TANGAZO


Monday, May 19, 2014

HOTUBA YA WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA NA WATOTO MHESHIMIWA SOPHIA M. SIMBA (MB.), AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA 2014/15

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Mhe. Sophia M. Simba (kushoto), akifurahi pamoja na Katibu Mkuu wa UWT, Mhe. Amina Makilagi (Mb), Naibu Waziri wa wizara hiyo, Mhe. Dk. Pindi H. Chana (Mb) na Katibu Mkuu wa wizara, Anna T. Maembe mara baada ya kupitishwa kwa Bajeti ya Wizara hiyo, juzi Jumamosi Bungeni, mjini Dodoma. (Picha zote na Hassan Mabuye, Ofisa Habari wa Wizara)
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Mhe. Sophia M. Simba (Mb.), akiwa na Nabu wake, Mhe. Dk. Pindi H. Chana (Mb) pamoja na Katibu Mkuu wa wizara, Anna T. Maembe, wakipongezana mara baada ya kupitishwa kwa Bajeti ya wizara hiyo juzi, Jumamosi Bungeni, mjini Dodoma.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Mhe. Sophia M. Simba (Mb.)

A:     UTANGULIZI

1.    Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba bunge lako tukufu baada ya kuzingatia taarifa iliyowasilishwa leo hapa Bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii,  sasa lijadili na kupitisha Makadirio ya Matumizi ya Kawaida na ya Maendeleo ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto kwa mwaka 2014/15.

2.    Mheshimiwa Spika, awali ya yote ninamshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujalia kuwa na afya njema na hivyo kuweza kushiriki mkutano huu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

3.    Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kuwapongeza Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Dkt. Mohammed Gharib Bilal, Makamu wa Rais na Mheshimiwa Mizengo Kayanza Peter Pinda, Waziri Mkuu na Mbunge wa Mpanda Mashariki kwa uongozi wao mahiri ambao umewezesha kushamiri kwa usawa wa jinsia na uzingatiaji wa haki za mtoto katika jamii ya watanzania. Mwenyezi Mungu awajalie afya njema ili waendelee kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

4.    Mheshimiwa Spika, napenda kukupongeza wewe Spika, Naibu Spika na  Wenyeviti wa Bunge, kwa uendeshaji bora wa shughuli za Bunge. Tunaendelea kumuomba Mwenyezi Mungu awajalie afya njema ili muweze kusimamia na kuratibu shughuli za Bunge kwa ufanisi.

5.    Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua fursa hii kuishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii ikiongozwa na Mwenyekiti wake mahiri Mheshimiwa Saidi Mohamed Mtanda (Mb.) na Makamu Mwenyekiti Mheshimiwa Kapteni Mstaafu John Damiano Komba (Mb.) kwa kuichambua na kuijadili bajeti ya Wizara yangu. Ushauri na maelekezo ya Kamati hiyo yametuwezesha kuboresha na kukamilisha bajeti katika muda muafaka.

6.   Mheshimiwa Spika, naomba nichukue fursa hii kuwapongeza Mheshimiwa Samuel Sitta (Mb.) kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti  wa Bunge Maalum la Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Samiya Suluhu Hassan (Mb.) kuwa Makamu Mwenyekiti. Aidha, nawapongeza Mheshimiwa Godfrey  William Mgimwa (Mb.) kwa kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Kalenga na Mheshimiwa Ridhiwani Jakaya Kikwete kuwa Mbunge wa Chalinze.

7.    Mheshimiwa Spika, naomba nitangulize dua zangu kwa Mwenyezi Mungu azipokee na kuzilaza mahali pema peponi roho za Marehemu William Agustino Mgimwa aliyekuwa Mbunge wa Kalenga na marehemu  Said Bwanamdogo aliyekuwa Mbunge wa Chalinze. Bunge hili litawakumbuka daima kwa michango yao.

8.    Mheshimiwa Spika, kwa masikitiko makubwa natumia fursa hii kuwapa pole wale wote waliopatwa na majanga pamoja na kufiwa na ndugu, jamaa na wapendwa wao katika matukio mbalimbali yaliyotokea nchini.

B:     MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA ILANI YA UCHAGUZI YA CCM YA MWAKA 2010 KWA KIPINDI CHA JANUARI, 2011 HADI MACHI, 2014

9.      Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2013/2014, Wizara yangu iliendelea kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2010. Mafanikio ya utekelezaji wa Ilani kwa kipindi cha kuanzia Januari, 2011 hadi Machi, 2014 ni haya yafuatayo.
          I.    Ajira na Uwezeshaji wa Wananchi

10.     Mheshimiwa Spika, Ibara ya 78 ya Ilani ya CCM, imeelekeza uimarishaji na upanuzi wa mafunzo ya Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi ili viweze kupokea vijana wengi zaidi na kuwapatia mafunzo ya  stadi na maarifa ya kisasa katika fani za kilimo, biashara, ufundi na ujasiriamali.

11.     Mheshimiwa Spika, Mafunzo ya kuwapatia wananchi ujuzi na stadi mbalimbali ili waweze kujiajiri na kuongeza uzalishaji mali na kipato ni muhimu hasa katika kipindi hiki cha ukosefu mkubwa wa ajira. Wizara kupitia Vyuo 55 vya Maendeleo ya Wananchi, iliwapatia mafunzo  wananchi146,383 wakiwemo wanawake 70,841 na wanaume 75,542 kupitia kozi fupi, kozi ndefu na mafunzo nje ya vyuo kwa kipindi cha Januari, 2011 hadi Machi, 2014. Mafunzo yanayotolewa ni pamoja na: uashi, useremala, ufundi magari, ufundi chuma na uchomeleaji, kompyuta, ushonaji, umeme wa majumbani, kilimo, ususi na upishi. Aidha, Wizara imeendelea kutoa mafunzo ya ufundi stadi yanayoratibiwa na Mamlaka ya Ufundi Stadi (VETA) kupitia vyuo 25 vya Maendeleo ya Wananchi ambapo kumekuwa na ongezeko la wanafunzi wanaopata mafunzo haya kutoka 1,125 mwaka 2013 hadi kufikia 2,722  mwaka 2014.

  II.      Kuyaendeleza Makundi Mbalimbali Watoto

12.     Mheshimiwa Spika, Ilani ya CCM ya mwaka 2010 Ibara ya 204 (a), (h) na (j) inaiagiza Serikali kukamilisha Sera ya Malezi na Makuzi ya Mtoto na kupitisha Sera Fungamanishi ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto ili watoto wote nchini waweze kunufaika kutokana na utekelezaji wake. Aidha, Ibara hiyo inaitaka Serikali kutekeleza mikataba ya haki za mtoto iliyoridhiwa na Bunge.

13.      Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza azma hiyo, Wizara yangu imeendelea kufanya mapitio ya Sera ya Mtoto na kutekeleza mikataba ya kimataifa kuhusu haki na maendeleo ya mtoto iliyoridhiwa na Bunge lako tukufu. Wizara imefanya marekebisho ya Sera ya Maendeleo ya Mtoto ya mwaka 2008 na imeandaa rasimu ya Sera ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Mtoto (2014) ili iweze kubeba masuala ya utoaji huduma fungamanishi na shirikishi kwa mtoto. Masuala mengine yaliyoingizwa katika sera hiyo ni pamoja na kuboresha upatikanaji wa huduma muhimu kwa watoto walio chini ya umri wa miaka nane. Aidha, katika kuwezesha utekelezaji wa mikataba ya kimataifa inayohusu haki na maendeleo ya mtoto, Wizara yangu inaandaa taarifa ya utekelezaji wa mikataba hiyo ili kuiwasilisha katika vikao vya tatu, nne na tano vya Mkataba wa Kimataifa kuhusu Haki za Mtoto (Convention on the Rights of the Child) katika mwaka 2014. Aidha, Wizara yangu imeendelea kuratibu utekelezaji wa Mpango wa Miaka Mitatu (2013 – 2016).

Wanawake

14.     Mheshimiwa SpikaIlani ya CCM ya mwaka 2010 Ibara ya 205 (e) na (f) inaitaka Serikali kuimarisha mifuko iliyopo ya mikopo na Benki ya Wanawake Tanzania ili wanawake wengi waweze kufaidika kiuchumi.

