TANGAZO


Tuesday, February 25, 2014

Wanamgambo waua wanafunzi Nigeria


Wanamgambo wa Boko Haram

Wanamgambo wa Kiislam wa kundi la Boko Haram kaskazini mashariki mwa Nigeria wametuhumiwa kushambulia shule moja na kuwaua wanafunzi kadhaa.
Polisi nchini Nigeria wameliambia Shirika la Habari la Uingereza, Reuters kwamba wote waliouawa ni wavulana na kwamba baadhi ya miili ya wanafunzi hao imeungua na kubaki majivu.

Taarifa ya jeshi la Nigeria imesema shambulio hilo limefanyika katika jimbo la Yobe.
Wakaazi wa mji wa Buni Yadi katika jimbo hilo, wamesema washambuliaji hao walivamia usiku na kuwachinja baadhi ya wanafunzi.
Wamesema baadhi waliuawa kwa kupigwa risasi.
Walimu katika chuo cha serikali ya shirikisho katika mji wa Buni Yadi wameliambia shirika la habari la AP kwamba wanafunzi wapatao 40 waliuawa katika shambulio hilo ambalo lilianza mapema Jumanne asubuhi.
Jeshi limethibitisha kwamba shambulio hilo limetokea katika hosteli za wanafunzi lakini limesema haliwezi kutoa taarifa zaidi kwa sasa.
Kundi la Boko Haram limekuwa likishutumiwa kuendesha vitendo vya mauaji kaskazini mwa Nigeria, yakiwemo mauaji ya mapema mwezi huu katika jimbo la Yobe.
Boko Haram, lina maana ya"Elimu ya Magharibi ni dhambi" katika lugha ya Kihausa, mara kwa mara limekuwa likishambulia shule katika siku za nyuma.
Watu kadhaa wameuawa katika mashambulio mawili yaliyotokea wiki iliyopita. Katika tukio moja, wanamgambo hao wa Boko Haram, waliteketeza kijiji kizima na kuwapiga risasi wakaazi wa eneo hilo waliokuwa wakijaribu kutoroka.

No comments:

Post a Comment