Jeshi la Nigeria limesema kuwa limewaua wapiganaji 38 wa Boko Haram wakati wa mapambano dhidi ya kundio hilo katika eneo la Kaskazini Mashariki mwa nchi.
Msemaji wa jeshi Kanali Muhammad Dule amesema kuwa wanajeshi waliokuwa wanashika doria walitibua njama ya mashambulizi waliyokuwa nayo Boko Haram.
Kwa mujibu wa taarifa ya jeshi, wanajeshi walifanikiwa kuwaua wapiganaji 38 wa Boko Haram huku baadhi wakitoweka na majeraha mabaya.Walitaka kuwashambulia raia na wanajeshi katika eneo la Damboa, jimbo la Borno mapema asubhi ya leo .
Moja ya magari yaliyoharibiwa kwenye makabiliano hayo, lilipatikana likiwa na mitungi ya gesi, pamoja na vifaa vingine vya mashambulizi.
Silaha nyinginezo kama bunduki na risasi zilipatikana.
Mwanajeshi mmoja aliuawa na wengine wawili kujeruhiwa kwenye makabiliano hayo.
Boko Haram, ni kundi linalosemekana kuwa la kigaidi kwa mujibu wa serikali za Marekani na Uingereza na limekuwa likipigana na serikali tangu mwaka 2009, likivamia shule ambazo zinafuata mitaala ya mataifa ya magharibi.
Wapiganaji hao pia wamekuwa wakishambulia shule na makanisa.
Serikali ya Nigeria mwaka jana ilitangaza sheria ya hali ya hatari katika jimbo la Borno, na majimbo mengine ya Yobe na Adamawa, katika juhudi za kukomesha ghasia na mauaji ya raia wasio na hatia.
Lakini juhudi za serikali zingali kuzaa matunda kwani kundi hilo limeendelea kufanya mashambulizi ya mara kwa mara dhii ya raia na taasisi za usalama nchini humo
No comments:
Post a Comment