15.     Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza azma hii ya Ilani, Wizara kupitia Mfuko wa Maendeleo wa Wanawake ilizipatia halmashauri 62 mikopo yenye jumla ya shilingi milioni 612 kwa ajili ya kuwakopesha wanawake katika maeneo yao ili kuwaendeleza kiuchumi.  Halmshauri zilipatiwa mikopo kupitia Mfuko huu katika kipindi cha kuanzia mwaka 2010/11 hadi 2013/14.

16.     Mheshimiwa Spika, Serikali pia iliendelea kuiwezesha Benki ya Wanawake Tanzania ili kuwafikia wananchi wengi zaidi hususan wanawake.  Katika kipindi cha Januari 2011 hadi Machi, 2014  Benki ilitoa mikopo yenye thamani ya shilingi 24,392,382,000 kwa wananchi 11,754, kati ya hao wanawake ni asilimia 88.

       III.    Elimu ya Juu

17.     Mheshimiwa Spika, Ilani ya CCM ya mwaka 2010 Ibara ya 85 (e) imeelekeza Serikali kuongeza udahili kwa wanafunzi katika vyuo vya elimu ya juu. Wizara kupitia Chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru iliendelea kudahili wanafunzi katika ngazi ya shahada ya kwanza katika fani za Upangaji na Usimamizi Shirikishi wa Miradi, Maendeleo ya Jamii, Maendeleo ya Jinsia na Stashahada ya Uzamili ya Maendeleo ya Jamii. Jumla ya wanachuo 546 wakiwemo wanawake 324 na wanaume 222 walidahiliwa kati ya Septemba, 2011 hadi Septemba, 2013.

18.       Mheshimiwa Spika, pamoja na kutoa mafunzo ya elimu ya juu, Wizara iliendelea kutoa mafunzo ya taaluma ya maendeleo ya jamii kupitia vyuo vinane vinavyotoa mafunzo katika ngazi ya Astashahada na Stashahada.  Vyuo hivyo ni Buhare, Missungwi, Rungemba, Uyole, Ruaha, Mlale, Mabughai na Monduli. Jumla ya wanachuo 11,368 wakiwemo wanawake 7,463 na wanaume 3,905walidahiliwa katika vyuo hivi kwa kipindi cha Septemba, 2011 hadi Septemba, 2013. Kati ya idadi hiyo, ngazi ya Stashahada ni 2,445 na  Astashahada ni wanachuo 8,923. Wahitimu katika fani hizi huajiriwa katika ngazi ya halmashauri na huwezesha jamii kutekeleza majukumu yao ya maendeleo kwa kutumia mbinu shirikishi na kuzingatia usawa wa kijinsia na haki za mtoto hivyo kuifanya jamii kuwa na maendeleo endelevu.

      IV.    Demokrasia na Madaraka ya Umma

19.     Mheshimiwa Spika, Ibara ya 188 (a) ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010, inaitaka Serikali kuhakikisha Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yanajishughulisha na majukumu yaliyoandikishwa kutekeleza na kwamba hayapati nafasi ya kujiendesha kinyume na malengo yao. Kwa kuzingatia agizo hili la Ilani, Wizara yangu imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa shughuli za Mashirika Yasiyo ya Kiserikali. Moja ya hatua hizo ni pamoja na kutoa elimu kwa wadau 11,674 kati ya Januari, 2011 na Machi, 2014 kuhusu Sera ya Taifa ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na Sheria ya NGOs Na.24 ya mwaka 2002 iliyorekebishwa mwaka 2005.

20.     Mheshimiwa Spika, elimu hiyo ilitolewa kupitia Ofisi ya Msajili wa NGOs na mikutano ya wadau iliyofanyika katika mikoa ya Morogoro, Mtwara, Njombe, Mwanza, Ruvuma, Lindi, Mbeya na Tanga. Jumla ya Wadau 560 walipata elimu hii ikiwa ni pamoja na Maafisa Maendeleo ya Jamii wa mikoa na wilaya 24, wawakilishi kutoka katika Mashirika Yasiyo ya Kiserikali 536 na wananchi mbalimbali. Lengo la kufanya hivyo ni kuziwezesha NGOs kufahamu wajibu wao na kujiendesha kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi. Aidha, kwa upande wa Maafisa Maendeleo ya Jamii wa ngazi ya wilaya na mikoa elimu hiyo imelenga kuwajengea uwezo wa kufuatilia shughuli za NGOs katika maeneo yao na kutoa taarifa kwa Wizara pindi wanapobaini mashirika hayo kujiendesha kinyume na masharti ya usajili wao.

21.     Mheshimiwa Spika, hatua nyingine ambazo Wizara yangu imechukua katika kutekeleza agizo hili la Ilani ni pamoja na kuwateua Maafisa Maendeleo ya Jamii kuwa wasajili wasaidizi na waratibu wa mashirika haya katika ngazi za wilaya na mkoa ili kufuatilia shughuli za mashirika hayo katika ngazi husika. Aidha, Wizara imekuwa ikifuatilia na kutathmini utendaji na uendeshaji wa NGOs nchini ambapo kwa kipindi cha Januari, 2011 na Machi, 2014, NGOs 55 zilitembelewa na kukaguliwa katika maeneo yao ya utekelezaji. Aidha, taarifa za mwaka za fedha na kazi zilizowasilishwa kutoka kwa mashirika 1,000 zilifanyiwa uchambuzi. Kutokana na ufuatiliaji na tathmini ya shughuli za NGOs, shirika moja lilibainika kujiendesha kinyume cha taratibu na kufutiwa usajili wake. Aidha, ilibainika kuwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali mengi yameendelea kutoa mchango mkubwa katika huduma za kijamii na masuala ya kisera.

22.     Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio yaliyofikiwa katika utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2010, Wizara yangu ilikabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo ni pamoja na:
   (i)        Uhaba wa wakufunzi wa kada mbalimbali katika Vyuo vya Maendeleo ya Jamii na Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi;
  (ii)        Upungufu wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia katika Vyuo tisa vya Maendeleo ya Jamii na Vyuo 55 vya Maendeleo ya Wananchi;
(iii)        Mahitaji ya mikopo ya Mfuko wa Maendeleo wa Wanawake ni mengi ikilinganishwa na fedha zinazotolewa. Aidha, mikopo inayotolewa kwa vikundi ni midogo isiyokidhi mahitaji halisi ya biashara na mafunzo ya ujasiriamali yanayotolewa kwa wakopaji kutotosheleza kuwajengea uwezo unaohitajika;
(iv)        Kutokuwepo kwa uwazi na uwajibikaji kwa baadhi ya Mashirika Yasiyo ya  Kiserikali.


C:     HALI HALISI YA SEKTA YA MAENDELEO YA JAMII NA CHANGAMOTO ZILIZOPO

23.     Mheshimiwa Spika, Sekta ya maendeleo ya jamii hapa nchini imeendelea kukua na kutambulika na wadau mbalimbali kutokana na mchango wake katika maendeleo ya taifa letu. Naomba kuchukua fursa hii kueleza kwa kifupi hali halisi ya sekta hii katika maeneo ya ushiriki wa wananchi katika maendeleo ya kiuchumi, maendeleo ya jinsia, maendeleo ya watoto na ushiriki wa mashirika yasiyo ya kiserikali katika maendeleo nchini Tanzania.

Hali ya Ushiriki wa Wananchi katika Maendeleo

24.     Mheshimiwa Spika, maendeleo ya jamii kama dhana ni hatua mbalimbali zinazowawezesha watu kutambua uwezo walio nao wa kubaini matatizo yao na kutumia fursa na rasilimali zilizopo ili kuondokana na ujinga, maradhi, njaa na umaskini kwa ujumla na hivyo kujiletea maisha bora. Msisitizo wa dhana hii ni ushiriki wa watu katika kuamua, kupanga na kutekeleza mambo yote yanayohusiana na maisha yao na nchi yao.  Wataalamu wa  Maendeleo ya Jamii ni mhimili muhimu kwa jamii katika kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo kwani ndiyo wenye jukumu la kushauri, kushawishi, kuelimisha, kuhamasisha na kuraghabisha  wananchi kujiletea maendeleo kwa kutumia mbinu shirikishi katika programu mbalimbali wanazoibua na kubuni. Hivyo, wataalamu hao ni muhimu katika kuiwezesha jamii kuleta mabadiliko chanya kwa kushiriki katika masuala mbalimbali ya maendeleo.

