TANGAZO


Monday, January 27, 2014

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto yatoa taarifa juu ya Maadhimisho ya miaka 50 ya Chuo Cha Maendeleo ya Jamii- Tengeru

TAARIFA YA MHE. SOPHIA M. SIMBA (MB)
WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA NA WATOTO KWA VYOMBO VYA HABARI JUU YA MAADHIMISHO YA MIAKA 50 YA
CHUO CHA MAENDELEO YA JAMII - TENGERU

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba.


A.           Ndugu Waandishi wa Habari,
Nimewaita kuwafahamisha kuwa mwaka huu, Wizara yetu, inaadhimisha miaka 50 ya Chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru, ambayo yatafanyika kuanzia tarehe 27 Januari 2014 mpaka tarehe 31 Januari 2014.

Maadhimisho hayo yataenda sambamba na Mahafali ya Tatu ya Shahada ya Kwanza; na Mahafali ya Pili ya Shahada ya Uzamili, (Post-graduate Diploma) ambayo yatafanywa Siku ya Kilele cha Maadhimisho haya tarehe 31 Januari, 2014.

B.           Ndugu Waandishi wa Habari,
Chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru kilianzishwa  mwaka 1963. Lengo la kuanzishwa kwa chuo hiki lilikuwa  ni  kutoa wahitimu katika taaluma ya maendeleo ya jamii, ambao watahamasisha jamii kuainisha matatizo/changamoto katika maeneo yao  na kuzitafutia ufumbuzi wao wenyewe kwa kutumia nyenzo na michakato shirikishi.

Awali Chuo hiki kilitoa mafunzo ya Cheti, baadaye Stashahada ya Juu na hivi sasa kimeongeza na kutoa mafunzo ya Shahada ya kwanza, Stashahada ya Uzamili (Post-graduate Diploma) katika fani ya maendeleo ya jamii.

Ambapo kauli mbiu ya maadhimisho haya ni “TAALUMA YA MAENDELEO YA JAMII; NYENZO MUHIMU KATIKA KUKUZA UCHUMI NA KUONDOA UMASKINI WA KAYA”.

Dhima ya kauli mbiu hii ni kutambua mchango wa taaluma ya Maendeleo ya Jamii wa kuwawezesha wananchi katika ngazi ya jamii kubaini matatizo na fursa zilizopo kwa lengo la kupambana na umaskini na kujiletea maendeleo yanayozingatia usawa wa jinsia na haki kwa watoto na watu wenye mahitaji maalumu.
C.           Ndugu Waandishi wa Hahari,
Katika kuadhimisha miaka 50 ya Chuo cha Tengeru, Wizara yangu inajivunia matokeo yafuatayo:-
-          Chuo kimetoa wahitimu zaidi ya 8,000 ambao wapo katika Sekta mbalimbali nchini na wanatumika katika kuwezesha utekelezaji wa Sera, Program, mikakati na kampeni za sekta mbalimbali kwa kutumia mbinu Shirikishi Jamii. (Community Participation), vilevile maafisa jamii hawa wanahamasisha jamii kujiongezea kipato kwa matumizi ya teknolojia sahihi, ujasiriamali n.k.

-          Sekta ya Maendeleo ya Jamii imewezesha wananchi kupokea, kushiriki katika kupokea shughuli za kimaendeleo toka awali kama katika malezi bora, kupeleka watoto shule, kutumia huduma za afya, ujenzi wa nyumba bora za kuishi. Aidha, na katika miaka ya hivi karibuni imehamasisha sana jamii katika ujenzi wa Shule za Sekondari, uendeshaji wa shule, upatikanaji wa madawati, kuchangia na kumiliki program za Maendeleo mbali mbali. Mfano miradi iliyoanzishwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) imekuwa endelevu na jamii nyingi zimeweza kutatua matatizo yaliyokuwa yakiikabili.


-          Kupitia tafiti zilizofanywa na chuo, sekta ya Maendeleo ya Jamii imeweza kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoathiri maendeleo ya wananchi.

-      Wataalamu wa Maendeleo ya Jamii wanaendelea kuhamasisha na kuelimisha jamii kuondokana na mila, fikra potofu na desturi zinazoleta madhara kama vile unyanyasaji wa kijinsia, mauaji ya albino na  ukeketaji wa wanawake, ndoa na mimba  za utotoni.

Dhana ya Maendeleo ya Jamii nguvu yake kubwa ni familia, vikundi na jamii kwa ujumla.  Tokea tulipopata  Uhuru – akina bwana na bibi Maendeleo, wamekuwa wakifanya  uhamasishaji wa matumizi ya  chakula bora kwa familia usafi wa mazingira,  kupambana na ukimwi, kilimo cha kisasa, ujasiriamali nk.  

D.           Ndugu Waandishi wa Habari,
Maadhimisho ya miaka 50 haya yataenda sanjari na Mkutano Mkuu wa mwaka wa Wizara utakaohusisha Maafisa Maendeleo ya Jamii  wa Mikoa na Wilaya kutoka Tanzania nzima wanaofanya kazi katika Halmashauri zetu, Wakuu wa Vyuo vya Maendeleo ya Jamii, Wakuu wa Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi na Wadau wengine.

Hii ni fursa yao ya kujadili mafanikio na changamoto mbalimbali zinazoikabili Sekta ya Maendeleo ya Jamii na kubuni mikakati ya kutimiza azma ya Serikali katika kuwezesha jamii kujiletea maendeleo ili kuondoa umaskini wa wananchi wake.

Vilevile kutakuwa na maonesho  ya kazi za mikono, kutoka katika vikundi vya wanajamii wa  Halmashauri za Arusha na Arumeru. Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) watafanya maonyesho, pia watatoa huduma za afya kwa jamii.

Hivyo, nichukue fursa hii kuwakaribisha wadau na wananchi wote kwa ujumla kushiriki maadhimisho ya miaka 50 ya Chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru.

Nachukua fursa hii, kuwapongeza wanahabari na kuwaomba  muendelee,  kutangaza umuhimu wa Sekta ya Maendeleo ya Jamii, kwa ustawi na maendeleo ya nchi yetu.

Ahsanteni kwa kunisikiliza.

No comments:

Post a Comment