Uchunguzi umeanzishwa nchini
Afrika Kusini kuhusu madai kuwa mkuu wa shirika la habari la SABC
alikabidhiwa msichana mwenye umri wa miaka 23 kama zawadi.
Tume inayohusika na maswala ya usawa wa
kijinsia, imesema kuwa imepokea malalamiko kwamba viongozi wa kitamaduni
walimkabidhi Mkuu shirika la habari la serikali SABC, Hlaudi Motsoeneng
mke kama zawadi.Viongozi hao walikuwa sehemu ya kikundi cha wazee wa kitamaduni waliokuwa wanataka vipindi zaidi vya lugha yao kupeperushwa kwenye televisheni hiyo.
Serikali imesema kuwa tabia hiyo ni ya kuchukiza sana na kwamba inajuta jambo kama hilo lilitokea.
'Wazazi walikubali'
Tukio hilo linasemekana kutokea wakati wa ziara ya hivi karibuni ya Hlaudi Motsoeneng katika mkoa wa Limpopo Kaskazini mwa nchi hiyo ambako yeye na maafisa wengine wakuu walikutana na wazee hao.
Taarifa ya serikali ilisema, ''Tabia ya kutumia wanawake kama zawadi na kufafanishwa na mifugo wanaotolewa kama zawadi wakati msichana anapooleka ni utamaduni usio kubalika na ni kinyume na haki za binadamu na pia ni kama matusi kwa demokrasia na uhuru wa watu. ''
Takriban wasichana 10 waliorodheshwa mbele ya maafisa hao huku wakitakiwa kuchagua.
'Alichagua aliyempendeza'
"wasichana wote waliambatana na wazazi wao. Wazazi walifahamu kilichokuwa kinaendelea na inaarifiwa kuwa wote walikubali.
Kwa mujibu wa jarida Sowetan, bwana Motsoeneng alichagua msichana aliyekuwa na umri wa miaka 23 ambaye pia ni mwanafunzi.
Alipigwa picha akiwa kifua uchi akisimama kando yake.
Pia inaarifiwa alikabidhiwa Ng'ombe na Ndama.
Wizara ya maswala ya wanawake nchini humo, ilisema tabia hiyo ni hujuma kwa utamaduni
"tabia ya kutumia wanawake kama zawadi ungedhani ni n'gombe, bila shaka ni hujuma kwa utamaduni, '' ilisema taarifa ya wizara hiyo.
Msemaji wa kituo cha SABC, Kaizer Kganyago, aliambia BBC kuwa hajapokea habari yoyote kuhusu uchunguzi unaofanywa na tume hiyo na kwamba ikiwa ina swali lolote kuhusiana na tukio hilo, inapaswa kuhoji viongozi hao wa kitamaduni.
Lakini msemaji wa tume hiyo, Javu Baloy naye aliambia BBC kuwa ujumbe tayari umewasilishwa kwa wote waliohusika na mapendekezo ya dhabu yatatolewa mwezi ujao.
No comments:
Post a Comment