Baadhi ya washiriki wa
mashindano ya resi za Ngalawa wakijiandaa tayari kwa kuanza mashindano
hayo katika shamra shamra za tamasha la 17 la ZIFF 2014 linaloendelea
visiwani Zanzibar.(Picha na Zainul Mzige wa MOblog).
Na Mwandishi wetu, Zanzibar.
NGALAWA zote 11 zilizoingia majini
kukamilisha mzunguko wa saa mbili wa resi za ngalawa mjini Zanzibar
zilimarisha mashamshamu hayo bila najali na timu tatu zilipewa zawadi za
ushindi.
Resi za Ngalawa kama zinavyojulikana
ni utamaduni halisi wa visiwa vya pemba na Unguja na ni sehemu ya
tamasha kubwa la filamu la kimataifa la Zanzibar ambalo linaendelea
visiwani hapa.
Kwa wale waliozaliwa maeneo ya bara,
resi hizi zilikuwa kivutio kikubwa kwao kutokana na maandalizi
yanayofanywa kabla ya kuingia majini na dau kunyanuliwa.
Wakati dau limenyanyuliwa, maji
yamekuwa yakichotwa ama ndani ya Ngalawa au nje katika bahari kumwagia
tanga katika hali inayoelezwa kuliimarisha katika ukinzani wa upepo.
“mbio za Ngalawa ni kipimo kikubwa
cha Uzanzibari wetu na kila mwaka ZIFF huhitimisha utashi wake wa kuwa
na tamasha la nchi za jahazi kwa kuwa na mbio za ngalawa” alisema
mshehereshaji Muslim Nassoro Abdalla katika shamrashamra zilizofanyika
ufukweni kandoani mwa hoteli ya Tembo.
Mwenyekiti wa Bodi ya ZIFF
ambaye pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Kiembesamaki Mhe. Mahmoud Thabit
Kombo (mwenye t-shirt ya njano) akupiliza Kipenga kuashiria kuanza kwa
mashindano hayo yaliyofanyika kwenye fukwe za Hoteli ya Tembo visiwani
Zanzibar.
Muslim ambaye alisema kwamba mwaka
huu walitaka kuwa na mbio za timu 20 (ngalawa) walishindwa kuhitimisha
ndoto hiyo kutokana na masuala nje ya uwezo wa ZIFF.
Ili kukamilisha vyema mbio hizo kunatakiwa kuwa na boti za kutosha za uokozi kama kutatokea ajali.
Mwaka juzi kulitokea ajali ambayo
hata boti ilipofanya uokozi nayo ikazidiwa na kulazimisha watu kukwama
mpaka jioni walipopata boti nyingine kutoka Bandarini.
Wakati wa mbio za resi ambazo
washindi wa kwanza ni timu iliyokuwa ikiongozwa na Hatibu Suleiman
waliokuwa ndani ya ngalawa Ipo Siku, ngoma mbalimbali za asili zilipigwa
ufukoni kama hamasa huku watu wakisubiri marejeo ya ngalawa hizo.
Baadhi ya Ngalawa zinazoshiriki mashindano hayo zikianza kukata mawimbi.
Mbio hizo ambazo zilianzishwa na
mbunge wa Kiembesamaki na Mwenyekiti wa Bodi ya ZIFF, Mahmoud Thabiti
Kombo mshindi wake wa pili alikuwa ni timu ya haji Hassan (kama
nadhodha) ndani ya ngalawa Kipanga. Aidha Hassan Simai na wenzake
waliokuwa katika ngalawa iliyoitwa peace of Love walikuwa washindi wa
tatu.
Timu ya ngalawa ambayo inahitaji
ujuzi katika utekaji tanga , kulirekebisha na kubalansi ngalawa
inahitaji watu wapatao watano na si chini ya watatu.
Tamasha la filamu linaendelea mjini
hapa kwa shughuli mbalimbali zikiwemo za mafunzo ya utunzi, utengenezaji
wa filamu na uhakiki wake.
Pichani juu na chini ni Sehemu ya wakazi wa Zanzibar wakishuhudia mashindano hayo.
No comments:
Post a Comment