TANGAZO


Friday, April 18, 2014

Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Idd atembelea maonesho ya kuadhimisha miaka 50 ya Muungano wa Tanzania


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi akiangalia Vibuyu na Chungu halisi vilivyotumiwa na Baba wa Taifa Marehemu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kuchanganya Udongo kuashiria Kuunganisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Vitu hivyo vimewekwa katika Banda la Ofisi ya Makamu wa Rais wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Maonyesho ya Kuadhimisha Miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yanayoendelea katika Viwanja vya Mnazi Mmoja Mjini Dar es Salaam.
Balozi Seif akiperuzi na kuangalia baadhi ya Machapisho yaliyoandikwa katika Gazeti Rasmi la Serikali kuhusu harakati za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kati kati ya  miaka ya Sitini.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akikagua Siwa maarufu { Rungu } linalotumika katika Shughuli za Kuendesha Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania lililowekwa kwenye Banda la Maonyesho ya Miaka 50 ya Muungano wa Tanzania Mnazi Mmoja Jijini Dar es salaam.

Ofisa wa Huduma wa Kitengo cha Kodi ya Thamani { VAT } kutoka Wizara  ya Fedha za Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Ndugu Saleh Haji Pandu akimueleza Balozi Seif mfumo mzima wa Utendaji kazi wa Kitengo hicho Bara na Zanzibar kwenye Maonyesho ya Miaka 50 ya Muungano wa Tanzania. (Picha zote na Hassan Issa – OMPR – ZNZ)

Na Othman Khamnis Ame, OMPR
 
LICHA ya baadhi ya Wabunge wa Upinzani wa Bunge Maalum  la Katiba kuamua kususia kuendelea kushiriki katika mjadala wa Rasimu ya Katiba iliyowasilisha ndani ya Bunge hilo Kundi kubwa la Wajumbe hao waliobaki wataendelea kuchapa kazi waliyotumwa na Wananchi bila ya kujali uwamuzi uliochukuliwa na wale walioamua kutoka nje ya mjadala huo.
 
Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ambae pia ni Mbunge wa Bunge hilo Maalum la Katiba Balozi Seif Ali Iddi mara baada ya kutembelea baadhi ya Mabanda ya Maonyesho katika Viwanja vya Mnazi Mmoja Mjini Dar es salaam ikiwa ni shamra shamra za Maadhimisho ya kutimia Miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar wa Mwaka 1964.
 
Balozi Seif alisema Kundi hilo lililobakia ndani ya Bunge hilo halitatetereka kamwe na litatekeleza wajibu wake na lina uwezo kamili wa kukamilisha kazi hiyo kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za Bunge hilo Maalum la Katiba na baadaye kuipeleka kwa Wananchi kwa ajili ya kupigiwa kura ya maoni.
 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameelezea masikitiko yake na kuvunjwa moyo kutokana na kitendo hicho kilichoibuka ndani ya Bunge hilo ambacho hakionyeshi uungwana wala uvumilivu na kinaonesha muelekeo wa kuwanyima haki ya Kidemokrasia Watanzania.
 
“ Kundi lililobakia ndani ya Bunge Maalum la Katiba ni kubwa na lina uwezo wa kutekeleza kazi hiyo muhimu katika Historia ya Tanzania kwa mujibu wa Sheria na Kanuni zetu tulizojipangia kwa  pamoja sisi na wale walioamua kuukimbia mjadala huo “, alifafanua Balozi Seif.

No comments:

Post a Comment