataka watu wa aina gani kama ana sifa
zinazohitajika aombe, anaweza akaajiriwa Kenya, Uganda, Rwanda na hata Burundi”
anasisitiza Vedastina.
Anasema kuwa katika kipindi hiki ambapo wanafunzi
wanahitimu katika vyuo vikuu waanze kuchngamkia soko la ajira la Afrika
Mashariki.
Kwa upande wa wafanyabiashara, Vedastina anasema
bado wako nyuma na kutoa mfano kuwa wakulima wanasubiri wafanyabiashara watoke
nchi jirani waende wakachukue bidhaa mashambani huku wao hawataki kuvuka mipaka.
Anatoa wito kwamba Watanzania wachangamkie fursa hizo
na watoke nje ilimradi wawe na pasipoti, bidhaa zao zinakidhi ubora na viwango na
zina uasilia wa bidhaa.
“Kama umezalisha bidhaa zako Tanzania tafuta cheti
cha uasilia wa bidhaa ambacho kinapatikana TRA auTCCIA uweze kukidhi vigezo vya
kuvuka nje ya Tanzania na kuweza kuangalia soko kubwa kwani sasa hivi
tunategemea tutaingiza bidhaa hadi Sudan Kusini” anasema Vedastina.
Anasema Watanzania wana bidhaa nyingi za kilimo na bidhaa
zao zina ubora huku akitolea mfano maonesho ya Juakali Nguvukazi, ambapo watu
wanakimbilia bidhaa za Tanzania ikiwemo asali, batiki, vinyago, mchele
na nyingine.
Kutokana na hali hiyo, Vedastina anawataka
Watanzania waache woga wa kwenda nchi za Afrika Mashariki kwani wafanyabiashara
wa nchi nyingine wanachangamkia masoko
bila kujali mipaka ya nchi yao.
Anafafanua kuwa “unajua sasa hivi wafanyabiashara
kutoka nje labda Kenya, anakuja ananunua shamba zima anasema nitavuna mwenyewe,
nakulipa tu shamba zima nitavuna mwenyewe nitapeleka nje.
Kwa nini ukubali mtu anunue shamba ajivunie mwenyewe, vuna mwenyewe wauzie wafanyabiashara wavushe mipakani au vuka mwenyewe ukauze nje uvumbuke macho.
Bila kuangalia wenzetu wanafanya nini utakaa tu unalaliwa bei unaouza kwa bei ya chini wenzako wanauza kwa bei ya juu sana, kwa hiyo natoa wito kwamba Watanzania waaamke wasisubiri watu kutoka nje kingia hadi mashambani”.
Anasema iwapo Watanzania watabaki hivyo walivyo matokeo yake hawatapata faida kubwa ya mazao yao na pia unakosa uzoefu wa kujifunza kwa kuangalia wafanyabiashara wa nchi nyingine wanafanya nini kuboresha biashara zao.
“Kwa mfano Tanzania, wafanyabiashara au wakulima hawajajua hata jinsi ya kufungasha vizuri hizi bidhaa utakuta wenyewe ufungashaji wao ni hafifu sana, lakini unapotoka nje akaangalia wenzetu wanafanya nini mtu anajifunza anakuja na yeye anafanya vizuri” anafafanua Vedastina.
Ili kuhakikisha Watanzania hawaachwi nyuma katika mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Vedastina anawataka Watanzania wajielimishe kuhusu mambo ya Jumuiya hiyo kwani bado wako nyuma na hawana uelewa wa kutosha.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini ambaye ni
Msemaji wa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki Vedastina Justinian
akimsikilia mwananchi aliyetembelea banda la wizara hiyo kwenye maadhimisho ya wiki
ya Utumishi ya Umma yaliyofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam.Picha na
Hussein Makame-MAELEZO.
No comments:
Post a Comment