25.     Mheshimiwa Spika, Wataalamu wa maendeleo ya jamii hufanya kazi katika ngazi mbalimbali ikiwa ni pamoja na wizara,  wakala na mamlaka za Serikali, Sekretariat za mikoa, halmashauri za miji, wilaya, manispaa na majiji, miji, kata na vijiji. Wataalamu hao pia hufanya kazi na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na taasisi mbalimbali za sekta binafsi. Mfano, katika ngazi za halmashauri takwimu zinaonesha kuwa kuna wataalamu wa maendeleo ya jamii 2,675 ambapo 1,381 hufanya kazi katika makao makuu ya halmashauri na 1,294  hufanya kazi katika Kata. Aidha, katika ngazi ya Sekretariat za mikoa kuna jumla ya wataalamu 21. Wataalamu hawa hutoa mchango mkubwa sana wa kuwaandaa wananchi kupokea na kutekeleza programu mbalimbali za huduma kama za afya, elimu, maji, nishati na miradi mingine ya kiuchumi na kijamii.

26.       Mheshimiwa Spika, Sera ya  Maendeleo ya Jamii ya mwaka 1996 inasisitiza  kuwepo kwa mtaalamu mmoja kwa kila Kata hivyo mahitaji halisi ya wataalamu hao kwa ngazi husika ni 3,339. Kwa takwimu hizo upungufu wa wataalamu kwenye kata ni 2,045 sawa na asilimia 61 ya mahitaji. Aidha, katika ngazi ya Sekretariati za mkoa upungufu wa wataalamu hao ni asilimia 16. Hali hii inaathiri kwa kiasi kikubwa utekelezaji wa  shughuli za Sekta ya Maendeleo ya Jamii. Katika kukabiliana na changamoto hii, Wizara yangu imeendelea kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu –TAMISEMI kuhakikisha halmashauri zote  zinaajiri wataalamu wa maendeleo ya jamii katika ngazi ya Kata.

27.       Mheshimiwa Spika, Wizara inaendelea kutoa mafunzo na kuzalisha wataalamu wa Maendeleo ya Jamii kupitia vyuo tisa vya maendeleo ya jamii nchini. Katika kipindi cha mwaka 2011/2012 hadi mwaka 2013/2014  jumla ya wanachuo 11,914 walidahiliwa katika vyuo hivyo. Idadi hii kubwa ni matokeo ya utekelezaji wa mipango mbalimbali ya kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia ikiwemo ujenzi na ukarabati wa majengo na miundombinu ya vyuo hivyo.

28.       Mheshimiwa Spika, wananchi wameendelea kunufaika na mafunzo yanayotolewa na Vyuo 55 vya Maendeleo ya Wananchi vilivyo chini ya Wizara yangu. Idadi ya wananchi wanaodailiwa katika vyuo hivyo imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka. Mfano, kati ya  mwaka 2010/2011 na mwaka 2013/2014 idadi ya wananchi waliodahiliwa kwa mafunzo ya muda mrefu na muda mfupi iliongezeka kutoka 32,133 hadi kufikia 40,692. Aidha, baadhi ya wananchi walipata maarifa na ujuzi kupitia mafunzo nje ya chuo (outreach courses). Mafunzo hayo yanawawezesha washiriki kujiajiri na kuajiriwa katika taasisi mbalimbali. Napenda kuliarifu Bunge lako tukufu kuwa Vyuo hivi kwa miaka ya hivi karibuni vimeanza kupokea vijana wengi waliohitimu mafunzo ya sekondari sambamba na wale wa elimu ya msingi.

Hali ya Maendeleo ya Jinsia

29.     Mheshimiwa Spika, hali ya usawa wa kijinsia katika nyanja mbalimbali hapa nchni imeendelea kuimarika. Ukweli huu unadhihirishwa na ushahidi wa kitakwimu na taarifa zilizopo katika maeneo ya ushiriki wa wanawake katika siasa na ngazi za maamuzi; uwezeshaji wa wanawake kiuchumi; elimu, mafunzo na ajira; kuongezeka kwa wanawake wajasiriamali (wadogo na wakati) na upatikanaji wa haki za wanawake kisheria.

30.     Mheshimiwa Spika, kwa upande wa ushiriki wa wanawake katika ngazi za siasa na maamuzi, idadi ya mawaziri wanawake imeongezeka kutoka asilimia 15 mwaka 2005 hadi asilimia 30 mwaka 2013, wakuu wa mikoa wanawake kutoka asilimia 10 mwaka 2005 hadi asilimia 24 mwaka 2013.  Majaji wanawake pia wameongezeka kutoka asilimia  33  hadi  61  kwa kipindi hicho na uwakilishi wa wanawake Bungeni umeongezeka kutoka asilimia 30.3 mwaka 2005 na kufikia asilimia 36 ya wabunge wote mwaka 2013.

31.     Mheshimiwa Spika, katika uwezeshaji wanawake kiuchumi taasisi za fedha na mifuko mbalimbali vimeendelea kutoa mikopo ya fedha na mafunzo ya ujasiriamali kwa wanawake. Baadhi ya taasisi na mifuko hiyo ni pamoja na Mfuko wa Maendeleo wa Wanawake, Benki ya Wanawake Tanzania, Women Convenant Bank, VICOBA na SACCOS. Mfano, Mfuko wa Maendeleo wa Wanawake umetoa mikopo yenye thamani ya shilingi milioni 705 kwa kipindi cha kati ya mwaka 2011/12 na  mwaka 2013/14.

32.     Mheshimiwa Spika, Mila na desturi kandamizi bado ni changamoto katika kuhakikisha kuwa kunakuwepo na usawa wa kijinsia kwa kuzingatia haki na usawa wa binadamu.  Mila zinazoleta madhara kwa wanawake na hasa watoto wa kike kama kukeketwa na kuozesha wasichana wa kike katika umri mdogo zimeendelea na bado ni changamoto katika maeneo kadhaa ya nchi yetu. Wizara inachukua hatua mbalimbali kupambana na changamoto hizi ambazo ni pamoja na kutoa elimu kwa kushirikiana na wadau hasa NGOs na washirika wa maendeleo na kuiwezesha Kamati ya Kitaifa ya Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake ili iweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

Hali ya Maendeleo ya Watoto

33.     Mheshimiwa Spika, Watoto ni sehemu muhimu ya jamii na ndiyo tegemeo ya Taifa lolote.  Watoto wanahitaji kukua na kuwa raia wema, hivyo wanatakiwa kupewa haki na mahitaji yao ya msingi ikiwa ni pamoja na: kuishi, kupewa malezi stahiki, kulindwa, kuendelezwa kiakili kwa kutambua na kukuza vipaji vyao, kutobaguliwa na kushirikishwa.


34.     Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa takwimu za Sensa ya Taifa ya Idadi ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, idadi ya watoto chini ya miaka 18 Tanzania Bara ni 21,866,258 sawa na asilimia 50.1 ya idadi ya watu wote.  Kati yao wasichana ni 10,943,846 na wavulana ni 10,922,412.

35.     Mheshimiwa Spika, Pamoja na Serikali kuweka mazingira wezeshi ya kuwapatia watoto haki zao kupitia sera,sheria, mipango, programu na mikakati mbalimbali, bado maendeleo ya mtoto yanakabiliwa na changamoto mbalimbali.  Changamoto hizo ni pamoja na: ukatili dhidi ya watoto, kuwepo kwa watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi, kushuka kwa maadili, ndoa na mimba za utotoni. 

36.     Mheshimiwa Spika, Kumekuwepo na jitihada mbalimbali za kukabiliana na changamoto hizo ikiwa ni pamoja na uanzishwaji wa Kituo cha Huduma za Pamoja (One Stop Centre) kwa majaribio katika Hospitali ya Amana - Manispaa ya Ilala kwa ajili ya kuhudumia watoto mbalimbali wanaofanyiwa aina mbalimbali za ukatili na kutoa elimu kwa wazazi na walezi juu ya wajibu wao katika malezi ya watoto.  Aidha, Wizara kwa kushirikiana na wadau imewezesha kuanzishwa kwa mtandao wa mawasiliano wa kusaidia  watoto (Child Helpline) namba 116 kwa ajili ya jamii inayotumika kutoa taarifa za ukatili dhidi ya watoto na ukiukwaji wa haki za watoto. Namba hii imeanza kufanya kazi katika maeneo machache kwa majaribio na utekelezaji wa kazi zake unaonesha mafanikio mazuri hadi sasa.


