TANGAZO


Saturday, March 1, 2014

Ujenzi wa mitambo ya kusafisha gesi kuanza mwezi Machi

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi

Na Teresia Mhagama

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi ameeleza kuwa ujenzi wa mitambo ya kusafisha gesi asilia katika kijiji cha Madimba mkoani Mtwara utaanza mwezi watatu mwaka huu.

Katibu Mkuu aliyasema hayo mbele ya viongozi wa dini wa Mikoa ya Lindi na Mtwara waliofika katika eneo la ujenzi wa mitambo hiyo juzi, ili kupata elimu ya shughuli zitakazofanyika katika eneo hilo na kujionea maendeleo ya ujenzi wa nyumba za wafanyakazi watakaoishi katika eneo hilo ili kuendesha mitambo ya kusafisha gesi asilia.

Katibu Mkuu alieleza kuwa ili kuhakikisha ajira zinabaki maeneo ambayo gesi inazalishwa Serikali imeamua mitambo ya kusafisha gesi asilia ijengwe katika maeneo hayo.

Alieleza kuwa mitambo hiyo katika eneo la Madimba itakuwa na uwezo wa kusafisha gesi asilia futi za ujazo milioni 210 kwa siku na itatoka katika eneo la Mnazi Bay, Ntorya na bahari ya kina kirefu.

Katibu Mkuu alieleza kuwa kukamilika kwa mitambo hiyo kutaiwezesha Serikali kuzalisha umeme wa uhakika na hivyo kuondokana na gharama kubwa zinazotokana na ununuaji wa mafuta ya kuendeshea mitambo ya umeme ambayo inaigharimu Serikali kiasi cha shilingi trilioni 1.6 kwa mwaka.

Naye mtaalamu wa masuala ya gesi kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC), Sultan Pwaga aliwaeleza viongozi hao wa dini kuwa mitambo mingine yenye uwezo wa kusafisha gesi asilia kiasi cha futi za ujazo milioni 140 kwa siku itajengwa katika kijiji cha Songosongo, Mkoa wa Lindi na itasafisha gesi asilia itakayozalishwa katika eneo la Songosongo, Kiliwani na maeneo ya jirani.

Mtaalamu huyo kutoka TPDC alieleza kuwa usimikaji wa mitambo ya kusafisha gesi katika eneo hilo, unatarajiwa kukamilika mwanzoni mwa mwezi Desemba mwaka huu na majaribio ya mitambo hiyo yataanza mwezi Januari, mwaka 2015.

Bw. Sultan Pwaga, aliwaeleza viongozi hao, kuwa katika eneo hilo kutajengwa mitambo ya kusafishia maji ambapo kijiji cha Madimba kitapatiwa maji safi kiasi cha lita 60,000 kwa siku.

Kuhusu ajira, Bw. Pwaga alieleza kuwa ujenzi wa mitambo ya kusafisha gesi katika eneo hilo, umetoa ajira kwa Watanzania wapatao 351 na raia wa kigeni wasiozidi 35.

Kongamano la viongozi wa dini wa mikoa ya Lindi na Mtwara limefanyika tarehe 25 na 26 mkoani Mtwara na ambapo Wizara ya Nishati na Madini na Taasisi  zake za Wakala wa Nishati vijijini (REA), Shirika la Umeme nchini (TANESCO) na Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) zilishiriki ili kutoa elimu na ufafanuzi wa masuala mbalimbali yanayohusu sekta za Nishati na Madini.

No comments:

Post a Comment