Mwendesha mashata wa serikali nchini Afrika Kusini ameanza kumhoji mwanariadha mlemavu Oscar Pistorius ambapo amemtaka akiri kumuua mpenziwe Reeva Steenkamp mwaka uliyopita.
Akimhoji Pistorius wakati wa siku yake ya tatu ya kutoa ushahidi Gerrie Nel alimtaka Pistorius kukubali kumuua mpenziwe nyumbani kwake februari tarehe 14.
Pistorius hata hivyo alijibu kwa kusema kuwa alikuwa amefanya makosa na hakutarajia kumuua Reeva Steenkamp .
Mwanaridha huyo amesema kuwa alifyatua risasi zilizomuua mpenziwe akidhani kuwa ni jambazi aliyekuwa amevamia nyumba yake.
Awali Oscar Pistorius alielezea hali ilivyokuwa punde baada ya kumpiga risasi mpenziwe wa kike Reeva Steenkamp nyumbani kwake.
Wakati wa ushahidi wake wenye majonzi mengi Mwanariadha huyo alisema kuwa Steenkamp alifariki mikononi mwake hata kabla ya gari la wagonjwa mahututi halijafika.
Alisema alijaribu kumsaidia ili apumue huku akizuia damu kububujika zaidi kutoka kiunoni mwake.
Viongozi wa mashtaka wana imani kuwa alimuuwa kimakusudi ndani ya choo chake kwenye bafu baada ya kuzozana.
Mwanariadha huyo mlemavu mwenye umri wa miaka 27, ambaye hana miguu yake yote mawili, huenda akahukumiwa jela maisha iwapo atapatikana na kosa la kuuwa.
Siku ya Jumanne, alilia kizimbani alipokuwa akielezea yaliyojiri nyumbani kwake kabla na baada ya mauwaji hayo.
Iwapo hatapatikana na hatia ya kukusudia kuua Reeva ,basi kulingana na sheria za Afrika Kusini ,Pistorious huenda akashtakiwa kwa kosa la kuua bila ya kukusudia ambayo hukumu yake ni kati ya miaka 6- 15 jela.
Mbali na shtaka la mauaji, Pistorius anakabiliwa na shtaka la kufyatua bunduki hadharani na shtaka lingine la kumiliki risasi kinyume na sheria.
No comments:
Post a Comment