Hali ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali

37.     Mheshimiwa Spika, idadi ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali chini ya Sheria ya NGOs Na. 24 ya mwaka 2002 iliyorekebishwa mwaka 2005 imeendelea kukua mwaka hadi mwaka.  Kufikia tarehe 17 Machi, 2014 idadi ya mashirika hayo ilifikia 6,427 kutoka mashirika 3,000 yaliyokadiriwa kuwepo mwaka 2001 wakati Sera ya Taifa ya NGOs ilipokuwa inaandaliwa. Hili ni ongezeko la zaidi ya asilimia 100. Kati ya mashirika yaliyosajiliwa, 254 ni ya kimataifa na 6,173 ni ya ndani ya nchi yanayofanya kazi katika ngazi za wilaya, mkoa na taifa.

38.     Mheshimiwa Spika, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yameendelea kutambulika kama wadau na wabia muhimu katika maendeleo. Mashirika haya yanajishughulisha na kazi mbalimbali ikiwemo elimu, mazingira na mabadiliko ya tabianchi, afya, maendeleo shirikishi, haki za binadamu, maendeleo ya jinsia, ushawishi na utetezi, kinga ya jamii, haki za watoto, kilimo, maji na ustawi wa jamii.

39.     Mheshimiwa Spika, kuongezeka kwa idadi na shughuli za NGOs katika nchi yetu ni matokeo ya mazingira wezeshi yanayoendelea kuboreka mwaka hadi mwaka. Hii ni pamoja na uwepo wa Sera ya Taifa ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ya mwaka 2001, Sheria ya NGOs Na.24 ya mwaka 2002 iliyorekebishwa mwaka 2005 na Kanuni za Maadili za Mashirika Yasiyo ya Kiserikali za mwaka 2008. Aidha, muundo wa kitaasisi unaowezesha NGOs kujitawala kwa uhuru na kujiratibu umeendelea kuwepo ikiwemo:  Bodi ya Uratibu wa NGOs, Baraza la Taifa la NGOs, Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya na mikoa ambao ni Wasajili Wasaidizi na mitandao ya NGOs ya wilaya, mkoa na  taifa. 

40.     Mheshimiwa Spika, pamoja na kuimarika kwa hali ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali hapa nchini, bado kuna changamoto zinazohitaji kufanyiwa kazi. Changamoto zilizopo ni pamoja na sehemu kubwa ya shughuli za Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kutegemea wafadhili kutoka nje na kutokuwa na vyanzo vya uhakika vya ndani ya nchi hivyo kuathiri uendelevu wa shughuli hizo pindi wafadhili hao wanapositisha misaada. Changamoto nyingine ni kutokuwepo kwa Kamati za Maadili ya NGOs katika baadhi ya mikoa na wilaya kunakoathiri uwezo wa NGOs kujitawala katika kuongeza uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya rasilimali na uendeshaji wa mashirika hayo.

41.     Mheshimiwa Spika, katika kutatua changamoto hizo wizara yangu imechukua hatua mbalimbali. Mojawapo ya hatua hizo ni kuhimiza Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kutumia fursa ya marekebisho ya Sheria ya NGOs yaliyofanyika mwaka 2005 kuanzisha na kuendeleza miradi ya kuzalisha faida kwa ajili ya kutekeleza malengo yao hata pale wafadhili wanapositisha misaada. Aidha, Wizara kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la NGOs inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuliwezesha kuanzisha Kamati za Maadili ya NGOs katika ngazi ya wilaya na mikoa ikiwa ni utekelezaji wa Kanuni za Maadili ya NGOs.

Mafanikio


42.     Mheshimiwa Spika, mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2013/2014, ni pamoja na:
(i)         Idadi ya vituo vya kutolea mikopo kwa wajasiriamali wadogo hususan wanawake imeongezeka  toka vituo  21 mwaka 2012/13 hadi vituo  50 mwaka 2013/14, sawa na ongezeko la asilimia 58;
(ii)        Matawi ya Benki ya Wanawake Tanzania yameongezeka toka tawi moja mwaka 2009/10 hadi matawi mawili mwaka 2013/14;
(iii)      Kuongezeka kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yaliyosajiliwa toka mashirika 3,000 mwaka 2001/02 hadi mashirika 6,427  mwaka 2013/14;
(iv)       Wanafunzi waliojiunga na mafunzo ya ufundi stadi katika Vyuo 25 vya Maendeleo ya Wananchi wameongezeka toka wanafunzi 1,125 mwaka 2013 hadi wanafunzi 2,722 mwaka 2014;
(v)        Wanafunzi waliojiunga na mafunzo ya elimu ya wananchi (Kozi ndefu) katika Vyuo 55 vya Maendeleo ya Wananchi wameongezeka toka wanafunzi 6,586 mwaka 2013 hadi wanafunzi 7,144 mwaka 2014;
(vi)       Kuongezeka kwa Halmashauri  zilizopata mikopo  kupitia Mfuko wa Maendeleo wa Wanawake toka Halmashauri 19 mwaka 2008/09 hadi Halmashauri 38 mwaka 2013/14; na
(vii)     Kuongezeka kwa Madawati ya Jinsia na Watoto toka madawati 9 mwaka 2008 hadi madawati 417 mwaka 2014.

Changamoto


43.     Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio yaliyopatikana, Sekta ya Maendeleo ya Jamii inakabiliwa na changamoto zifuatazo:
(i)         Uhaba wa wakufunzi wa kada mbalimbali katika Vyuo vya Maendeleo ya          Jamii na Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi;
(ii)        Ukosefu wa vyombo vya usafiri katika Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi, Vyuo vya Maendeleo ya Jamii na uchakavu wa vyombo vya usafiri Makao Makuu ya Wizara; 
(iii)      Upungufu wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia katika Vyuo tisa vya Maendeleo ya Jamii na Vyuo 55 vya Maendeleo ya Wananchi;
(iv)       Uchakavu wa majengo na miundombinu katika Vyuo vya Maendeleo ya Jamii na Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi;
(v)        Kuendelea kukua kwa madeni ya watumishi, wakandarasi na watoa huduma mbalimbali Wizarani. Madeni yamefikia shilingi 2,558,735,065 katika deni hilo shilingi 774,308,379.84 ni madeni ya watumishi, shilingi 773,166,431.80 ni madeni ya wazabuni na shilingi 1,011,260,253.36 ni madeni ya wakandarasi;
(vi)       Fedha kutolewa na Wizara ya Fedha bila kuzingatia Mpango Kazi na Mtiririko wa Mahitaji ya Fedha;
(vii)     Mahitaji ya mikopo ya Mfuko wa Maendeleo wa Wanawake ni mengi ikilinganishwa na fedha zinazotolewa. Aidha, mikopo inayotolewa kwa vikundi kuwa kidogo isiyokidhi mahitaji halisi ya biashara na mafunzo ya ujasiriamali yanayotolewa kwa wakopaji kutotosheleza kuwajengea uwezo unaohitajika;
(viii)   Kupanua huduma za Benki ya Wanawake Tanzania ili kuwafikia wanawake wengi zaidi; na
(ix)      Kutokuwepo kwa uwazi na uwajibikaji kwa baadhi ya Mashirika Yasiyo ya  Kiserikali.
(x)        Kuongezeka kwa matukio ya ukatili wa kijinsia katika jamii.

D:     MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA MPANGO WA MWAKA 2013/14 NA MALENGO YA MWAKA 2014/15

44.     Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/14, Wizara yangu iliendelea kusimamia utekelezaji wa majukumu yake kulingana na malengo yaliyopangwa. Katika bajeti ya mwaka 2013/14, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto iliidhinishiwa jumla ya shilingi 25,964,170,000 kwa ajili ya matumizi ya Kawaida na Maendeleo. Kati ya fedha za matumizi ya kawaida, shilingi 5,397,496,000 ni kwa ajili ya matumizi mengineyo na shilingi 8,656,002,000 kwa ajili ya malipo ya mishahara na shilingi 11,910,672,000 ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.

