TANGAZO


Friday, January 17, 2014

Waandamanaji washambuliwa Bangkok

 

Wanajeshi wamekuwa wakipambana na waandamanaji wanaoipinga serikali ya waziri mkuu Yingluck Shinawatra
Watu wapatao ishirini na wanane wamejeruhiwa katika shambulio dhidi ya waandamanaji wanaoipinga serikali mjini Bangkok, Thailand.
Kumekuwa na mashambulio kadha ya kurusha risasi kuelekea katika maeneo yaliyokaliwa na waandamanaji mjini Bangkok kwa zaidi ya wiki moja, lakini mpaka sasa matukio hayo yamekuwa yakitokea usiku, na mara nyingi yalilenga vituo vya ulinzi.
 
Shambulio la leo lililotokea mchana kweupe limehusisha mlipuko-huenda ni gruneti, likiwa limerushwa kutoka ghorofa ya pili ya jengo moja kuelekea katika maandamano yaliyokuwa yakiongozwa na Suthep Thaugsuban katikati ya mji wa Bangkok.
Kiongozi huyo hakujeruhiwa, lakini waandamanaji kadha pamoja na walinzi wa usalama walipigwa na vipande vya gruneti.
Shambulio hilo lilitokea saa moja baada ya msafara wa magari na pikipiki kuwafyatulia risasi waandamanaji wa kundi lingine kaskazini mwa mji mkuu Bangkok.
Mapema wiki hii maafisa wanne wa polisi waliovalia kiraia walikamatwa na walinzi wa waandamanaji na kupigwa vibaya.
Waziri mkuu Yingluck Shinawatra amesema leo kuwa kufanyika kwa uchaguzi aliouitisha ufanyike tarehe Pili Februari ni njia pekee itakayosaidia nchi hiyo kuondokana na vurugu za sasa – amesema serikali imekuwa ikijizuia kwa kiasi kikubwa katika kukabiliana na waandamanaji – lakini ni makundi yaliyojiimarisha kisilaha kwa pande zote mbili hali inayoonyesha kuwa yako tayari kwa mapmabano zaidi.

No comments:

Post a Comment