Katibu wa vijana wa CCM mkoa wa Iringa Halawi Haidaria akizungumza
Baadhi ya viongozi wa ccm wakiwa katika picha ya pamoja sambambana picha za waasisi wa muungano katika ngome ya mkwawa iliyoko Kalenga.
Baadhi ya washiriki wa mbio za pikipiki wakijiandaa kuanza mbio hizo.
Seki Kasuga akizungumza kuhusu umuhimu wa Serikali mbili
Na Denis Mlowe, Iringa
KATIKA kuhakikisha Chama cha Mapinduzi kimedhamiria kupitisha serikali mbili katika bunge maalum la katiba, Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) wako katika harakati za kuhamasisha wananchi kukubaliana serikali mbili ambazo wamekuwa wakitumia mbio za pikipiki kueneza ujumbe huo kwa kutumia jumuiya ya vijana wa chama hicho.
Akihutubia katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Stand ya Mlandege juzi,Kiongozi wa mbio za pikipiki kitaifa, Hassan Bamboko alisema lengo za mbio hizo ni kufikisha ujumbe wa chama hicho kwa wananchi kuwa serikali mbili ndizo zitakazopitishwa na chama hicho na kuwataka wananchi kuuwanga mkono katika harakati hizo.
Alisema licha ya kuhamasisha ujumbe wa serikali mbili ambao wananchi wengi wamekuwa wakiukataa mbio hizo zinatumika kuadhimisha miaka 50 ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar ambao nao uko mashakani kutokana na chama cha mapinduzi kuendelea kung’ang’ania serikali 2 badala ya tatu ambazo ni chaguo la wengi.
"Mbio hizi za pikipiki tunaenda nazo nchi nzima lengo nikuwaeleza wananchi kuwa serikali mbili zinatosha wanaotaka tatu wanauchu wa madaraka na ni mzigo kwa kweli na nawaomba muelewe hili kutokana na ni ya chama cha mapinduzi kwa wananchi wake kuwa ni nzuri katika kulinda usalama wa nchi" alisema Bamboko na kuongeza kuwa tuna miaka 50 tukiwa na Muungano wa serikali mbili licha ya kuwa na kasoro zilikuwa chache na kuongezeka zinaweza kurekebishwa na hakika serikali mbili zinatosha" alisisitiza.
Kwa upande wake kiongozi mwingine wa mbio za pikipiki,Seki Kasuga alisisitiza kuwa serikali mbili ndio mustakabali wa Watanzania katika maisha ya mbele na wanaotaka kuugawa Muungano watafute kwanza udongo uliochanganywa ili ugawanywe.
Naye Katibu wa ccm wilaya ya Mufindi Miraji Mtaturu akizungumzia kuhusu muundo wa Serikali Tatu alisema Chadema wanatumiwa na magaidi wa nchi za nje kutaka serikali tatu ili kuwavuruga wananchi.
Aliwataka wananchi kumfikishia ujumbe Mwenyekiti wa Ukawa, Freeman Mbowe kuwa serikali tatu haikubaliki kwa Watanzania hivyo wanajidanganya kwa kuwa mwarubaini wa maendeleo ya Watanzania ni serikali mbili na sio tatu kama zinazoshinikizwa na wapinzani.
Na Katibu wa vijana wa CCM mkoa wa Iringa Halawi Haidari mwenyeji wa Zanzibar, alisema Wazanzibar wanautambua Muungano wa Serikali mbili hivyo hawawezi kutoka katika Muungano kwa sababu Wazanzibar wapo huru kuishi popote katika ardhi ya Tanzania
Alisema kuwa muungano ukivunjika na kufikia hatua ya mgawanyiko watambue kuwa hata Unguja na Pemba navyo vitagawanyika kwa sababu leo wamedai hati ya Muungano wa Watanzania mwisho watataka hati ya Unguja na Pemba lakini Wazazibar hawakubali msimamo wa serikali tatu.
Katika mbio hizo vijana hao walikabidhi kwa kaimu mkuu wa wilaya ya Iringa, Gerald Guninita picha ya Rais wa kwanza wa Tanzania mwalimu Julius Kambarage Nyerere na picha ya Rais wa kwanza wa Zanzibar Shekhe Abeid Amani Karume pamoja na mabango mawili moja likiwa na ramani ya Tanzania na lingine likiwa na ujumbe maaulum wa mbio hizo unaosema, miaka 50 ya Muungano, “Dumisha Muungano vijana tutumie fursa zilizopo kwa maendeleo yetu, Tanzania kwanza mengine baadae.
No comments:
Post a Comment