TANGAZO


Wednesday, February 12, 2014

70 wahusishwa na Al Shabaab Kenya

 

Masjid Musa ni moja ya misikiti inayosemekana kueneza mafunzo ya itikadi kali miongoni mwa vijana.
 
Washukiwa sabini waliokamatwa katika fujo zilizotokea Msikiti Musa Mombasa wameshitakiwa katika mahakama ya Mombasa.
Wanakabiliwa na mashitaka saba yanayohusiana na ugaidi yakijumuishwa kuwa wanachama wa kundi la kigaidi la Al Shabaab na wamewekwa rumande hadi Februari 26 ambako mahakama itatoa uamuzi kuhusu ombi la wakili wao kutaka waachiliwe kwa dhaman.
 
Baada ya kuzuiliwa na polisi kwa takriban siku kumi, washukiwa hao walipelekwa katika mahakama ya Mombasa lakini wakakanusha mbele ya hakimu Richard Odenyo mashitaka saba yanayowakabili.

Mbali na ugaidi washtakiwa hao wanakabiliwa na makosa mengine ya kumiliki silaha kinyume cha sheria, wizi wa kutumia mabavu na uchochezi.

Hao ni miongoni mwa 104 waliokuwa wamezuiliwa ila 33 waliachiliwa jana baada ya serikali kuwaondolea mashtaka ya ugaidi na wizi wa kutumia mbavu kwa kukosekana ushahidi.

Mawakili wa washtakiwa hao Mohammed Balala na Mureithi Mbugua walikuwa wamewasilisha ombi mahakamani kutaka waachiliwe kwa dhamana lakini upande wa mashtaka ukapinga ukisema kuwa walikuwa hatari kwa usalama wa taifa.

Hii ni moja ya kesi ambayo inapigwa darubani zaidi kwa misingi kuwa inazingatiwa serikali imehusisha msikiti Musa kwa kutoa mafunzo ya misimamo mikali miongoni mwa vijana wakiambiwa kuwa ni Jihad ama vita vitakatifu.
Inadaiwa kuwa vijana wanaoshiriki sala katika msikiti huo wamekuwa wakisajiliwa na kuelelekea Somalia kujiunga na kundi la ugaidi la Al Shabab.

Kutokana na kukamatwa kwa washukiwa hao msikitini viongozi wa dini ya kiislamu walishutumu maafisa wa polisi kuingia msikitini na viatu . Watu wawili waliuawa katika makabiliano hayo
Serikali ya Rais Uhuru Kenyatta imeahidi kupambana vilivyo dhidi ya makundi ya vijana wapiganaji wanaosema wanafanya hivyo kwa lengo la kidini.

Kundi la wanamgambo la Al Shabaab lilikiri kufanya mashambulizi ya kigaidi dhidi ya jengo la kifahari la maduka la Westgate na kuwaua wakenya 67 mjini Nairobi mwezi Septemba mwaka jana.

Serikali imesema kuwa haitakubali maeneo ya maombi kutumiwa kama vituo vya kuhubiri itikadi kali za kidini.

No comments:

Post a Comment