TANGAZO


Thursday, February 27, 2014

Mashambulizi ya Boko Haram yakithiri

Jeshi la Nigeria limekosolewa kwa uzembe katika kupambana na Boko Haram
Maafisa wakuu nchini Nigeria wanasema kuwa wapiganaji wa kundi la wanamgambo la Boko Haram, wameshambulia vijiji kadhaa katika jimbo la Adamawa Kaskazini mwa nchi hiyo.
Mwandishi wa BBC, Kaskazini mwa Nigeria, anasema kuwa idadi kubwa ya wapiganaji waliokuwa wamejihami kwa maguruneti, wameripotiwa kuvamia vijiji.
Wakazi wanasema kuwa maduka na nyumba ziliharibiwa.Watu wawili wameripotiwa kuuawa.
Viongozi wa Afrika pamoja na Rais wa Ufaransa,Francois Hollande wanahudhuria mkutano kuhusu usalama barani Afrika mjini Abuja.
Mkutano huu unafanyika wakati Nigeria ikisherehekea miaka 100 tangu kuwa nchi.
Wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo,Rais Goodluck Jonathan ametoa wito kwa mataifa ya Afrika kushirikiana kupambana na ugaidi.
Alisema ugaidi dhidi ya nchi moja ni ugaidi dhidi ya bara zima la Afrika.
Kuna wasiwasi mkubwa nchini Nigeria kuhusu ghasia zinazoendelea Kaskazini mwa nchi.
Wiki hii wanafunzi waliuawa na kundi hilo lilipovamia shule yao ya mabweni.
Zaidi ya watu miatatu wameuawa katika mashambulizi makubwa yaliyofanywa na kundi hilo Kaskazini Mashariki mwa nchi .
Wakati huohuo, Waziri wa maswala ya ndani nchini Nigeria amesema serikali yake haitakataa usaidizi kutoka kwa vikosi vya kulinda amani vya kimataifa ili kukabiliana na wanamgambo wa kundi la Boko Haram.
Patrick Abamoro ameiambia BBC kwamba kwa sasa serikali inaweza kudhibiti ghasia za kundi hilo lakini akakiri kwamba taifa hilo limeomba usaidizi wa kimataifa.
Bwana Abamoro amezungumza baada ya gavana wa jimbo la Yobe Ibrahim Gaidam kuishtumu serikali ya Nigeria kwa kushindwa kuwalinda raia wanaoshambuliwa na kundi la Boko haram .

No comments:

Post a Comment