45.     Mheshimiwa Spika, hadi kufikia tarehe 15 Mei, 2014, Wizara ilikuwa imetumia jumla ya shilingi 10,305,162,100 sawa na asilimia 100 ya fedha za Matumizi ya Kawaida zilizopokelewa na shilingi 2,923,620,590 sawa na asilimia 100 ya fedha za Maendeleo zilizotolewa.

46.     Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha utekelezaji wa mpango wa  mwaka 2013/14 na malengo ya mwaka 2014/15 kwa kuzingatia maeneo yafuatayo:

Maendeleo ya Jamii

47.     Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha 2013/2014 Wizara yangu ilidahili na kutoa mafunzo kwa wanachuo 2,869 kupitia vyuo tisa vya Maendeleo ya Jamii vya Tengeru, Buhare, Rungemba, Monduli, Missungwi, Ruaha, Uyole, Mlale na Mabughai. Wanachuo 2,036 walidailiwa katika ngazi ya cheti, 591 katika ngazi ya stashahada, 234 ngazi ya shahada na 8 katika ngazi ya Stashahada ya Uzamili. Aidha, Wizara yangu ilikarabati majengo na miundombinu katika Chuo cha Maendeleo ya Jamii Mlale, Misungwi na Mabughai. Katika mwaka 2014/2015, Wizara yangu itaendelea kukamilisha jengo la maktaba ya Chuo cha Tengeru na maabara ya kompyuta katika chuo cha Mabughai kwa lengo la kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia.

48.     Mheshimiwa Spika, Katika mwaka 2013/14 Wizara yangu ililipa shilingi 84,114,523 zikiwa ni gharama za ujenzi zilizoongezeka katika ujenzi wa bwalo, jiko na nyumba za watumishi katika vyuo vya Maendeleo ya Wananchi vya Mputa na Muhukuru mkoani Ruvuma.  Aidha, Wizara ilifanya ukarabati wa mabweni na jengo la utawala katika chuo cha Maendeleo ya Wananchi Tarime; ukarabati wa nyumba za watumishi na uwekaji wa mfumo wa umeme katika chuo cha Maendeleo ya Wananchi Mwanhala; ukarabati wa jengo la utawala na bweni katika chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kilwa Masoko; ukarabati wa mabweni na nyumba za watumishi katika chuo cha Maendeleo ya Wananchi Msaginya, Mputa, Sofi na Singida; ujenzi wa vyoo katika chuo cha Maendeleo ya Wananchi Masasi na Chilala; na kuvipatia vyuo vya Maendeleo ya Wananchi 25 vifaa vya kujifunzia na kufundishia masomo ya ufundi stadi.

49.      Katika mwaka 2014/2015 Wizara yangu itaendelea kudahili na kutoa mafunzo kwa wananchi na pia itakarabati majengo na miundombinu ya vyuo vya Maendeleo ya Wananchi vya Mto wa Mbu, Msaginya na Nandembo.

50.      Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuboresha mafunzo ya maendeleo ya wananchi kwa kutoa huduma kwa watoto kupitia vituo vya kulelea watoto ndani ya vyuo vya Maendeleo ya Wananchi 55 ambapo jumla ya watoto 1,033 walinufaika. Kuwepo kwa vituo hivi katika vyuo vya Maendeleo ya Wananchi kumewawezesha watumishi katika vyuo hivi na jamii inayovizunguka vyuo hususan wanawake kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali kwa uhuru zaidi. Aidha, vituo hivi vimewawezesha washiriki wanawake 97 wenye watoto wadogo kupata mafunzo wakiwa na watoto wao vyuoni. 

51.     Mheshimiwa Spika, kwa kipindi cha mwaka 2014/15, Wizara itaendelea kuimarisha vituo vya kulelea watoto katika vyuo 55 vya maendeleo ya wananchi kwa kutoa vifaa vya kufundishia na kujifunzia na kutengeneza viwanja vya michezo. Aidha, Wizara itawajengea uwezo wakufunzi 30 kwa ajili ya kuwawezesha kupata elimu ya kuendesha vituo vya kulelea watoto wadogo ikiwa ni pamoja na kuwapatia ujuzi wa kufundisha watoto hao elimu ya awali. Mafunzo ya kuwajengea uwezo wakufunzi katika Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi yatakuwa yanatolewa kwa awamu kulingana na Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Elimu.

Maendeleo ya Jinsia

52.     Mheshimiwa Spika, uwezeshaji wanawake kiuchumi ni suala muhimu katika kufikia usawa wa kijinsia na kupunguza umaskini wa kipato katika jamii. Katika mwaka 2013/14, Wizara kupitia Mfuko wa Maendeleo wa Wanawake iliziwezesha Halmashauri 39 kutoa mikopo yenye thamani ya shillingi milioni 428. Katika kuhakikisha Mfuko unafikia malengo yaliyopangwa, Wizara ilifuatilia utendaji wa Mfuko katika mikoa tisa na kuiwezesha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii kufuatilia utekelezaji wa Mfuko katika Halmashauri mbalimbali. Halmashauri ambazo Kamati ya Bunge ilifanya ufuatiliaji huo ni Kinondoni, Ilala, Kibaha, Korogwe na Jiji la Tanga. Mikoa ambayo Wizara ilifuatilia shughuli za Mfuko ni Arusha, Manyara, Singida, Pwani, Tanga, Katavi, Rukwa, Morogoro na Kagera. Matokeo ya ufuatiliaji yanaonesha kwamba Halmashauri nyingi hazichangii asilimia tano ya mapato yao kama inavyotakiwa. Kutokana na matokeo hayo, Halmashauri ziliagizwa kuchangia katika Mfuko huo.

53.     Mheshimiwa Spika,   katika mwaka 2014/2015, Wizara yangu itaendelea kutoa fedha kwa Halmashauri nyingine zitakazokuwa zimemaliza marejesho pamoja na kufanya ufuatiliaji kwa mikoa na halmashauri zilizobaki. Napenda kutumia fursa hii kuzikumbusha halmashauri zote zilizokopeshwa kuzingatia mkataba wa marejesho. Aidha, nazikumbusha halmashauri zote nchini kuchangia asilimia tano ya mapato yao kwenye Mfuko wa Maendeleo wa wanawake ili wanawake wengi zaidi wanufaike na huduma za Mfuko huu.

54.      Mheshimiwa Spika, kupitia Benki ya Wanawake Tanzania  huduma za kibenki zimewafikia wananchi wengi zaidi wakiwepo wanawake kwani imeweza kufungua tawi la pili   la Benki ya Wanawake Tanzania eneo la Kariakoo Mkoa wa Dar es Salaam,  Mtaa wa Agrey/Likoma.  Aidha, vituo 29 vya kutolea mikopo na mafunzo kwa wajasiriamali vimefunguliwa katika Mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma na Mwanza. Vituo hivyo ni  kama ifuatavyo: Dar es Salaam (Tabata Kisukuru, Mbande, Sabasaba, Ubungo Kibangu, Chanika, Chamazi na Kunduchi Mtongani); Dodoma (Airport, Chamwino, Ipagala, Posta, Hazina Kikuyu, Kizota, Savanna Kikuyu,  Chang’ombe, Mnadani, Veyula, Mpwapwa, Kongwa na Mbande); na Mwanza (Nyakato, Igogo, Nyegezi, Pansiansi, Igoma, Kisesa, Magu, Misungwi na Kitangiri). Kwa mwaka 2014/15, Wizara yangu itaendelea kutoa ruzuku kwa Benki ya Wanawake Tanzania ili iweze kuwafikia wananchi wengi zaidi.

55.     Mheshimiwa Spika, Ukatili wa kijinsia umeendelea kuwa ni tatizo katika jamii zetu ambapo wananchi wengi wameendelea kuumizwa na kuteseka na hata kuuawa kutokana na vitendo vya kikatili vinavyofanyika hapa nchini.  Mwaka 2013/2014, Wizara ilifanya tathmini ya mafunzo yaliyotolewa kwa Kamati za Ulinzi na usalama katika Mkoa wa Manyara kuhusiana na kupiga vita ukatili wa kijinsia. Moja ya matokeo ya tathmini hiyo imeonyesha kuwa Kamati husika zinahitaji kujengewa uwezo zaidi ili ziweze kufanya kazi zake kikamilifu. Katika mwaka 2014/15, Wizara itaendelea kufanya tathmini ya mafunzo yaliyotolewa kwa Kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya kuhusu mbinu za kutokomeza ukatili katika mikoa ya Mwanza, Shinyanga na Mara. Aidha, itaendelea kuzijengea uwezo kamati za ulinzi na usalama  ili ziweze kupambana na kutokomeza ukatili katika ngazi ya wilaya na kuendelea kuiwezesha  Kamati ya Kitaifa ya Kuzuia na Kuondoa Ukatili Dhidi ya Wanawake na  Watoto ili iweze kutekeleza shughuli zake kikamilifu.

