Madaktari nchini India wametumia saa 7 kufanikisha upasuaji wa
kinywa cha kijana Ashik Gavai mwenye umri wa miaka 17 aliyekuwa akipata maumivu
ndani ya kinywani .
Dr Sunanda Dhiware, mkuu wa Kitengo cha tiba ya meno katika hospitali ya JJ mjini Mumbai ameiambia BBC kuwa wamefanikiwa kuyang’oa meno 232 kinywani mwa Ashik aliyeletwa hospitalini hapo akiwa amevimba taya huku akilalamika kwa maumivu makali.
Madaktari wamesema wamelazimika kutumia nyundo na tindo kuyatoa meno hayo na wakadai kwamba hilo ni tukio la ajabu na linaingia katika rekodi ya dunia.Hata hivyo Upasuaji huo umehusisha jopo la madaktari wanne.
Dr Dhiware anasema katika uzoefu wake wa miaka 30 ya udaktari wa kinywa na meno hajawahi kukutana na tukio la namna hiyo. Ameongeza pia kuwa kulingana na vitabu vilivyopo vinasema hali kama hiyo inaweza kujitokeza katika taya la juu na meno yaliyowahi kung'olewa katika hali hiyo yalikuwa 37 lakini cha kushangaza ni kuwa tukio la Ashik Gavai limetokea katika taya ya chini na ameng'olewa meno 232 idadi ambayo ni kubwa huku akisalia na 28 kwa matumizi yake ya kawaida wakati kitaalamu mtu mzima anapaswa kuwa na meno 32.
Baba mzazi wa kijana Ashik ,Suresh Gavai amenukuliwa akisema mtoto wake alikuwa akilalamika kwa miezi kadhaa juu ya maumivu na kwamba walidhani inaweza kuwa ni matatizo ya saratani na ndipo wakamleta Mumbai.
No comments:
Post a Comment