Mkulima akifafanua jambo kwenye moja ya mafunzo ya kilimo. (Picha zote na John Banda)
Mtaalamu wa masuala ya nyuki akitoa maelezo kwa wakulima (hawapo pichani), wakati wa mafunzo ya kilimo.
Wakulima wakiwa katika mafunzo ya kilimo cha alizet, mtama na ufugaji nyuki.
Na John Banda, Dodoma
KILIMO ni moja ya sekta ambazo zinategemewa kwa kiasi kikubwa hapa nchini na watanzania waliowengi ikiwa kama ni sehemu yao ya kipato ili waweze kujikwamu kiuchumi, Makala hii inaeleza.
KILIMO ni moja ya sekta ambazo zinategemewa kwa kiasi kikubwa hapa nchini na watanzania waliowengi ikiwa kama ni sehemu yao ya kipato ili waweze kujikwamu kiuchumi, Makala hii inaeleza.
Pamoja na idadi kubwa ya wananchi kukitegemea kilimo kama ni sehemu yao
ya kujikwamua kiuchumi bado kuna changamoto
mbalimbali zinazowakabili wakulima.
Changamoto hizo ni pamoja na ukosefu wa elimu ya kutosha katika suala
zima la kilimo inatokana na wakulima wengi kuendelea kulima kilimo cha kienyeji
hivyo kuwafanya washinde kujikwamua kiuchumi.
Nyingine ni serikali bado haijaweka mkazo katika kuwasaidia wakulima wadogo
ili kuboresha namna ya kilimo chao kwa kuwawezesha pembejeo za kisasa na kwa
wakati mwafaka.
Hali hii imechangia kwa kiasi kikubwa wakulima wadogo kuendelea kulima
kilimo kisicho kuwa na tija na kuendelea kuwa masikini pamoja na kutumia muda
wao mwingi kulima maeneo makubwa na kupata mavuno kidogo tofauti na gharama
walizo tumia.
Kutokana na hali hiyo inaisukuma kampuni ya wasindikaji wadogo wa mafuta
ya alizeti mjini Dodoma ya Three sisters, kwa kushirikiana na Shirika lisilo la
kiserikali linalojihusisha na wakulima wadogowadogo(Rldc) kuanzisha utaratibu
wa kutoa mafunzo kwa wakulima ili kuweza kuwasaidia kuboresha kilimo chao.
Mmoja wa wakurugenzi wa Kampuni hiyo Mariam Majengo, anasema kuwa
wakulima wadogowadogo zaidi ya 6,000 katika wilaya za Chemba na Chamwino mkoani
Dodoma watanufaika na mafunzo ya kilimo cha kisasa cha mtama, alizeti,ufugaji
nyuki na upandaji wa miti utakaowasaidia kujikwamua katika hali duni ya maisha.
Anasema kuwa mafunzo hayo yanatolewa kwa ushirikiano wa shirika hilo na kampuni
ya kukamua mafuta ya alizeti ya Three Sisters Company Ltd.
Anasema kuwa mradi huo utahusisha jumla ya vijiji 36 ambapo wakulima
watapatiwa mafunzo ya kilimo cha kisasa ili kuweza kuzalisha mavuno mengi
tofauti na ilivyo hivi sasa.
Majengo anasema kuwa mafunzo hayo yamelenga kuwawezesha wakulima wenye
maisha duni ili kuweza kujikwamua kiuchumi na kuboresha maisha yao kupitia
kilimo na ufugaji wa nyuki.
Anasema kuwa pamoja na mafunzo hayo pia watawapatia mikopo ya pembejeo
mbalimbali za kilimo ambazo watazitumia katika kufanikisha kilimo bora na cha
kisasa ili kuweza kujikwamua kiuchumi.
Anafafanua kuwa katika mafunzo hayo yatawasaidia wakulima kulima alizeti
yenye kiwango bora na kukidhi viwango vya kimataifa ili kuwauzia watu wenye
viwanda vya kukamua mafuta.
“Kama wakulima watakuwa na elimu ya kutosha juu ya kilimo cha alizeti
watatoa alizeti iliyo bora hali ambayo itasaidia hata viwanda vyetu kutoa
mafuta yenye ubora na kukidhi viwango pia na wao kujipatia kipato kwa kuuza
mazao yaliyo bora,” anasema.
Anaongeza kuwa kilimo cha zao la
mtama kitawasaidia kupata chakula cha kutosha.
Kuhusu ufugaji nyuki anasema wataweza kuuza zao la asali wakati msimu wa
kilimo ukiwa umekwisha hivyo kuwafanya kila wakati kuwa na uhakika na maisha
yao.
Anasema kuwa katika mafunzo hayo wanawasisitiza sana wakulima
kuhakikisha pia wanafuga nyuki ambao watawasaidia katika kuchavusha maua ya
alizeti katika mashamba yao.
Anasema kuwa mazao yanayochavushwa na nyuki huwa yanaubora tofauti na
yale yanayochavushwa kwa upepo hivyo itawasaidia kuuza mazao yenye ubora na kwa
bei nzuri tofauti na sasa.
“Pamoja na nyuki kutumika katika kuchavushwa pia wakulima wakishavuna
asali watauza kwa bei nzuri ambayo itawawezesha kujipatia kipato na kuondokana
na suala la uharibifu wa mazingira kwa kuendekeza tabia ya ukataji wa mkaa
unachangia kwa kiasi kikubwa kuharibu mazingira,”alisema Majengo.