56.     Mheshimiwa Spika, suala la uingizaji wa masuala ya kijinsia katika sera, mipango na bajeti limekuwa likitiliwa mkazo ili kuhakikisha kuwa mipango na bajeti za kila sekta, idara na taasisi mbalimbali inawanufaisha wote, yaani wanawake, wanaume, wavulana na wasichana. Katika kipindi cha mwaka 2013/14, Wizara kupitia wataalamu wake ilifanya tathmini ya uingizaji wa masuala ya jinsia katika Halmashauri 6 ambazo ni Halmashauri ya Jiji la Tanga na Arusha, Halmashauri za Wilaya ya Iringa na Moshi pamoja na Manispaa ya Temeke na Morogoro.  Lengo la tathmini ilikuwa ni kubaini mafanikio na changamoto zinazojitokeza katika uingizaji wa masuala ya jinsia katika sera na mipango na bajeti mbalimbali.  Katika mwaka 2014/15, Wizara itaendelea kutoa mafunzo ya uingizaji wa masuala ya jinsia kwa wataalamu mbalimbali ili waweze kuelewa na kutekeleza mkakati huu ikiwa ni pamoja na kukamilisha Sera ya Taifa ya Jinsia. Aidha, Wizara imeanza mchakato wa kuandaa taarifa ya hali ya jinsia nchini (Tanzania Country Gender Profile) na kuanzisha benki ya Takwimu ya usawa wa jinsia. Taarifa hii na Benki ya Takwimu zitawezesha kufanya maamuzi, upangaji wa mipango, ushawishi na uhamasishaji kuhusu masuala ya jinsia ili kuwa na maendeleo endelevu. Aidha, zitasaidia kupima utekelezaji wa mipango na programu mbalimbali kuona kama zinaweza kupunguza changamoto za kijinsia na kuleta usawa unaotarajiwa.

57.     Mheshimiwa Spika, mwaka 2013/2014, Wizara iliandaa rasimu ya 7 na 8 ya nchi ya Mkataba wa Kuondoa Aina zote za Ubaguzi dhidi ya Wanawake. Maandalizi ya taarifa hiyo yaliwashirikisha wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na Watendaji wa Madawati ya Jinsia kutoka Wizara mbalimbali, asasi za kijamii na Maafisa wa Maendeleo Jamii. Rasimu ya Taarifa hiyo imekamilika na inatarajiwa kujadiliwa na wadau mbalimbali wakiwemo Kamati ya Bunge ya Sekta ya Maendeleo ya Jamii kwa lengo la kupata maoni zaidi kwa ajili ya kuiboresha.

58.     Mheshimiwa Spikatarehe 8 Machi kila mwaka, Wizara imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali kuratibu maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani. Kwa mwaka 2013/2014, maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yalifanyika kimkoa ambapo lengo kuu lilikuwa ni kuwakutanisha wanawake wa ngazi zote ili waweze kubadilishana uzoefu wa masuala mbalimbali yanayowakabili, kubaini fursa zilizopo katika kujiletea maendeleo na kutafuta ufumbuzi wa changamoto mbalimbali zinazowakabili.  Katika mwaka 2013/14, Wizara yangu iliratibu maadhimisho ya siku hiyo katika ngazi ya mikoa ambapo Kauli mbiu ilikuwa ni “Chochea Mabadiliko Kuleta Usawa wa Kijinsia” Kauli mbiu hii inasisitiza na kuhamasisha jamii juu ya umuhimu wa kuzingatia masuala ya jinsia katika kupanga na kutekeleza mikakati na mipango ya maendeleo kwa kuzingatia ushiriki stahiki wa wanawake, wanaume, wavulana na wasichana katika kujiletea maendeleo yao na taifa kwa ujumla. Kwa mwaka 2014/15, Wizara itaratibu maadhimisho haya Kitaifa ili kuweza kupima mafanikio yaliyopatikana katika miaka mitano (2010 – 2015) katika juhudi za kumwendeleza mwanamke pamoja na kubainisha changamoto zilizojitokeza kwa kipindi hicho toka maadhimisho haya yalipofanyika kitaifa mwaka 2010.

59.     Mheshimiwa Spika, ili kutekeleza mikataba na maazimio mbalimbali ambayo nchi imesaini na kuridhia, mwaka 2013/14, Wizara ilishiriki katika mkutano wa 58 wa Kamisheni ya Hali ya Wanawake na mkutano wa nchi za Maziwa Makuu kuhusu masuala ya jinsia. Lengo la mikutano hiyo ni kutafuta mbinu za pamoja za kukabiliana na changamoto mbalimbali, kubadilishana uzoefu na kukubaliana maeneo muhimu ya utekelezaji katika kuleta usawa wa kijinsia na maendeleo ya wanawake katika nchi husika. Katika mwaka 2014/15, Wizara itaendelea kushiriki na kutoa mchango wake katika mikutano ya kikanda na kimataifa kuhusu utekelezaji wa masuala ya usawa wa kijinsia na kuwaendeleza wanawake.

Maendeleo ya Watoto

60.     Mheshimiwa Spika, maendeleo ya taifa lolote duniani hutegemea sana namna ambavyo linawalinda na kuwakuza watoto wake. Kwa kuzingatia hilo, Wizara yangu imekuwa ikichukua hatua mbalimbali katika kukabiliana na changamoto zinazowakabili watoto hapa nchini.

61.     Mheshimiwa Spika, mwaka 2013/2014, Wizara yangu iliandaa mpango kazi wa jamii wa kudhibiti tatizo la watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani. Lengo likiwa ni kuongeza ushiriki wa wadau katika kudhibiti na kuondoa tatizo hilo kwa kuwaelimisha na kuhamasisha ili wabebe jukumu la kuwapatia watoto mahitaji na haki zao za msingi. Utekelezaji wa Mpango kazi unahusisha familia, jamii, serikali, asasi za kiraia, vyombo vya habari na wabia wa maendeleo. Katika mwaka 2014/2015, Wizara itasambaza mpango katika mikoa yote na kuratibu utekelezaji wake.

62.     Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Wizara yangu imefanya marekebisho ya Sera ya Maendeleo ya Mtoto ya mwaka 2008 kuwa Sera ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Mtoto ya mwaka 2014 ili iweze kujumuisha masuala ya utoaji huduma fungamanishi na shirikishi za Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Mtoto. Aidha, Sera hiyo imezingatia masuala ya kukabiliana na changamoto zinazotokana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia pamoja na upatikanaji wa huduma za malezi na makuzi kwa watoto walio chini ya umri wa miaka nane. Katika mwaka 2014/2015, Wizara itakamilisha Sera hiyo na mkakati wake wa utekelezaji. Aidha, Wizara itasambaza kwa wadau sera na mkakati huo kwa ajili ya utekelezaji.
63.     Mheshimiwa Spika, ukatili dhidi ya watoto ni moja ya changamoto zinazoathiri malezi, makuzi na maendeleo ya mtoto. Katika kupunguza matukio ya ukatili huo, mwaka 2013/2014 Wizara yangu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali iliandaa Mpango Kazi Shirikishi wa Kuzuia Ukatili dhidi ya Watoto wa mwaka 2013 hadi 2016.  Aidha, Wizara yangu iliwezesha kufanyika kwa mkutano wa mwaka wa Kikosi Kazi cha Taifa cha Kuzuia Ukatili dhidi ya Mtoto ambapo sekta zote zinazohusiana na maendeleo ya mtoto zilitoa taarifa kuhusu mapendekezo ya namna ya kutekeleza mpango huo. Pia, Wizara iliandaa mkutano uliowakutanisha watekelezaji wa Mpangokazi wa miaka mitatu wa kuzuia ukatili wa watoto na wadau wa maendeleo na tayari wadau kadhaa wa maendeleo wajitokeza na kuanza kuchangia fedha za utekelezaji wa baadhi ya kazi zilizoainishwa katika mpango huu. Tunawashukuru sana wadau hawa. Katika mwaka 2014/2015, Wizara itaendelea kuratibu na kusimamia mpango huo kwa kushirikiana na kikosi kazi hicho.

