TANGAZO


Tuesday, March 4, 2014

Suala la Jinsia Laibua Mjadala ndani ya Bunge Maalum la Katiba, mjini Dodoma

Mwenyekiti wa Muda wa Bunge Maalum la Katiba, Pandu Ameir Kificho akifafanua jambo wakati akikiendesha kikao kilichokaa kama semina kupitia Rasimu ya Kanuni za bunge hilo, mjini Dodoma leo. (Picha zote na Kassim Mbarouk-www.bayana.blogspot.com)
Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Zanzibar, Othman Masoud Othman, akifafanua moja ya kifungu cha Sheria, wakati wa kujadili vipengele vya Rasimu ya Kanuni za bunge hilo, mjini Dodoma leo.

Na Jovina Bujulu
 
SUALA la Jinsia katika uongozi wa Bunge Maalum la Katiba limeibua Mjadala mzito katika nafasi ya Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa bunge hilo.

Mjumbe wa Bunge hilo Lediana Mung’ong’o ndiye aliyekuwa wa kwanza kuibua suala hilo wakati wa mjadala kuhusu marekebisho ya kanuni za bunge kipengele 8(i) kinachozungumzia utaratibu wa kumchagua Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti katika kikao kilichoketi leo bungeni mjini Dodoma, kama semina kujadili Rasimu ya Kanuni za bunge hilo.

Mung’ong’o alitaka kipengele hicho kuzingatia uhusiano wa kijinsia, ambapo kama mwenyekiti atakuwa ni mwanaume, makamu wake awe mwanamke au kama Mwenyekiti atakuwa mwanamke, makamu wake awe mwanaume.

“Mwenyekiti hili suala la Mwenyekiti na Makamu wake hatuna budi kuangalia suala la jinsia kwamba ikiwa mwenyekiti atakuwa ni mwanaume, makamu wake awe mwanamke au kama Mwenyekiti atakuwa mwanamke, makamu wake awe mwanaume” alisema Mung’ong’o.

Naye Mjumbe wa Bunge hilo Anna Abdalah alisema kuwa suala hilo lilikosewa Tangu awali hivyo hakuna budi makubaliano yafanyike kwa busara maana wanawake wenye sifa na uwezo wapo wengi Tanzania Bara na Zanzibar.

Akichangia katika suala hilo Mjumbe wa Bunge Hilo ambaye ni Naibu Waziri Wizara ya Fedha Adam Malima alisema kuwa ili kuwepo kwa amani na Mshikamano sheria haina budi kusema wazi endapo Mwenyekiti atatoka Tanzania Bara basi Makamu wake atoke Zanzibar.

Akijibu hoja hiyo Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Othman Masoud Othman alisema kuwa suala hilo liwe la marekebisho lakini si kwa kuvunja sheria hiyo.


“Sharti hilo likibadilishwa litakuwa ni kituko na tutakuwa tunarekebisha sheria ambazo hazikutungwa na Bunge Maalum la Katiba hivyo ni busara kufanya makubaliano ili kufikia muafaka wa jambo hilo" alisema Othman Masoud Othman.

No comments:

Post a Comment