Anabainisha kuwa toka waanze kutoa mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa
zaidi ya miaka mitatu iliyopita hali ya ubora wa mazao imebadilika tofauti na
ilivyo kuwa awali kwakuwa wakulima wanazalisha mazao yenye ubora na kujipatia
soko la kutosha kwa watu wenye viwanda vidogovidogo vya kusindika mafuta ya
alizeti.
“Zamani mkulima alikuwa analima heka nne na kupata gunia mbili hadi tatu
lakini hivi sasa anao uwezo wa kupata gunia nane hadi 15 kupiti kilimo cha
kisasa na matumizi ya mbegu bora,” anasema Majengo.
Anasema pamoja na kutoa mafunzo hayo ya kilimo lakini bado wamekuwa wakikabiliana
na changamoto mbalimbali ikiwemo kutoka kwa wakulima wenyewe kutotoa
ushirikiano kwa asilimia kubwa.
Anasema kuwa wakulima wengi wamekuwa wakienda kinyume na mafunzo
yanayotolewa kwa kuendelea kulima kienyeji bila ya kufuata utaratibu hivyo
kusababisha kushindwa kufikia malengo yao ya kupata mazao yenye ubora kwenye
soko.
Aidha anasema kuwa changamoto nyingine ni kukosa ushirikiano kutoka kwa
viongozi wa vijiji ambao wamekuwa wakishindwa kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa
wingi katika kupata mafunzo hayo.
Changamoto nyingine anasema ni katika kupatikana kwa masoko ya mazao
hayo pamoja na bidhaa yake ya mafuta ambayo imekuwa ikikabiliana na changamoto
ya uingizaji wa kiwango kikubwa cha mafuta kutoka nchi nyingine.
“Mafuta mengi yamekuwa yakiagizwa kutoka nchi jirani hali inayo changia
ushindani katika soko kutokana na kutokuwepo kwa ushuru wa uingizaji bidhaa
hiyo...lakini pia gharama za uzalishaji hapa kwetu ziko juu,”anasema.
Naye mmoja wa wakulima waliopatiwa mafunzo ya kulima kwa kisasa, Abuu
Mickdadi, anasema kuwa kiasi cha mavuno kimeongezeka sana ukilinganisha na hapo
awali.
Anasema kuwa awali walikuwa wakitumia nguvu nyingi kwa kulima mashamba makubwa
na kupata kiasi kidogo cha mavuno ambacho kilikuwa hakikidhi kabisa gharama waliyokuwa
wakiitumia katika kulima.
“Toka tumeanza kulima kwa kufuata mafunzo ya kilimo cha kisasa hata
kipato kimebadilika sana tunavuna mazao mengi lakini pia yenye ubora ambayo
hatuna shaka ya kupata wanunuzi,” anasema Abuu.
Mwenyekiti wa chama cha wasindikamafuta kanda ya kati (Cezosopa) Ringo
Iringo, anasema kuwa mafunzo hayo yamesaidia wakulima wengi wa zao la alizeti
kuongeza kiwango cha uzalishaji wa mafuta kutokana na kutumia mbegu zenye ubora
na kulima kwa kisasa.
Ringo anasema kuwa moja ya changamoto zilizokuwa zikiwakabili wakulima wa
zao hilo ni kutumia mbegu zisizo na ubora hivyo kusababisha kiwango cha
uzalishaji kushuka.
“Wakulima wanatakiwa kubadilika na kuanza kutumia mbegu bora ambazo
zinatoa mafuta kwa wingi na yenye ubora tofauti na ilivyo wakati huu,” anasema
Ringo.
Anasema kuwa kwakutumia mbegu bora wakulima watanufaika kwa kupata
mafuta mengi pamoja na mashudu bora kwaajili ya matumizi mengine.
Anaeleza kuwa kiwango cha uzalishaji wa mafuta nchini bado kiko chini kutokana na utumiaji wa mbegu za
kienyeji ambazo hazitoi mafuta mengi na yenye ubora.
“Mahitaji ya mafuta nchini ni takribani tani 300,000 lakini sisi kwa
kiwango cha ndani tunazalisha tani 90 elfu na asilimia nyingine yote inatoka
nje hivyo hatuna budi kujipanga katika kuzalisha mafuta mengi na yenye ubora na
ni matumaini yangu kupitia mafunzo haya kwa wakulima kiwango kitaongezeka” anasema.
Aidha anabainisha kuwa wadau wa mafuta na serikali kwa pamoja wamekutana
na kuweka mikakati madhubuti ambayo itasaidia kwa miaka michache ijayo kuongeza
uzalishaji.
“Miaka michache ijayo tutaweza kuwa tunazalisha kwa kiwango cha juu
kiasi ambacho tutakuwa hatuna haja ya kuagiza mafuta kutoka nchi za nje” anasema.
Hatahivyo anatoa wito kwa serikali kuwasaidia wasindikaji wadogo katika
kupata viwanja kwajili ya kuwekeza viwanda vyao pamoja na kuongeza mafunzo kwa
wakulima wengi walioko vijijini ili kuongeza uzalishaji.
No comments:
Post a Comment