64.     Mheshimiwa Spika, Wizara yangu pia iliandaa kitini cha elimu ya malezi kwa familia kuhusu kukabiliana na ukatili dhidi ya watoto. Kitini hicho kitatumiwa na wawezeshaji jamii katika kuwajengea uwezo wazazi na walezi ili kudhibiti ukatili dhidi ya watoto.  Aidha, kuanzia ngazi ngazi ya familia Wizara ilitoa mafunzo kuhusu Kitini hicho kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii kutoka halmashauri za Hai, Temeke, Magu na Kasulu. Katika mwaka 2014/2015, Wizara itaendelea kuratibu usambazaji wa kitini hicho katika halmashauri nyingine.

65.     Mheshimiwa Spika, vilevile, Wizara iliendelea kuratibu utoaji wa taarifa za ukatili dhidi ya watoto kupitia namba ya simu 116 inayosimamiwa na Shirika Lisilo la Kiserikali la C-SEMA. Hadi kufikia Machi, 2014 jumla ya simu 6,188 zilipigwa kupitia namba hiyo na kufanyiwa kazi. Mwaka 2014/15, Wizara itaendelea kuratibu na kusimamia mtandao huo na kuendelea kutathmini ili kuwezesha kupeleka huduma hii katika maeneo mengine ya nchi.

66.     Mheshimiwa Spika, Watoto wanayo haki ya msingi ya kushiriki na kushirikishwa katika masuala yote yanayowahusu. Katika kuhakikisha ushiriki wa watoto katika kutoa maoni yao, mwaka 2013/2014, wizara iliandaa Mkutano Mkuu wa Baraza la Watoto ili kupitia rasimu ya kwanza ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aidha, wizara yangu iliratibu utekelezaji wa shughuli za mabaraza ya watoto katika ngazi ya Wilaya/Mikoa pamoja na Azimio la Bujumbura kuhusu haki na ustawi wa watoto.  Katika mwaka 2014/2015, Wizara itaendelea kushirikiana na Halmashauri kuimarisha Baraza la Watoto la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na mabaraza ya watoto ya mikoa na wilaya ili yaweze kutoa fursa nzuri za ushiriki wa watoto katika maeneo husika.

67.     Mheshimiwa Spika, Katika mwaka 2013/2014, Wizara yangu iliratibu maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika ambayo yaliadhimishwa katika ngazi ya mkoa. Katika maadhimisho hayo, kila mkoa ulipata fursa ya kuadhimisha siku hii muhimu kulingana na mazingira na uhitaji wa mkoa husika.  Kauli mbiu ya mwaka 2013/2014 ilikuwa ni “Kuondoa Mila zenye kuleta Madhara kwa Watoto: ni Jukumu Letu Sote”. Lengo la kaulimbiu hiyo ni kuhamasisha jamii kubaini baadhi ya mila ambazo zimekuwa zikileta madhara kwa watoto  na kuweka mikakati ya kuzitokomeza.

68.     Mheshimiwa Spika, Vile vile, Wizara yangu iliratibu maadhimisho ya siku ya Familia Duniani ambayo  yalifanyika kimkoa. Kauli mbiu ya maadhimisho haya ilikuwa ni “Imarisha na Endeleza Ushirikiano na Mshikamano wa Familia na Makundi Mbalimbali ya Jamii”.  Kauli mbiu hii inasisitiza wazazi, walezi na jamii kuwajibika kwa pamoja katika malezi ya familia.  Katika mwaka 2014/2015, Wizara itaendelea kuratibu maadhimisho ya siku hizo kwa lengo la kuhamasisha jamii kuhusu haki na ustawi wa mtoto na maendeleo ya familia.

Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali

69.     Mheshimiwa Spika, Katika kipindi cha mwaka 2013/2014, Serikali iliendelea kusajili Mashirika Yasiyo ya Kiserikali chini ya Sheria ya NGOs Na.24 ya mwaka 2002. Jumla ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali 435 yalipatiwa usajili katika ngazi ya wilaya, mkoa, taifa na kimataifa. Kati ya hayo, mashirika ya kimataifa ni 23 na mashirika ya ndani ya nchi yaani ya ngazi za wilaya, mkoa na taifa ni 412.  Hii imefanya idadi ya NGOs kuongezeka kutoka mashirika 5,992 mwezi Julai, 2013 na kufikia mashirika 6,427 mwezi Machi, 2014 ikiwa ni ongezeko la asilimia 7.  Aidha, katika kipindi cha mwaka 2014/15, Wizara yangu itaendelea na usajili wa mashirika hayo.

70.     Mheshimiwa Spika, Wizara yangu pia iliratibu shughuli za NGOs kwa kuwezesha ushiriki wa wadau katika utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali. Hii ni pamoja na kuiwezesha Bodi ya uratibu wa NGOs kukagua shughuli za NGOs 21 na kufanya vikao vitatu katika mikoa ya Tanga, Lindi na Mbeya. Vikao hivyo vilifikia maamuzi mbalimbali ikiwemo utatuzi wa migogoro katika Mashirika Yasiyo ya Kiserikali. Aidha, Wizara kupitia Bodi ya Uratibu wa NGOs ilikutana na wadau 175 na kujadili mafanikio na changamoto zinazozikabili NGOs katika mikoa husika na kutoa elimu kuhusa Sera ya Taifa ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ya mwaka 2001 na Sheria ya NGOs Na. 24 ya mwaka 2002.  Wizara pia imeanzisha utaratibu wa kukutana na NGOs zinazofanyakazi za watoto na wanawake na mapendekezo ya kuboresha ushirikiano yameandaliwa. Kwa mwaka 2014/15, Wizara yangu itaendelea kuiwezesha Bodi ya Uratibu wa NGOs kufanya vikao vinne na kukutana na wadau ili kuboresha uratibu wa NGOs nchini na pia itaendelea na utaratibu wa kukutana na NGOs zinazofanyakazi na watoto na wanawake ili kuboresha ushirikiano na utekelezaji wa majukumu haya. 

71.     Mheshimiwa Spika, katika kuendelea kujenga mazingira wezeshi na kuboresha uratibu wa mashirika haya, Wizara yangu itatekeleza mambo mbalimbali katika kipindi cha mwaka 2014/2015. Kazi hizo ni pamoja na kufuatilia na kutathmini mchango wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na hali ya uendeshaji wa mashirika hayo hapa nchini.Aidha, itawezesha kufanyika kwa tathmini kuhusu ufanisi wa Sera ya Taifa ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika kujenga mazingira wezeshi kwa NGOs. Vilevile, Serikali kupitia Wizara yangu itawezesha kufanyika kwa mafunzo ya ndani kuhusu usajili, ufuatiliaji na tathmini ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii wa wilaya na mikoa kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kiutendaji ili kuboresha utoaji wa huduma za usajili na uratibu katika ngazi  husika.

Uratibu wa Sera na Mipango

72.     Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/14 uratibu na mapitio ya Sera ya Maendeleo ya Mtoto ya mwaka 2008 pamoja na mkakati wake ulifanyika. Katika mwaka 2014/15, uratibu wa mapitio ya Sera ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ya mwaka 2001 na tathmini ya utekelezaji wa Sera ya Wanawake na Jinsia ya mwaka 2000 na Sera ya Taifa ya Mashirika Yasiyo Ya Kiserikali ya mwaka 2001utafanyika. Aidha, uratibu wa mipango na bajeti ya mwaka 2015/16 pamoja na uandaaji wa mfumo wa ufuatiliaji na tathmini wa Wizara utaandaliwa ili kuimarisha ukusanyaji, uhifadhi na usimamizi wa takwimu na taarifa za sekta ya maendeleo ya jamii. Watumishi 20 wa Wizara watajengewa uwezo wa ukusanyaji takwimu, ufuatiliaji na tathmini.


Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu

73.     Mheshimiwa Spika, watumishi ni rasimali muhimu yenye kutekeleza majukumu ya kila siku ya Wizara. Kutokana na umuhimu wake inahitaji kusimamiwa vizuri, kujengewa uwezo wa kiutendaji na mazingira mazuri ya kazi ili kuongeza ufanisi na tija. Katika mwaka 2013/2014, Wizara iliwezesha watumishi 62 kupata mafunzo ya muda mrefu na mfupi, ndani na nje ya nchi ili kuwaongezea ujuzi na utaalamu katika utekelezaji wa majukumu yao. Katika mwaka 2014/15, Wizara yangu itaendelea kuwawezesha watumishi 84 kupata mafunzo mbalimbali ya muda mfupi na mrefu ndani ya nchi.

74.     Mheshimiwa Spika, katika kuwapatia motisha wafanyakazi, Wizara yangu kwa mwaka 2013/14, ilipandisha vyeo watumishi 126 na kuwabadilisha kada watumishi wanne. Aidha, watumishi 86 walithibitishwa kazini. Kwa kipindi cha mwaka 2014/15, Wizara itaendelea kuwapandisha vyeo watumishi wake kwa mujibu wa Miundo ya Utumishi wa Kada zao na Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma ili kuongeza tija katika utendaji kazi.

75.     Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imekuwa ikikabiliwa na upungufu mkubwa wa watumishi hasa katika Vyuo vya Maendeleo ya Jamii na Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi. Katika kukabiliana na changamoto hii mwaka 2013/14, Wizara yangu iliajiri jumla ya watumishi 92 kutokana na kibali cha ajira kilichotolewa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma chenye Kumbukumbu Namba BC.62/97/014/11 cha tarehe 4 Juni, 2012. Kwa mwaka 2013/14 Wizara iliwasilisha maombi ya kibali cha ajira ya watumishi 603. Katika mwaka 2014/15, Wizara inatarajia kuendelea kuajiri watumishi wengine ili kuendelea kupunguza pengo lililopo.

76.     Mheshimiwa Spika, katika kuboresha mazingira ya utendaji kazi kwa watumishi, mwaka 2013/14, Wizara iliwapatia watumishi vitendea kazi mbalimbali. Kwa mwaka 2014/2015, Wizara yangu itajenga eneo la kuegesha magari la Makao Makuu ya Wizara, kununua jenereta na kuendelea kuwapatia wafanyakazi vitendea kazi mbalimbali.  Aidha, Wizara itawawezesha watumishi kushiriki katika mashindano ya SHIMIWI ili kuboresha afya na kuimarisha mahusiano miongoni mwa watumishi wa Serikali.

77.     Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/14, Wizara yangu iliendelea kuwezesha sekta binafsi za ulinzi na usafi kutoa huduma hizo kwa Wizara kwa lengo la kuboresha mazingira ya utendaji kazi na usalama wa vifaa na mali. Katika mwaka 2014/15, Wizara itaendelea kuwezesha sekta binafsi kutoa huduma hizo.

78.     Mheshimiwa Spika, Wizara yangu iliendeleza mapambano dhidi ya UKIMWI na Virusi Vya UKIMWI mahala pa kazi. Katika mwaka 2013/14, Wizara iliwapatia watumishi nasaha za namna ya kujikinga na maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI. Katika mwaka 2014/15, Wizara itaendelea kuhamasisha watumishi wajitokeze kupima afya zao pamoja na kuwapatia huduma ya viini lishe na chakula.

Mawasiliano kwa umma

79.     Mheshimiwa Spika, mawasiliano ni nguzo muhimu katika kuwawezesha wananchi kufahamu huduma zinazotolewa na Wizara na pia kuiwezesha kupata mrejesho kutoka kwa wadau ili kuboresha huduma hizoKwa mwaka 2013/2014, Wizara yangu iliandaa vipindi vya luninga, radio na mikutano na waandishi wa habari kwa ajili ya kuelimisha umma kuhusu masuala ya maendeleo ya jamii, jinsia, wanawake, familia, haki za watoto na uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali. Aidha, Wizara iliandaa matangazo mbalimbali kupitia magazeti, vipeperushi na mabango.

80.     Mheshimiwa Spika, Katika mwaka 2013/14, Wizara pia ilianzisha mawasiliano na umma kupitia mitandao ya kijamii. Mitandao hiyo ni pamoja na: Blog ya wizara,www.maendeleoyajamiijinsianawatoto.blogspot.com; Facebook ya wizara,facebook.com/maendeleoyajamii; na twitter ya wizara, Twitter.com/wmjjwtz. Kwa mwaka 2014/2015, Wizara itaandaa mkakati wa mawasiliano na kuendelea kuwezesha mawasiliano kwa umma kupitia njia mbalimbali ikiwemo mitandao ya kijamii, radio, luninga, magazeti, gari la sinema, majarida, vipeperushi na uhamasishaji jamii kwa kushirikiana na Maafisa Maendeleo ya Jamii katika ngazi ya kata, wilaya na mkoa.

E:  HITIMISHO

81.     Mheshimiwa Spika, mapitio ya utekelezaji wa Mpango wa Wizara wa mwaka 2013/14 na Malengo ya mwaka 2014/15 yanaonesha jinsi Wizara yangu ilivyo na umuhimu katika kuleta usawa wa jinsia, upatikanaji wa haki na ustawi wa watoto, ongezeko la ajira kwa vijana na ushawishi wa jamii katika kupokea na kutekeleza miradi ya maendeleo endelevu. Ili Wizara itekeleze vema majukumu yake inahitaji ushirikiano mkubwa wa wadau mbalimbali na rasilimali fedha za kutosha.
F:     SHUKRANI

82.     Mheshimiwa Spika, napenda sasa kumshukuru sana Naibu Waziri, Mheshimiwa Dk. Pindi Hazara Chana (Mb.), kwa ushirikiano, ushauri na usaidizi mkubwa anaonipa katika kuongoza Wizara hii. Vilevile, napenda kutoa shukrani za dhati kwa: Katibu Mkuu, Bibi Anna Tayari Maembe, Naibu Katibu Mkuu, Bibi Nuru H. M. Millao; Wakurugenzi; Wakuu wa Vitengo; Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Wanawake Tanzania - Bibi Magreth Chacha; Wakuu wa Vyuo; na Wafanyakazi wote wa Wizara yangu wa ngazi zote, kwa jitihada zao katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara, ambayo ni pamoja na kuniwezesha mimi kuwasilisha hotuba hii mbele ya Bunge lako tukufu.

83.     Mheshimiwa Spika, kabla sijamaliza hotuba yangu, sina budi kuwashukuru wadau wote tunaofanya nao kazi na wengine ambao kwa namna moja au nyingine tunashirikiana. Peke yetu kama Wizara tusingefikia mafanikio niliyoyataja. Naomba kupitia Bunge lako tukufu, kutoa shukrani zangu za dhati  kwa wafuatao: Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Asasi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA); Mfuko wa Fursa Sawa kwa Wote (EOTF); Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP); Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA); Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA); Shirikisho la Vyama vya Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (FAWETA); Medical Women Association of Tanzania (MEWATA); White Ribon; Plan International; Save the Children; Mashirika mbalimbali yasiyo ya Kiserikali pamoja na wale wanaofanya kazi kwa maslahi ya jamii kwa namna moja au nyingine.

Napenda pia kuyashukuru Mashirika kutoka nchi rafiki ambayo yameendelea kutusaidia na kufanya kazi na sisi. Mashirika hayo ni pamoja na: DFID; GPE; CIDA; KOICA na UK Education. Aidha, nayashukuru Mashirika ya Umoja wa Mataifa ambayo ni: UNICEF; UNDP; UNFPA na UN WOMEN kwa misaada yao mbalimbali iliyofanikisha utekelezaji wa majukumu mengi ya Wizara yangu.

G.  MAKADIRIO YA BAJETI YA WIZARA MWAKA 2014/15

84.     Mheshimiwa Spika, ili Wizara yangu iweze kutekeleza majukumu na malengo yake kwa mwaka 2014/15, sasa naliomba Bunge lako tukufu liidhinishe matumizi ya shilingi 30,233,474,000. Kati ya maombi haya:
(a)      Shilingi 21,215,930,000 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida;
(b)     Shilingi 12,818,434,000 ni kwa ajili ya mishahara;
(c)      Shilingi 8,397,496,000 ni kwa ajili ya matumizi mengineyo;
(d)     Shilingi 9,017,544,000 ni kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo ambapo shilingi 7,000,000,000 ni fedha za ndani na shilingi 2,017,544,000 ni fedha za nje.

85.     Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

No comments:

Post a Comment